Bukobawadau

Baraza la wawakilishi laidhinisha kufunguliwa serikali kuu Marekani

Baraza la wawakilishi nchini Marekani limeidhinisha muafaka katika dakika za mwisho za mashauriano ya kufungua tena serikali kuu na kuongeza kiwango cha kukopa ili kuepuka uwezekano wa Marekani kushindwa kulipa madeni yake.
 
Baraza la wawakilishi lili-idhinisha mpango huo Jumatano usiku kwa kura 285 dhidi ya 144 baada ya mswaada kuidhinishwa awali na baraza la Seneti kwa kura 81 dhidi ya 18 .

Rais Barack Obama anasema mara mswaada huo ukifika kwenye meza yake atautia saini haraka na serikali kuu itafunguliwa mara moja. Bwana Obama aliwashukuru viongozi wa vyama vyote na alisema huu ni wakati wa kurudisha imani tulioipoteza kwa watu wa Marekani.

Kiongozi wa walio wengi katika baraza la Seneti, m-Democrat, Harry Reid na mwenzake wa Republican, Mitch McConnell waliuandaa pamoja  mswaada huo Jumatano siku moja kabla ya muda wa  kukopa kumalizika.

Mswada huo utaiwezesha serikali kuu kuendesha shughuli zake hadi angalau Januari 15 na kupandisha kiwango cha kukopa ili kuepuka hatari  ya kushindwa kulipa madeni  hadi angalau Februari 7. Wakati huo huo wabunge watashauriana juu ya kukata matumizi.
Reid aliita kufungwa kwa serikali kuu na hasira kulisababishwa na mzozo wa kutengenezwa ambao umeleta maumivu kwa nchi bila ya sababu nzuri. Kama kiwango cha kukopa kisingeongezwa Marekani ingepoteza mamlaka ya kukopa fedha ili  kuendelea kulipa bili zake.

Serikali kuu ilifungwa Oktoba mosi wakati baraza la Seneti lilipokataa matakwa  ya baraza la wawakilishi la kutofadhili  au kuchelewesha sheria ya huduma ya afya ya Rais Obama maarufu kama OBAMACARE kama sehemu ya mswada wa matumizi. Rais amesema hatojadili mabadiliko yeyote katika sheria hiyo hadi serikali kuu ifunguliwe tena.
 
Spika wa Bunge la Marekani, John Boehner alisema wabunge wa Repuplican walipambana kwa kila kitu walichokuwa nacho ili kulazimisha mashauriano juu ya sheria hiyo maarufu ya OMABACARE. Alisema chama chake kitaendelea kusukuma kuangaliwa tena kwa mswaada huo  na kuzungumzia mapungufu yaliyomo.
Next Post Previous Post
Bukobawadau