Bukobawadau

DOKEZO LA WADAU Bunge linahusika kifungo cha Mwananchi, Mtanzania

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lenye wajibu wa kutunga, kurekebisha na hata kufuta sheria linahusika moja kwa moja katika kuyafungia magazeti ya Mwanahalisi, Mwananchi na Mtanzania. Ndiyo, kuanzia Bunge la Pius Msekwa ambalo lilikuwa na wajibu wa kufuta sheria 40 mbovu (ikiwamo Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976) zilizopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Rais, iliyoongozwa na Jaji Mkuu wa zamani, Francis Nyalali.
Kuendelea kuishi kwa sheria hiyo mbovu, maana yake ni kwamba Bunge limeridhia na pale serikali inapoitumia sheria hiyo, Bunge haliwezi kukwepa lawama na kimsingi, kila mbunge hawezi kukwepa lawama. Kwa kuzingatia dhana ya kiutawala ya checks and balances, Bunge limefeli kutumia madaraka yake kuhakikisha nchi inabaki na sheria zinazokidhi mahitaji ya wakati.
Sikubaliani na wabunge wanaoitupia lawama serikali kwa sababu tu imetekeleza sheria hii, wote wanahusika, serikali pamoja na kila mbunge hadi pale sheria hii itakapofutwa. Unafiki wa baadhi ya wabunge hauwezi kukubalika, unafiki wa kuvifurahia vyombo vya habari pale vinapokidhi malengo yao kisiasa lakini kufunga midomo yao pale vyombo hivyo vinapofungiwa kwa sheria ambayo wanaweza kuifuta.
Kwa mwenendo huu ya kufungia vyombo vya habari wakati wowote, ni vigumu pia kukubaliana moja kwa moja na mawazo ya Rais wa 16 wa Marekani, Kapteni Abraham Lincoln, kijana wa Mzee Thomas na Mama Nancy, kwamba namna pekee ya kuelekea kufutwa kwa sheria mbaya ni kuitumia sheria hiyo mbaya kikamilifu (The best way to get a bad law repealed is to enforce it strictly). Kwamba sheria mbaya inapotumika ndipo wengi huweza kuichukia zaidi na hivyo shinikizo la kutaka ifutwe kuzidi na hatimaye sheria husika kufutwa, tukitumia msemo huo, tutazidi kuumia zaidi katika suala hili la sheria ya magazeti ya mwaka 1976.
Ni vigumu kutumia mtazamo huo ili hatimaye Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 ifutwe, sheria ambayo inaigeuza serikali kuwa mlalamikaji mwenye kupanga na kutangaza hukumu dhidi ya magazeti. Hii ni sheria kandamizi, kuzidi kuitumia zaidi na zaidi kama ulivyo mtazamo wa Lincoln si uungwana.
Sheria hii imekwishasababisha madhara dhidi ya wanataaluma kadhaa wa tasnia ya habari, achilia mbali wamiliki na makundi mengine ambayo shughuli zao za kiuchumi zinaingiliana na uwepo wa magazeti nchini. Kwa miaka kadhaa sasa, sheria hii ya magazeti ya mwaka 1976 imelalamikiwa na kupingwa. Hata hivyo, kwa bahati mbaya mno, watunga sheria wetu ambao wanapaswa kuwa wawakilishi wa Watanzania, kuanzia katika majimbo yao hadi ngazi ya kitaifa, hawaoni ubaya wa sheria hii, wamebweteka, wamekaa kimya.
Je, wabunge wetu wanafurahia sheria hii? Kama hawafurahii wamefanya nini kuipinga? Tukianzia katika Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria- je, kamati hii inafanya kazi yake vizuri kwa niaba ya Bunge? Katika uhai wake, kamati hii inaweza kujivunia kufanikisha ushauri wa aliyepata kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Francis Nyalali wa kufuta sheria takriban 40 kandamizi nchini?
Je, wabunge (wasio wajumbe wa kamati ya Katiba na Sheria) wanajua mpango kazi wa kamati hii ambayo kwa bahati nzuri orodha ya sheria mbovu zisizofaa kuendelea kuwapo nchini ilikwishawekwa hadharani na Jaji Mkuu Nyalali?
Kuendelea kuwapo na kutumika kwa Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 maana yake ni Bunge kushindwa kufanya kazi yake vizuri katika dhana ya checks and balances. Katika nchi yenye mgawanyo wa mihimili mitatu yenye wajibu wa kusimamiana, Bunge limefeli. Rafu zinazofanywa na serikali kupitia sheria hii dhidi ya magazeti zinapaswa kudhibitiwa na Bunge lakini kwa bahati mbaya, Bunge limefeli katika eneo hili mahsusi.
Bunge ndilo linalopaswa kusukuma kuondolewa kwa sheria ya magazeti ya mwaka 1976, na kwa hiyo, hapa mchawi wa kwanza si yule anayetekeleza sheria inayomfaidisha, bali mchawi namba moja ni yule mwenye uwezo wa kuizuia na hata kufutilia mbali sheria husika. Mchawi huyo ni Bunge. Kwa watu werevu, katika sakata hili wabunge ndiyo wa kung’ang’aniwa. Serikali haiwezi kukubali kujipunguzia nguvu zake bila kushinikizwa na chombo sahihi ambacho ni Bunge.
Kuendelea kuwapo kwa sheria hii ni ushuhuda mwingine wa namna ambavyo Bunge kwa ujumla wake linavyosinzia katika kutimiza wajibu wake katika dhana ya checks and balances. Tumuulize Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, anaweka mchango gani kwa nafasi yake kama mbunge? Tumuulize, Naibu Spika, Job Ndugai, anafurahia sheria hii. Tumuulize Spika Anne Makinda, Bunge linatimiza wajibu wake ipasavyo kwa kuendelea kuwapo kwa sheria hii?
Kuendelea kuomba huruma ya serikali katika kuifuta sheria hii ni sawa na kutekeleza makosa mengine. Serikali haiwezi kuwa na huruma kwa kiwango hicho cha kujipunguzia mabavu yake. Lazima tubadili mwelekeo, na kwa kweli, mwelekeo ni katika Bunge linalopaswa kutengeneza mfumo wa sheria unaohakikisha uwapo wa mustakabali bora wa nchi.
Kila mwananchi mpenda haki amhoji mbunge wake kama anaridhika na sheria hii, haitoshi kuendelea kulalamika katika vipindi vya televisheni au mikutano ya hadhara dhidi ya serikali wakati, watu wanaotambulika kama wawakilishi wetu wapo, tuwasukume wafanye kazi yao. Hatuwezi kuendelea kusubiri magazeti zaidi yafungiwe ili ubaya wa sheria hii uzidi kuwa dhahiri, kama ambavyo Lincoln anavyowaza.
Bila kujali makosa au usahihi wa magazeti yaliyofungiwa, tatizo la msingi hapa limegawanyika katika maeneo makubwa mawili. Mosi, ni Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 na pili, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao ndiyo wenye jukumu la kutunga sheria na hata kufuta sheria. Ili Bunge lisiendelee kuwa tatizo na wabunge wasionekane tatizo, wafute sheria hii.
Ujumbe pekee unaojitokeza katika uamuzi huu wa Septemba 27, mwaka 2013 wa kulifungia gazeti la Mwananchi siku 14 na gazeti la Mtanzania siku 90 ni kwamba, Bunge limefeli katika kutimiza wajibu wake, hasa ikizingatiwa kwamba, tukio hili lilitanguliwa na kifungo dhidi ya gazeti la kila wiki la Mwanahalisi. Endapo Bunge lingetimiza wajibu wake, basi, sheria hii ingefutwa.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
Chanzo;Raia mwema
Next Post Previous Post
Bukobawadau