Bukobawadau

Heko vyombo vyetu kuyazima mazoezi ya ugaidi

Na Prudence Karugendo
 Habari za hivi karibuni kuwa polisi imewakamata vijana 11 katika msitu mmojawapo mkoani Mtwara wakifanya mazoezi ya ugaidi imewashtua sana baadhi ya wananchi, wananchi walikuwa wakiamini kwamba hicho ni kitu ambacho kisingeweza kutokea hapa Tanzania. Hiyo ni kutokana na kuizoea sana amani wakiichukulia kama sehemu ya urithi wao ambao haupaswi kuguswa na mtu yeyote! Ukweli ni kwamba kuyaendekeza mawazo ya aina hiyo ni kujidanganya kabisa na kujiweka katika hali isiyotabirika, sababu amani ni matunda ya umakini wa watu wa sehemu husika, kuzembea kidogo tu na kuusahau umakini kunaweza kuifanya amani inayoonekana ipotee na kusahaulika kama iliwahi kuwepo. Mfano shambulio la kigaidi lililotokea katika jumba la biashara la Westgate Shopping Mall Jijini Nairobi, nchini Kenya, limeonyesha mengi ambayo yalikuwa yamejificha kwenye mazoea tuliyo nayo. Kwa bahati mbaya mazoea waliyo nayo Wakenya kwa kiasi fulani yamefanana na mazoea ya Watanzania, au niseme mazoea ya watu wengi wa nchi za kanda hii inayoihusisha hata na Kenya yenyewe. Kutokuzoea matukio mabaya, kama hayo ya kigaidi yaliyotokea Westgate, Nairobi, kumetufanya wakazi wa eneo hili ikiwemo Kenya, kubweteka na kuimba nyimbo za amani na utulivu huku tukiichukulia amani hiyo kama moja ya mazao tunayoyazalisha. Kinachosahaulika ni kwamba amani tunaweza kuwa nayo kweli, bila kukumbuka kuwa hicho ni kitu kinachokuja kwa kudra za Mwenyezi Mungu bila sisi kujihangaisha sana kukitafuta. Nitoe mfano mwingine kuhusu niliyosimuliwa na rafiki yangu aliyetembelea nchi ya Israel. Rafiki yangu huyo alinisimulia kuwa nchi ya Israel ni nzuri isipokuwa ulinzi wake unakera mno. Alisema kwamba kila baada ya hatua chache unakutana na vituo vya kufanyia upekuzi vilivyosheheni askari wa kila aina. Hali hiyo ilimfanya rafiki yangu huyo auone uzuri wa nchi hiyo kama vile unapunguzwa kwa kiasi kikubwa na kitu hicho, ukaguzi, aliousema kuwa ni kama hauna mpangilio wala sababu, na umezidi kiasi. Lakini Waisrael ni watu walio na amani, kwa kiasi kikubwa, wakiwa wanaishi katikati ya maadui zao. Ulinzi wao mkali unaoonekana hata kuwakera baadhi ya wageni wao ndiyo salama yao inayowafanya waonekane wana amani kwa kiasi fulani. Kwahiyo amani inayoonekana nchini humo siwezi kushangaa hata kidogo nikiwasikia Waisrael wanatamba nayo kama moja ya mazao wanayoyazalisha wenyewe. Sababu wanaitafuta na kuilinda wao wenyewe. Kwa maana hiyo ndiyo sababu naliona tukio la Westgate kama moja ya mafundisho kwetu, kwa maana ya Wakenya wenyewe pamoja na sisi majirani zao, ambao tumezoea kuimba amani bila kuonyesha juhudi za makusudi za kuitengeneza amani hiyo. Mara zote tunategemea amani iliyotengenezwa na Mwenyezi Mungu kana kwamba tayari tuko ahera. Simulizi za shambulio la Westgate zinaonyesha jinsi magaidi walivyofika kwenye kizuizi cha mwisho cha ukaguzi na kumuua mlinzi kwa kumfyatulia risasi nane, baada ya hapo wakaingia ndani ya jumba hilo bila kizuizi kingine. Hiyo inaonyesha namna ambavyo mlinzi huyo aliyeuawa alivyokuwa pale ilimradi, sababu kama kweli angekuwa pale kiulinzi, akijua kuwa lolote baya linaweza kutokea, asingekuwa katika hali hiyo ya kushambuliwa bila majibu huku kukiwa hakuna mwingine wa kumpa msaada. Maana yangu ni kwamba siamini kabisa kama magaidi wanao uwezo unaouzidi uwezo wa serikali. Siamini kama magaidi wanavyo vifaa vya kufanyia ugaidi wao vilivyo vingi kuzidi vifaa ilivyo navyo serikali kwa ajili ya kuyaokoa na kuyalinda maisha ya wananchi wake. Ni wazi kwamba serikali ya Kenya mbali na polisi inalo jeshi, inavyo vifaa vya kijeshi vingi mno. Tumeweza kuvishuhudia baada ya tukio la kigaidi kufanyika. Vifaa hivyo pamoja na askari kwa nini havikuonekana katika kulizuia tukio vikaja kuonekana baada ya tukio? Swali la kujiuliza ni kwamba vifaa hivyo vya kijeshi na kiulinzi vinanunuliwa kama mapambo tu au kwa ajili ya maonyesho ya mbwembwe na kisha kuwekwa ndani kuhifadhiwa? Kama ni kwa ajili ya ulinzi wa wananchi inawezekanaje visionekane kwa ajili ya kinga, katika kuyakinga na kuyaokoa maisha, ila tu baada ya tukio baya kama hilo la Westgate ndipo vionekane wakati maisha ya wananchi yakiwa yameishapotea? Niliwahi kuandika nikiuliza, kwa mfano, kwamba hapa Tanzania kuna tatizo la ajira, watu wanaotafuta ajira wako chungu nzima, lakini papohapo kuna watu wasio na idadi toka nje ya nchi wanaovamia ajira ambazo zingechukuliwa na Watanzania wenyewe! Nikauliza, katika hali kama hiyo vyombo vinavyohusika na usalama wa taifa vinaliangaliaje jambo hilo? Kila mwaka vyuo vyetu vya ualimu vinatoa maelfu ya walimu, mpaka sasa kuna baadhi ya walimu ambao hawana ajira za uhakika kutokana na kutopata nafasi za kufundisha, lakini wakati huohuo tunao walimu wasio na idadi toka nje ya nchi wanaofundisha hapa nchini. Kibaya zaidi wengine hawaeleweki kama ni walimu kweli, ila tu wawe wanaweza kuongea lugha ya Kingereza! Hali hiyo inanifanya nihisi kwamba tumebweteka kwa kiasi fulani, nashindwa kuamini kama njia zilizopo za ulinzi, ambazo watu kutoka nje wanaweza wakazipenya kiurahisi na kuingilia ajira za hapa nchini, wakati wenyeji wanalia na ajira, zinaweza zikawazuia watu wanaokuja kwa lengo baya. Kitu kilichopaswa kuangaliwa ni kwamba ajira ni mojawapo ya bomu ambalo linaweza kulipuka kwa kishindo kuliko hata ule mlipuko uliotokea Westgate na kuteketeza sehemu ya jengo hilo ukiwa umeligeuza kifusi. Hivyo watu wanaotoka nje ya nchi na kuvamia ajira za hapa nchini, wakati wenyeji wanalia na ajira hizo bila kuzipata, hawapaswi kutofautishwa sana na watu wanaotoka nje ya nchi wakiwa wamejifunga milipuko, kama wale walioiteka Westgate. Fundisho tulilolipata toka kwenye uvamizi wa Westgate linapaswa kuwa la umakini. Tunapaswa kuwa makini katika mambo mbalimbali yanayoweza kupenyeza uadui katika usalama wetu. Umakini wetu unapaswa uwe wa kwamba sio lazima uadui uje kwa njia moja ileile kama iliyotokea kwa jirani. Kule Kenya imevamiwa sehemu ya biashara ambako watu wengi, hasa kwenye siku ya mwisho wa juma, wanakwenda kufanya manunuzi na mambo mbalimbali yakiwemo “matanuzi”. Tukio hilo limesababisha maduka mengi hapa Jijini Dar es salaam yaliyo katika mwonekano kama wa Westgate kuwekewa ulinzi wa ziada. Lakini katika mikusanyiko mingine inayoweza kutumiwa kiuhalifu bado imesahaulika. Sehemu za burdani, ambako nako kuna mikusanyiko mingi ya watu, bado haijaonekana kuwa na ulinzi ulioimarika. Maana yangu hapa ni kwamba watu wanaoingia katika sehemu hizo za burdan bado hawafanyiwi ukaguzi wa kutosha kuhakikisha kwamba wahalifu hawajipenyezi kirahisi kwenye sehemu hizo. Watu wanaoingia kwenye viwanja vya mpira, kwa mfano, hawakaguliwi kwa kiasi cha kutosha. Kwa maana hiyo pia hiyo inaweza ikawa njia mojawapo ambayo wahalifu wanaweza kuitumia kufanya unyama wao bila watu wala vyombo vya usalama kuhisi kama kitu cha aina hiyo kingeweza kutokea. Kutokana na funzo la Kenya naona ni wakati muafaka kuhakikisha kila uchochoro unaoweza kutumiwa na uhalifu unafungwa kwa nguvu zote. Ninaamini uweza huo upo. Kinachotakiwa ni kuchangamsha akili tukiwa tumeacha kubweteka kwa kuegemea kwenye neno amani ambayo tunatengenezewa na Mwenyezi Mungu Tunapaswa tuitegemee zaidi amani tuliyoitengeneza na kuilinda sisi wenyewe. Katika kufanya hivyo inabidi wageni tuwaachie uhuru wa kipimo, tuwapende wageni wetu na kuwaacha wakafanya mambo yao lakini tukiwa tumewawekea mipaka ya uhuru huo. Nadhani hiyo wataielewa kwa vile ni sehemu ya usalama wetu na wa kwao pia. Baya lolote linapotokea halibagui mwenyeji na mgeni. Ni jukumu la mwenyeji kutunza usalama wa sehemu yake, wageni wetu itabidi watuelewe katika kuhakikisha usalama wetu unalindwa sambamba na kuwahakikishia usama wao vilevile. Katika hili hatupaswi kuendelea kutegemea amani tuliyopewa na Mwenyezi Mungu, tunapaswa tuwe kama Waisraeli, tuhakikishe amani tunaitafuta na kuilinda sisi wenyewe. Mambo ya kuendelea kuimba amani na utulivu ambako hatujawekeza lolote yamepitwa na wakati. Huu sasa ni wakati wa kuitafuta amani kwa udi na uvumba na kuhakikisha tunailinda kwa njia zote tulizo nazo, hiyo ni kwa sababu dunia ya sasa imebadilika, baadhi ya watu wanauona unyama ndiyo njia iliyobaki kuyaendesha maisha! Nawapongeza wote waliohusika kuyagundua na kuyasambaratisha mazoezi ya kigaidi yaliyokuwa yakiendeshwa katika msitu kuko Mtwara. prudencekarugendo@yahoo.com 0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau