Bukobawadau

Kinachonifanya nimpende Lowassa ni hiki

na Denis B. Mwanukuzi

WAKATI tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, tayari yanasemwa mambo mengi kuhusu ni nani atakayekuwa mrithi wa nafasi ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Wananchi wanasema yao, na ni halali yao kikatiba na kiutaratibu, kwa sababu wanayemsema ni kiongozi wao mkuu wanayemchagua wao. Sidhani kama ni kosa la jinai kusema kwamba fulani ndiye anayepaswa kuwa au atakayekuwa rais wao.

Kwahiyo hata mimi nimetumia njia hiyo kuonyesha kilicho moyoni mwangu. Nataka nitaje ni mtu gani ambaye naona anafaa kupewa nafasi ya kuongoza nchi yetu baada ya muda wa rais aliyepo kwasasa kuisha. Nalisema hili kwa nia njema nikisukumwa na mapenzi niliyo nayo kwa nchi yangu.

Mtu mwenye mapenzi mema na nchi yake ni lazima atizame ni namna gani nchi yake itaongozwa vyema, kwa ufanisi, ikiwa inapiga hatua kwenda mbele huku kila jambo la ustawi wa nchi likiwa limezingatiwa, usalama wa nchi na wananchi, maendeleo, na mahitaji mengine ya kiutu nakadhalika.

Hayo yote yanahitaji mtu aliye makini katika kuhakikisha yanapatikana bila aina yoyote ya visingizio. Sababu kama tunavyoona, matatizo mengine katika nchi yetu yanatokana na uzembe katika uongozi na usimamizi. Na hilo linatokana na ukosefu wa umakini.

Kwahiyo kwa upande wangu mimi mtu ninayemuona kuwa anatufaa kuwa kiongozi wetu mkuu, rais, ni Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa. Ni mtu makini, mbunifu na mwenye kujisimamia kimaamuzi.

Nilianza kuuona uwezo wa Lowassa zamani kidogo, tangu alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, AICC. Namna alivyokiongoza kituo hicho bila matatizo yoyote ya kukifanya kishindwe kujiendesha, ndilo jambo lililonifanya nianze kumuona kuwa anafaa. Nilitamani sana mtu huyo aingie kwenye siasa za nchi yetu ili aweze kutumia uwezo wake aliokuwa akiuonyesha pale AICC kuusaidia uongozi wa nchi yetu.

Mungu si Athumani, taratibu Lowassa akaingia kwenye siasa za nchi yetu. Akaingia Bungeni kwanza, na baadaye akaupata uwaziri. Aliyoyafanya akiwa waziri ndiyo yaliyozidi kunidhihirishia uwezo wake.

Kinachonisukuma nimuone Lowassa ana uwezo tofauti na watu wengine ni moyo wake wa uchapakazi. Pamoja na hiyo yeye ana uwezo wa kuthubutu, ni mtu asiyebabaika katika kufanya maamuzi. Hiyo ni tabia ambayo kiongozi yeyote anatakiwa kuwa nayo.

Viongozi wengi wana tatizo la kushindwa kuchukua maamuzi. Tatizo hilo halijionyeshi kwa Lowassa. Tunaweza kujikumbusha maamuzi aliyoyachukua Lowassa kipindi akiwa waziri wa kawaida.

Wakati fulani akiwa Waziri wa Ardhi aliwahi kuchukua uamuzi ambao mara nyingi wengi unawashinda na hivyo kuyafanya mambo yaende kombo. Mfano kuna mtu alikuwa ametumia njia za kughushi na kujifanya eti anawekeza kwenye viwanja vya wazi vya Mnazimmoja, akavizungushia uzio wa mabati eti kwa lengo la kujenga mabanda kuzunguka viwanja hivyo.

Baada ya watu kulalamika, Lowassa alisema mara moja kwamba alichokifanya mhusika ni ukiukaji wa sheria za Mipango Miji, kwahiyo akataka mabati hayo yaondolewe mara moja. Wananchi waliokuwa wanafuatilia kauli ya serikali, baada ya kusikia kauli hiyo, walimsaidia mwekezaji feki huyo kwa kuuondoa uzio wa mabati katika viwanja vya Mnazimmoja kwa muda mfupi sana, walichojilipa kwa kazi hiyo ni kujibinafsishia mabati yenyewe.

Kwahiyo naweza kusema kwamba maamuzi ya Lowassa ndiyo yaliyovinusuru viwanja hivyo. Si ajabu bila yeye eneo hilo kwa sasa lingekuwa vingine kabisa, pengine viwanja vya wazi vya Mnazimmoja visingekuwepo na badala yake kungekuwepo na maduka, mahoteli nakadhalika.

Vilevile Lowassa aliweza kuunusuru ufukwe wa bahari uliotazamana na hoteli ya Kilimanjaro, kuna mtu aliyekuwa amejitokeza eti naye ni mwekezaji akitaka kulichukua eneo hilo!

Kitu kingine alichokifanya Lowassa akiwa waziri wa kawaida ni kuifuta kazi kampuni iliyokuwa imepewa zabuni ya kuendesha masuala ya maji Jijini Da es salaam, kampuni ya City Water, wakati huo akiwa Waziri wa Maji.

Kwahiyo tunaona kwamba mambo mengi yanazorota na kufikia kuwa matatizo katika utendaji wa serikali yetu kutokana na ukosefu wa maamuzi kutoka kwa wanaokuwa wamepewa majukumu ya kuyasimamia.

Baada ya hapo Lowassa alikuwa Waziri Mkuu baada ya Kikwete kuingia Ikulu. Kwa kipindi kifupi aliweza kufanya mambo kama mtu aliyekalia cheo hicho kwa muda mrefu. Sababu ya kuonekana hivyo ilikuwa ni uwezo wake wa kuchukua maamuzi bila kusita.

Tuliona jinsi alivyolishughulikia suala la ukosefu wa umeme nchini kiasi cha kuingia mkataba na kampuni “feki” ya Richmond. Lakini si yeye aliyefanya hivyo bali watu wasiokuwa waaminifu waliokuwa chini yake. Lengo la Lowassa lilikuwa zuru, kuiona nchi inaendeshwa bila matatizo ya umeme.

Ikumbukwe kwamba sio maamuzi yote yenye malengo mazuri yanayokuwa na matokeo mazuri. Kuna matokeo mengine yanayoweza kuwa kama ajali, kilicholengwa ni kizuri ila matokeo yanakuwa mabaya. Ni sawa na mtu anayepanga safari bila kuelewa kuwa gari litapata ajali. Ajali ikishatokea huwezi kumlaumu aliyepanga safari.

Kutokana na upungufu wa mashule na ongezeko la watoto wanaoingia sekondari, Lowassa akabuni ujengaji wa shule za kata. Lengo lake lilikuwa kila kata iwe na shule yake ya sekondari. Huo ni ubunifu mzuri ambao wengi waliomtangulia hawakuwahi kuufikiria.

Kwahiyo kukosekana kwa vifaa vya kufundishia pamoja na upungufu wa walimu kamwe hakufanani wala kulingana na kutokuwepo kabisa kwa shule za sekonfari, yaani kuwaacha watoto wakilandalanda mitaani baada ya darasa la saba bila mahali pa kuwapeleka.

Nina imani Lowassa angeendelea kuikalia nafasi yake ya uwaziri mkuu ni lazima angebuni pia namna ya kuwapata walimu pamoja na vifaa vya kufundishia, kwa vile ubunifu unaonekana kuwa kipaji chake.

Mfano wakati fulani alikuwa amebuni njia ya kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Jiji. Alisema barabara zenye njia nne ziwe na njia tatu kila siku kutegemea na muda ambao magari yanakuwa mengi.

Huo wote ni ubunifu anaopaswa kuwa nao kiongozi wa wananchi. Ubunifu unaoongozwa na maamuzi yaliyo katika mamlaka anayopewa kiongozi na wananchi. Sababu kushindwa kubuni pamoja na maamuzi hafifu ndio mwanzo wa matatizo yanayotupata kwa sasa. Jambo dogo linageuka kuwa kubwa na wananchi kuishia kwenye matatizo yasiyo ya lazima.

Kwahiyo, kwa mtazamo wangu, tukimpata mtu kama Edward Lowassa akawa mtu wa maamuzi ya mwisho yasiyotaka kuhojiwa na yeyote kabla ya kutekelezwa, tutakuwa tumepata kura ya turufu. Mtu huyu, kwa uwezo wake huo, ni lazima atatuvusha salama kwenye haya matatizo tuliyomo kwa sasa ambayo si kila yote yatafutiwe suluhisho nje ya nchi.

Kwa maana hiyo ni sababu hizo zinazonifanya nimuone Lowassa kama mtu anayefaa kuwa kinara wetu ifikapo 2015. Kwahiyo wananchi wanaoifikiria nchi yao kwa mapenzi mema wanapaswa kulitilia maanani jambo hilo. Si kwa kumpenda mtu kwa sura yake tu bali kwa uwezo wake.

Tukiondoa mambo ya mizengwe, ambayo nahisi hayamsaidii lolote mwananchi wa kawaida, Lowassa ndiye anayefaa kuwa rais wetu ajaye. Sisemi haya kwa vile tunafahamiana na Lowassa, la hasha, hanifahamu hata kidogo, ila nayasema kwa mapenzi mema niliyo nayo kwa nchi yangu.

Hivyo ninapomsema Lowassa, pamoja kuona kuwa ndiye mtu anayefaa kuwa rais wetu mtarajiwa, siyasemi haya kutokana na uwezo huo alio nao, bali nayasema kwa mapenzi niliyo kwa nchi yangu. Nchi yangu naitakia mema na mazuri, ndiyo maana namtaja mtu ninayeamini anafaa kuiongoza.

Watanzania tujiangalie, tusifanye makosa kama ambayo tumekuwa tukiyafanya muda wote. Tukumbuke kwamba kosa ni kurudia kosa na wala si kufanya kosa.

0717 599 579
Next Post Previous Post
Bukobawadau