Bukobawadau

MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA FEDHA YA SERIKALI AWASILI MKOANI KAGERA NA KUANZA UKAGUZI MAALUM MANISPAA YA BUKOBA • Awaonya Wahusika Kutojaribu Kutembeza Vibahasha kwa Wakaguzi

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha ya Serikali Bw.Ludovick Utouh amewasili mkoani Kagera kwa ajili ya kufanya Ukaguzi maalum katika Manispaa ya Bukoba ili kutafuta ufumbuzi wa kutatua mgogoro uliodumu takribani miaka miwili na kukwamisha maendeleo ya wananchi wa Manispaa hiyo.
Bw. Ludovick mara baada ya kuwasili katika mkoa wa Kagera Septemba 30, 2013 alifanya kikao cha ufunguzi wa Ukaguzi Maalum katika Manispaa ya Bukoba na kufafanua madhumuni ya Ukaguzi huo ikiwa ni pamoja na ni namna gani ukaguzi huo utafanyika.
Bw. Ludovick alisema chimbuko la Ukaguzi Maalum lilitokana na hoja zilizojitokeza baada ya kutokea kutoelewana baina ya Waheshimiwa Madiwan wa Manispaa ya Bukoba ambapo ilisababisha mgawanyiko mkubwa wa makundi na kuchangia kuzorotesha utendaji kazi wa Manispaa hiyo.
Hoja hizo kuu zikiwa ni pamoja na kukosekana kwa uwazi kuhusu miradi ya uwekezaji ilivyopatikana, Mstahiki Meya kufanya maamuzi yake binafsi bila kushirikisha maamuzi ya Waheshimiwa Madiwani kupitia Baraza la Madiwani.
Akifafanua kifungu cha sheria kinachompa mamlaka ya kufanya ukaguzi maalum Bw. Utouh alisema, “Kwa mujibu wa kifungu cha 36 cha sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anayo mamlaka ya kufanya ukaguzi pale atakapoona kuwa inafaa katika masuala yanayohusiana na fedha na mali za Umma.”
Aidha Bw. Utouh alieleza kuwa alichelewa kufika katika Manispa ya Bukoba kufanya Ukaguzi Maalum kutokana na kukufanya maandalizi ya kutosha kabla ya ukaguzi huo ikiwemo na kuuandaa Adidu za Rejea wakati wa kufanya ukaguzi huo ili kutenda haki katika pande zote mbili na kuumaliza mgogoro.
Adidu za Rejea 13 za Ukaguzi Maalum Manispaa ya Bukoba
Kuchunguza usahihi wa utaratibu uliotumika kumpata mwekezaji wa kituo cha kuosha magari (ACE Chemical Ltd), Kuchunguza uhalali wa nyaraka na kiasi kilichowekezwa cha sh.297,000,000kwenye mradi wa kuosha magari
Kuchunguza tatizo na sababu zilizopelekea viwanja 800 kutogawiwa kwa wananchi waliochangia gharama za upimaji, Kuchunguza wa upimaji viwanja 5,000
Kuchunguza miradi wa ujenzi wa soko, ujenzi wa kitega uchumi na kituo cha Mabasi, ujenzi wa chuo cha ualimu, ujenzi wa kituo cha maarifa na ujenzi wa Bwawa kwa ajilli ya utalii.
Kuchunguza Kiwanja cha Shule ya Msingi Kiteyagwa, Barabara ya kupitia Kagondo Kaifo hadi Kagondo Karuguru na kuchunguza masuala mengine ya matumizi ya fedha yanayoashiria ubadhirifu.
Onyo, Bw.Utouh pia alitoa onyo kali kwa viongozi wanaolumbana katika Manispaa ya Bukoba kutojaribu kuwarubuni wakaguzi ambao ameambatana nao katika ukaguzi huo. “Wakaguzi hawa ni wenye ujuzi wa kutosha na wa muda mrefu msije mkajaribu kuwapelekea vibahasha mtajisumbua bure na hawatapokea.” Alisema Bw. Utouh.
Vilevile Bw. Utouh aliwaagiza Katibu Tawala Mkoa na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba Kuhakikisha kuwa watendaji wote walikwishahama na watahitajika kutoa maelezo katika ukaguzi huo maalum wapatikane ili kutoa ushirikiano wa dhati.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kanali Mstaafu Fabian Massawe alimshukuru Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha ya Serikali kufika mkoani hapa ili kutoa suruhu ya mgogoro wa muda mrefu uliokwamisha jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi wa Manispaa ya Bukoba.
Taarifa ya ukaguzi maalum katika Manispaa Bukoba itakamilika ndani ya siku 35 kuanzia Septemba 30, 2013 na mara baada ya kukamilika taarifa hiyo itakabidhiwa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwawajibisha wale wote watakaobainika kufuja fedha na mali za serikali na kuuumaliza mgogoro uliodumu miaka miwili.
Imeandikwa na:
Sylvester Raphael
AFISA HABARI
RS-KAGERA@2013
Next Post Previous Post
Bukobawadau