Muundo wa serikali tatu huenda ukawa suluhisho la matatizo ya muungano
Written by Msemaji mkuu // 18/10/2013
Nina matumaini makubwa kwamba mfumo wa serikali tatu katika muungano, huko mbele, unaweza kuwa ni suluhisho kubwa la matatizo ya muungano. Sio moja kwa moja katika mpangilio uliopangwa na jaji Warioba na kamati yake, la hasha.
Ukiangalia rasimu ya katiba mpya kama ilivyotolewa na timu ya Warioba utaona haileti matumaini makubwa kwa Zanzibar kwa sababu mambo makubwa na muhimu katika uhuru wa nchi bado yamo kwenye serikali ya muungano. Lakini nategemea huko mbele mambo yatabadilika na uhuru zaidi utapatikana.
Ikiwa kweli kutakua na serikali ya Tanganyika, ya Zanzibar na ile ya Muungano, na kwamba hautafanyika ujanja ule ule uliofanyika April 1964, ambapo baada tu ya makubaliano ya muungano Nyerere aligeuza kibao na kutangaza kwamba kuanzia 26/04/64 mambo yote ya Tanganyika yatakua chini ya serikali ya muungano, na ikiwa kila serikali itashughulikia mambo yalioko katika mamlaka yake, sulhu itapatikana.
Sababu kubwa ya kuamini hivyo nikwamba serikali ya Tanganyika katu haitokubali kuburuzwa na serikali ya muungano kama inavyofanywa serikali ya Zanzibar kwa miaka hamsini sasa. Serikali ya Tanganyika ambayo kwa hivi sasa ndio serikali ya muungano itakapoona haina mamlaka ya kutekeleza mipango yake itakuja juu na ndio itakayokua mstari wa mbele kudai na kumegua mambo ya muungano yatoke katika muungano.
Siamini kwamba Watanganyika wakitaka kuanzisha mradi wa maendeleo katika nchi yao, na kama wakati huo kiongozi wa serikali ya muungano ni Mzanzibari na baraza la mawaziri lina Wazanzibari, watakuja Zanzibar kuja kupiga magoti kwa mkurugenzi fulani ili mradi wao ukubaliwe. Hilo hawatakubali. Na kama kiongozi wa muungano atakua Mtanganyika hakuna kitakachokwamishwa kwa sababu ndio wao kwa wao.
Serikali ya Zanzibar kwa miaka hamsini haijapata kufanikiwa hata mara moja kutoa jambo la muungano na kulifanya lisiwe la muungano. Ingawa wamejaribu mara nyingi kwa lengo la kutaka kuinasua Zanzibar kutoka katika magando ya kaa(muungano) lakini juhudi zao zilipigwa na chini. Kilichofanyika ni kuyafanya mambo yasiokua ya muungano kuyafanya ya muungano. Tulianza na mambo 11 na sasa yamekua 38.
Katika wakati wa Karume(senior) Baraza la Mapinduzi liliandaa orodha ya mambo ambayo walitaka yatolewe katika mambo ya muungano; lakini yalipopelekwa Bungeni Nyerere aliyazima. Lakini kutokana na kuchachamaa kwa Karume baadhi ya mambo hayakuweza kuingizwa katika muungano mpaka alipouwawa ndio yakapata njia.
Katika wakati wa Aboud Jumbe na yeye alijaribu kwa upande wake kujaribu kupambanua mambo yepi yawe ya muungano na yepi yasiwe. Nayeye yaliompata yanajuilikana. Tumeona yaliomfika Maalim Seif na kundi lake kwa kujaribu kuufafanua muungano na kutafuta maslahi ya Zanzibar katika muungano.
Katika kipindi kilichofata kuanzia 1995 hadi hivi sasa hakuna juhudi yoyote kubwa ya viongozi wa Zanzibar kujaribu kutoa jambo lolote kutoka kwenye muungano. Sababu kubwa ni kwamba viongozi wa Zanzibar katika kipindi hicho ni mamluki wa serikali ya Muungano/Tanganyika.
Naamini kabisa kwamba kama kutakua na serikali ya Tanganyika katika muungano mpya, haitokubali kukabwa koo na serikali ya muungano. Na kwa sababu mabadiliko yote yatakua yanafanyika katika bunge la muungano ambalo litakua na Watanganyika 50 na Wanzibari 20, lolote watakalopeleka bungeni litapita. Wataanza kuumegua muungano kidogo kidogo mpaka mwisho kila nchi itaweza kua na mamlaka yake kamili.