Muungano wenye dosari hauwezi kuwa imara
Na Prudence Karugendo
SIKU za nyuma kigo mwandi mmoja machachari hapa nchini aliandika anajiuliza swali kwamba Wazanzibari wanatarajia nini nje ya Muungano? Katika maelezo yake yaliyobebwa na swali hilo mwandishi huyo anaonyesha kuwa na wasiwasi juu ya mustakabali wa Wazanzibari wanaojaribu kuutekenya Muungano ili kuona kama unaweza kuitapika nchi yao wanayoamini ilimezwa na Tanganyika na baadaye Tanganyika kujigeuza Tanzania. Jambo ambalo ningependa kumkumbusha mwandishi huyo ni kwamba fikra kama alizo nazo yeye ndizo zinazo wachochea Wazanzibari waifikirie zaidi nchi yao badala ya kuufikiria Muungano. Fikra zile za kwamba maadamu Zanzibar ilikuwa nchi ya visiwa vidogo na idadi ndogo ya watu ikilinganishwa na Tanganyika, basi ilikuwa ni haki na halali nchi hiyo kumezwa na Tanganyika. Hii ni kwa sababu mwandishi haonyeshi kama visiwa vile vilikuwa ni nchi inayojitegemea kabla ya Muungano na vilivyokuwepo mamilioni ya miaka kabla ya hapo. Yeye mawazo yake yanaanzia mwaka 1964, mwaka wa kuundwa kwa Muungano wa Tanzania. Hilo hasa ndilo jambo linalowasukuma baadhi ya Wazanzibari, wanaojihisi wamo ndani ya tumbo la Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania, waanzishe madai ya kutaka kutapikwa ili nao waende sambamba na Watanganyika wakiwa nao kama watu waliokuwa na nchi yao, kuliko ilivyo sasa ambapo wanaona kama wanalazimishwa kuwa kama sehemu ya Watanganyika waliokuwa wamepotea. Yapo madai yanayotolewa na baadhi ya watu, akiwemo mwandishi huyo, ya kwamba Wazanzibari walio wengi asili yao ni Tanganyika, wakitaka hiyo hoja iwe ndiyo nguzo kuu ya Muungano! Muungano wa Tanganyika na Zanzibar si wa kwanza hapa duniani, zipo nchi nyingi zilizoungana na nyingine baadaye zikaja kutengana kutegemea sababu zilizoshawishi kuungana huko. Lakini katika kuungana huko hakuna nchi iliyokuwa tayari kutelekeza maslahi yake kwa ajili ya kuungana na nchi nyingine. Na pale ambapo nchi moja itakuwa ilijisahau na kutelekeza maslahi yake ni lazima baadaye wajitokeze wananchi wa kurekebisha kasoro hiyo ili kuimarisha muungano au hata kuuvunja kama hapana budi ilimradi kasoro zisiendelee kutumika kama mhimili wa muungano wa watu wenye akili timamu. Tumeona muungano wa nchi za Kisoviet ulivyovunjika na nchi zilizokuwa zinaunda muungano huo kujiendesha kila moja kivyake salama salimini. Muungano wa Yugostlavia vivyohivyo, pia na muungano wa Czechoslovakia ambapo sasa ni nchi mbili, Czech na Slovakia. Swali la msingi la mwandishi nimtajaye ni nini matarajio ya Wazanzibari nje ya Muungano? Nataka nimkumbushe mwandishi kuwa daima matarajio ya mwanadamu ni ubora. Watanganyika tulipokubali kuunganishwa na Wingereza, muungano uliofanywa na League of Nations wakati ule, baada ya Vita kuu ya Kwanza ya Dunia, tulitarajia tungepata maisha bora kuliko yale tuliyokuwa nayo chini ya Mjerumani. Lakini baada ya kuona mambo hayabadiliki hata baada ya miaka arobain, tukaona bora tujitawale wenyewe na huo kuwa mwanzo wa kutafuta kuuvunja muungano kati ya Tanganyika na Wingereza. Waingereza pia waliuliza swali kama la mwandishi wakati ule, kwamba Watanganyika wanatarajia nini nje ya muungano? Hivi ni kweli hatukuweza kujimudu nje ya muungano ule? Mwandishi anasema kwamba kuna Wazanzibari walio na matajio binafsi nje ya Muungano wa Tanzania. Hiyo siwezi kuipinga moja kwa moja, maana sisi ni wanadamu. Sababu hata Mwenyezi Mungu alipomuumba mwanadamu ilitokea mwanadamu huyo akawa na matarajio binafsi nje ya matakwa ya Mwenyezi Mungu, ndio ukawa mwanzo wa ibilisi. Tukiacha hilo, tunaweza kuamini kwamba iwapo halikuwa kosa kwa watu kuwa na matarajio binafsi ndani ya Muungano basi haliwezi kuwa kosa kama kunatokea baadhi ya watu wakawa na matarajio ya aina ileile nje ya Muungano Yawezekana kuna walioutaka Muungano ili uweze kuwalindia mamlaka zao, haya yalikuwa matarajio bonafsi. Kutaka kuyahami mamlaka dhidi ya wale unaowatawala ni matarajio binafsi na wala siyo matarajio yenye kuunufaisha umma. Kuna waliotaka kufanya biashara kwenye eneo kubwa la Tanganyika bila kizuizi cha kuwaonesha kuwa ni wageni, na hayo ni matarajio binafsi. Vilevile kuna walitarajia nafasi za kazi na vyeo kwenye Muungano nakadhalika. Yote hayo ni mambo yaliyokuwa katika matarajio binafsi ambayo kwa namna yoyote ile hayaunufaishi umma wa Wazanzibari ambao ndani ya zaidi ya miaka arobaini ya Muungano bado unaiona hali ya maisha kuwa ileile au inayozidi kuwa mbaya zaidi. Kampeni zisizo rasmi za kuushawishi umma kuuchukia Muungano anazoziona, mwandishi tajwa upande wa Zanzibar, kama kweli zipo, ni lazima aelewe kuwa hapo kuna tatizo. Katika hali ya kawaida haiwezekani uzuri wa Muungano ukawa unajionesha wazi halafu pakatokea wa kuwaonesha watu vinginevyo. Kwahiyo cha kuangalia ni hilo tatizo linalotumiwa kuwashawishi watu kuuchukia Muungano, na wala kumtafuta mshawishi hakuwezi kusaidia maana itakuwa ni kulifunika tatizo badala ya kuliondoa. Kitu kingine kinachomfanya mwandishi huyo authamini zaidi Muungano kiasi cha kuona giza mbele yake na kutoelewa nini utakuwa mustakabali wake nje ya Muungano, ni ile dhana ya kwamba maadamu vile ni visiwa na viko karibu na Tanganyika kwa vyovyote vile wenyeji wake watakuwa walitokea Tanganyika. Hii ni dhana inayoyatawala mawazo ya walio wengi wa upande wa Tanganyika. Na wengi wanaichukulia dhana hiyo kama kihalalisho cha Muungano huu. Mara kadhaa nimesikia maneno ya kwamba Muungano wa Tanzania ni wa lazima kwa vile Wazanzibari wengi wana asili ya Tanganyika. Hii ni dhana potofu, na nahisi ndiyo inayo chochea maswali ndani ya Muungano huu. Kwa nini tuitizame Zanzibar tu katika kuangalia uasili wa wakazi? Kwa nini hatujiulizi ilikuwaje tusiungane na Msumbiji ambako zaidi ya makabila manne ya Tanzania yanapatikana vilevile nchini mle? Wapo Wamakonde, Wayaho, Wangoni, Wanyasa nakadhalika. Vilevile tunaweza kujiuliza kwa nini hatukuungana na Uganda ambako unakuta kuna makabila matano yaliyo sawa na makabila kama matatu ya Tanganyika. Kuna Wanyankole, Watoro, Wakiga kwa upande wa Uganda, ambao ni sawa na Wanyambo, Wasubi na Wahaya kwa upande wa Tanzania. Kuna Waganda, ambalo ndilo kabila kuu la nchi ile, lililoenea hadi Kasikazini mwa Tanzania ambako wanajulikana kama Waganda Kyaka. Pia Kenya nako kuna Wajaluo, Wakurya na Wamaasai wanaopatikana vilevile Tanzania. Mbali na hiyo kwa nini hatujiulizi Watanganyika tulitokea wapi? Kama Muungano ungekuwa unalazimika kuhusishwa na uasili wa wananchi wa nchi husika, tunaonaje kama Afrika Kusini ingekuja kulazimisha Muungano na Tanzania sababu ya Wangoni ambao wana asili ya nchi ile? Kwahiyo mwandishi yampasa aelewe kwamba kuendelea kuzikwepa hoja muhimu katika Muungano wetu huu na kuzipa kipaumbele hoja nyepesi nyepesi kama ile ya kwamba Wazanzibari wakitoka katika Muungano hawawezi kuwa wamoja, tutakuwa tunaudhoofisha Muungano wetu kadiri unavyozidi kula chumvi na kuzeeka. Tishio la kwamba Wazanzibari hawawezi kuwa wamoja nje ya Muungano ni sawa na kumtishia mtu mzima nyau. Sababu kama Wazanzibari walikuwepo tena wakiwa wamoja mamia ya miaka kabla ya Muungano, kinachoweza kuwavuruga baada ya Muungano ni kitu gani? Nakumbuka maneno ya Baba wa Taifa aliyoyasema pale Kilimanjaro Hotel mwaka 1995, kwamba Wazanzibari wakiamua kujitenga kwa jeuri ya ubaguzi, hawawezi kuwa wamoja. Pale Mwalimu alikuwa anaongelea ubaguzi wa kikabila. Mwalimu aliongeza kwamba iwapo Watanganyika wakiamua kuwanyanyapaa Wazanzibari na Wazanzibari wakaondoka zao, Wazanzibari watabaki salama ila Watanganyika hawatabaki salama. Sasa kitendo cha mwandishi kuonesha kwamba madhali Wazanzibari ni wachache na ni kama wamemezwa ndani ya Watanganyika walio wengi, na hivyo hawapaswi kuwa na kauli juu ya kile wanachokiona ni halali yao, haoni kwamba ni sawa na kuwanyanyapaa? Haoni kwamba Wazanzibari wanaweza wakaondoka wakaenda kuwa wamoja na kuwaacha Watanganyika wanatafunana kwa dhambi ileile ya mkubwa kumtafuna mdogo, kabila kubwa kutaka kulimeza kabila dogo kwa kwenda mbele? Wazanzibari kuhoji masuala ya muhimu kuhusu Muungano wetu sioni kama ndiyo sababu ya kutufanya tuwaone wanataka kujitenga au kuuvunja Muungano. Mathalan, wanasema kwamba kabla ya Muunagano wa nchi mbili hizi, Tanganyika na Zanzibar zilikuwa tayari ni wanachama wa Umoja wa Mataifa. Wanauliza, baada ya kuungana ni lini Tanzania iliomba uanachama wa Umoja wa Mataifa kama sio kuendelea kukalia kiti kilekile cha Tanganyika wakati kile cha Zanzibar kikifutwa? Sasa wanaposema wamemezwa tutasemaje kuwa wanataka kujitenga? Moyo wa uzalendo nao unaweza kugeuka dhambi ya ubaguzi? Tujiulize, Wazanzibari wanawezaje kujenga moyo wa uzalendo kwa Tanzania iwapo hawana mahali pa kuanzia kujenga uzalendo huo? Si ni lazima waanze kuipenda Zanzibar ili wapate pa kusimama kuipenda Tanzania? Wasiwasi wa mwandishi kuhusu hatima ya Muungano wa Tanzania inatia mashaka kwa wenye kufuatilia kwa karibu suala la Muungano huu, hasa wale wadau wa upande mmoja wa Muungano, Wazanzibari, endapo mawazo yake yanawakilisha ya wengine wenye mtizamo kama wa kwake. Ikiwa mwandishi anaushuku upande wa pili wa Muungano kwa kuzua kasoro ambazo anadai zikitaka zishughulikiwe zote matokeo yake itakuwa ni kuuvunja Muungano, huo Muungano anataka umnufaishe nani kama upande wa pili unaziona kasoro anazolazimisha zifumbiwe macho eti kuunusuru Muungano? Ukishamshuku mshirika wako halafu ukaendelea kushirikiana naye ujue ushirika huo unakunufaisha wewe zaidi ya mshirika mwenzako unayemshuku. Wazanzibari hawatarajii chochote nje ya Muungano zaidi ya Muungano ulio imara bila dosari, ndilo jibu ninaloweza kulitoa kwa mwandishi huyo.. prudencekarugendo@yahoo.com 0784 989 512