Bukobawadau

Tibaijuka akemea migogoro ya ardhi


Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa  Anna Tibaijuka amesema migogoro mingi ya ardhi inayojitokeza sababu kubwa ni watu kushindwa kutii sheria za chini.
Tibaijuka alisema watu hujenga au kuendeleza maeneo ambayo, ama yameachwa wazi na serikali au yanamilikiwa na watu wengine wakiwa na ufahamu wa jambo hilo.
Waziri Tibaijuka alisema hayo jana, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani, ambayo pamoja na mambo mengine hutumiwa kutafakari hali halisi ya makazi katika nchi husika.
“Hivi mtu aliyejenga sehemu ya wazi, bondeni  au kwenye hifadhi ya barabara, unadhani hajui kama anavunja sheria?”, alihoji Tibaijuka.
Alisema ni kweli kuna sehemu ambazo serikali ilichelewa kupima na kutenga maeneo ya huduma muhimu pamoja na miundombinu kutokana na ukuaji wa kasi wa miji,  lakini hiyo siyo sababu ya watu kuvamia.
Aidha, Waziri alizitaka  Halmashauri  za miji kote  nchini kuhakikisha inapanga miji na kutenga maeneo ambayo yatatumika katika kujenga sehemu za kutolea huduma muhimu, ili kupunguza bomoa bomoa isiyokuwa na lazima.
“Sehemu za mijini hususan katikati ya  jiji la Dar es Salaam kumekuwa na msongamano mkubwa wa watu kwa sababu ya kupatikana kwa huduma zote muhimu pamoja na ofisi nyingi za serikali na binafsi katika eneo moja. Tunatakiwa tujifunze sasa wakati tunabuni miji mingine,” alisema Waziri.
Alisema kazi ya kupanga miji si ya kisekta ni kazi ya wadau wote, kwani ukipanga mji vizuri maisha ya mjini yanakuwa mazuri na changamoto zinazopatikana sasa kama foleni zitapungua.
Next Post Previous Post
Bukobawadau