Bukobawadau

TUNAIWAZA KESHO YA WANETU?.

Moja ya maswali magumu ambayo yamepita mara kadhaa kwenye akili yangu ni juu ya kwanini Tanzania na Watanzania tumeendelea kubaki nyuma huku hali hiyo ikionekana kutotusumbua sote kama jamii?. Hali hii huenda inawasumbua wachache wetu lakini nao haiwasumbui kwa maana pana ya Tanzania na Watanzania kwa ujumla wetu bali kila mmoja kwa mtizamo binafsi wa kutaka kila mmoja binafsi kuwa bora kuliko mwenzake lakini si wananchi ama watawala wa Tanzania na Afrika wa leo ambao wanasumbuliwa na suala la Tanzania na hata Afrika kuendelea kubakia taifa na bara la mwisho na sehemu ya majaribio na hata mwanya wa mafanikio kwa watu wa mabara mengine.
Bara zima la Afrika leo linakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii kuliko lilivyokabiliwa nayo kwa miaka mingi huko nyuma na moja ya sababu ni kwamba Waafrika walio wengi Watanzania wakiwa sehemu yao, wanafunguka fahamu na kuona hitajio la maisha bora kuliko wanayoishi hasa kwa kuzingatiwa kwamba bara hili ndilo bara peke yake ambalo bado lina hazina ya rasilimali za aina zote zinazohitajika kwa ajiri ya kuboresha maisha ya watu wake, lakini ndilo maskini kuliko mabara yote hapa ulimwenguni. Kutoka katika historia, Afrika ina rasilimali watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa juhudi na nguvu kuliko mabara yote na huenda hiyo ndiyo ilikuwa moja ya sababu kwamba watumwa wengi waliouzwa kwenye mabara mengine enzi hizo kutokea Afrika kuliko maendeo mengine. Lakini Afrika ni bara peke yake ambalo kwa sababu kadhaa ikiwamo ukweli kwamba kuchelewa kwetu kufikiwa na ‘mfumo rasmi’ wa elimu, elimu yetu iliyozingatia mila na desturi zetu na ambazo nyingi zilikuwa rafiki kwa mazingira, mazingira yetu bado ni bikra kwenye maeneo mengi na huu ni ukweli unaokubalika na wanasayansi wengi duniani.
Maendeleo ya kiviwanda kwenye maeneo mengi duniani siyo tu yamemaliza rasilimali za asili kwenye ardhi ya maeneo hayo, bali pia yameharibu mazingira kiasi cha dunia kufikia kwenye hatari ya majanga makubwamakubwa ya kimanzigira kama tunavyoshuhudia kote ulimwenguni. Kwa hiyo Afrika ina watu na mazingira sahihi kwa ajiri ya maendeleo ya watu wake, sasa kwanini Afrika bado ni maskini na ambayo iko chini ya kongwa la ukoloni mamboleo?. Sikusudii kusema nimepata majibu yote kwa swali hili, lakini nadhani ninawajibika kukushirikisha yale ambayo binafsi nayaona kama changamoto ambazo zinatukinza leo katika juhudi za kujitafutia maisha bora.
Moja ni ukweli kwamba mtizamo wa Waafrika tulio wengi ni duni. Waafrika walio wengi tunajiona duni mbele ya wengine hata katika mambo mengine ambayo kimsingi sisi ni bora kuliko wao. Wengi wa Waafrika sisi, tunadhani watu kutoka mabara mengine wana kitu fulani cha ziada katika utu wao ambacho ama sisi hatuna na hatuwezi kuwa nacho na huu ni sehemu ya utamaduni mpana wa Waafrika kutojiamini. Kama ukifanya uchunguzi kidogo tu utagundua kwamba Waafrika sisi tunajivunia mambo manyonge na kudhani unyonge huo ama ni majaaliwa ya kimaumbile kutoka kwa mwenyezi muumba ama ndiyo hasa uungwana wenyewe na ugonjwa huu uko ndani ya jamii kuanzia watawala walio wengi hadi sisi watawaliwa na hivyo hakuna kati yetu anayeweza kumwambia mgeni umekosea ama hili kwa hapa si sahihi. Mara nyingi nimesoma na kusikia watu wengi wakilalamikia tabia ya wageni kuja nchini wakiwa na brifkesi zao tu na kisha kukopa fedha na kuanzisha biashara kubwa wakitumia fedha zetu na rasilimali zetu na kujiondokea wakituacha maskini kama walivyotukuta. Walio wengi wanawalaumu watawala kwamba wameshindwa kuweka sera nzuri zenye kumsaidia mwananchi kujipatia matunda yatokanayo na yeye kuwa na asili ya rasilimali husika na kwa sehemu wanaweza kuwa sahihi lakini nadhani wanachokisahau wakosoaji hawa wa watawala ni ukweli kwamba kwanza umaskini wa waafrika si umaskini wa rasilimali bali umaskini wa mawazo. Wengi wetu tuna utajiri wa mawazo duni. Pili wakosoaji hawa wanasahu kwamba viongozi tulio nao leo wanatokana na jamii yetu wenyewe na hivyo ikiwa tuna watawala wabovu, ni mazao ya moja kwa moja ya jamii mbovu hasa kwa vile Nyoka hawezi kuzaa Mjusi hata kama kimaumbile viumbe hawa wanafanana kwa sehemu.
Ili kujua unakowenda, wanahistoria wanakubaliana kwamba ni lazima kujua kwanza kule unakotoka na hivyo turejee walau kidogo historia ya bara la Afrika ingawa mengi tumeyasoma kwenye shule za msingi na sekondari. Pana vitu kadhaa hata hivyo ambavyo ama kwa makusudi ya waandishi wa mitaala ya historia tuliyofunzwa mashuleni au kwa sababu wakati vuguvugu la kudai uhuru lilipoanza, wakubwa wale walitengeneza mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba tunaendelea kuzilisha akili zetu vitu ambavyo havitatusaidia kufikiri zaidi ya wanavyotutaka kufikiri ili waendelee kututawala kupitia kile kijulikanacho leo kama ukoloni mkongwe, basi mengi ya tuliyofundwa kwenye masomo ya historia mashuleni japokuwa yana ukweli usiopingika, lakini si ukweli unaotusaidia ama kujivunia kuwa sisi ama kuamsha hali ya kujitambua na kuendeleza juhudi zetu katika kuwa watu bora. Kwa hiyo changamoto yetu ya kwanza ni kubadili kabisa mfumo wetu wa elimu na hapa nazungumzia mfumo wote kwa maana ya elimu rasmi na ile isiyo rasmi.
Ni ukweli wa kihistoria kwamba mfumo wa elimu utumiwao leo Tanzania na kwingineko kwingi barani Afrika ni mwendelezo ama mazao ya mfumo wa elimu ya kikoloni ambao kwa hapa nchini pamoja na kwamba mfumo huu umechanwa na kutiwa viraka kadhaa, bado haujawa mfumo wa mapinduzi ya kifikra unaomuwezesha mTanzania kufikiri zaidi ya yale anayoyaona na kuyasikia na hivyo si ajabu kwamba hadi sasa ni wachache kati ya wasomi wetu waliotoka vyuoni na kuanzisha shughuli zao wenyewe zaidi ya kusubiri ajira. Hata uwezo wa wasomi wetu kujitambua na kutumia vipawa vyao kwa ajiri ya kujiletea maendeleo ni mdogo na si ajabu kwamba wafanyabiashara wakubwa wa Tanzania, wasanii wakubwa, waandishi mahiri na kadhalika ni watu amabo walianza na elimu ya msingi na wengine kujiendeleza baada ya kufanikiwa huku wenyewe elimu kutoka vyuoni wakiwa ni watumishi wa hawa. Ni ajabu pia kwamba wengi wetu hata hatujui tofauti iliyoko kati ya mfumo uitwao Rasmi na ule usio rasmi na mchango wake kwenye maisha yetu ya kila siku na hivyo tumejenga mitizamo isiyoendana na mazingira na hata changamoto zetu. Hili laweza kudhihirika kwenye maeneo mengi na nitaje machache. Kwanza vipaumbele vyetu kama watu mmoja mmoja na hata taifa na bara kwa ujumla vinaendeshwa zaidi na mahitajio ya leo kuliko kesho yetu kama kizazi. Sasa tusizungumzie hili katika uendeshaji wa taasisi za serikali tu ijapokuwa ni kweli kwamba hata nyingi ya taasisi zetu za kitaifa zinatafuta matokeo ya kizazi hiki bila kufikiri vizazi vitatu vine mbele, lakini hata kwenye maisha ya mtu mmoja mmoja, ni wachache wanaoanzisha biashara ama kufanya shughuli yoyote ya kimaendeleo kwa ajiri ya vizazi vijavyo baada yao na hili si jambo dogo. Si ajabu basi kwamba kwa sababu ya kuwa na vipaumbele finyu, matumizi yetu ya rasimali watu, rasilimali pesa na hata muda havitumiki ipasavyo na hatuwekezi badala yake tunatumia kila tulicho nacho. Tabia hii ya matumizi makubwa kwa ajiri ya kujionyesha tu inaonekana kuanzia kwa mtu mmoja mmoja ambapo kijana anayetoka chuo kikuu leo na ambaye wazazi wake wamemlea na kumpeleka shule wakiishi kwenye nyumba ya vyumba viwili na sebule, miezi sita baada ya kupata ajira ama kuanzisha bishara, anapanga nyumba ya mamilioni kwa mwezi ili tu kuendana na kile anachodhani ni mahitaji ya nafasi yake katika jamii, hadi kwenye matumizi makubwa ya watawala wanaotumia kodi za nchi kujinunulia magari makubwa ya kifahari ambayo hata hivyo ukiwachilia unafuu wa barabara zetu ulioko sasa, huyaacha nyumbani na kupanda ndege kwa kodi za wananchi wanapokwenda kwenye ziara maeneo ya mbali na hivyo magari hayo kuishia kuwachukua waheshimiwa hawa kutoka majumbani kwao hadi makazini na kwenye warsha na makongamano ya ndani ya miji yao. Ufahari huu kwa faida ya nani?.
Tazama matumizi ya muda wa watendaji kwenye maofisi ya umma hadi kwenye maisha binafsi ya vijana walio nguvu kazi ya taifa na hutasita kujiuliza ni kwanini tunatumia muda wetu kufanya vitu, kusoma vitu, kuzungumza vitu, kukaa na watu ambao hawana mchango madhubuti kwenye kesho yetu na kizazi baada yetu?. Ukiingia kwenye mahoteli, mabaa na maeneo mengi ya starehe, utawakuta vijana kwa wazee wakijiburudisha kwa vinywaji na vitafunwa nusu au hadi robo tatu ya siku nzima na mazungumzo yanayoendelea hapo hayana mchango wa kuchukua hatua yoyote kesho yake kwa ajiri ya maendeleo zaidi ya kujadili siasa, mahusiano ya kijinsia, na mambo yanayoendelea katika vidunia vyetu vidogo tunavyoishi.
Si sahihi kulaumu tu pasina kujaribu kubainisha moja ya vyanzo vya tabia hizi na tumesema hapo awali kwamba elimu ipatikanayo kwenye mfumo rasmi ni duni na isiyotuwezesha kufikiri vyema na hivyo sisi pia ni waathirika wa mfumo mbovu ulioachwa tangu ukoloni wa kufundisha watu kwa ajiri ya kuwa watumwa na si watawala. Imempasa binadamu kuyatawala mazingira yake badala ya kuwa mtumwa wa mazingira hayo na hili lilifundishwa sana kwenye mifumo yetu ya elimu kabla ya ukoloni mkongwe ambapo kwa mazingira yao, jamii ilihakikisha kwamba vijana wake wanafundishwa jinsi ya kukabiliana na majukumu yao na kutawala mazingira yao siyo tu ya kiuchumi, bali ya kijamii. Jambo hili limepotea kwenye mfumo wetu wa elimu wa sasa ambapo vijana hujifunza jinsi ya kuwa wafanyakazi kwa watu wengine katika taaluma wanazopewa huko mashuleni kwao. Swali linabaki ikiwa elimu katika mfumo usio rasmi inatosha kuamsha udadisi ambao ukichanganywa na elimu hii ya mfumo rasimi, ambayo japo inahitaji marekebisho makubwa, ungeweza kuibua uwezo wa vijana kujitambua na hivyo kushadidia mabadiliko katika jamii?. Ni aibu iliyoje kwamba hata elimu katika mfumo usio rasmi imebunguliwa kabisa na hata pale ambapo ingalipo, imepoteza mantiki na heshim yake huenda kwa sababu ya kusimamiwa na watu waliokwishaharibika kimaadili.
Ebu tuzungumze juu ya ukweli kwamba elimu katika mfumo usio rasmi ilitolewa tangu kale kuanzia ngazi ya familia kwa familia kuwa na miiko ya familia, hadi jamii nzima kuwa na miiko ya jamii hiyo na sasa jamii kubwa ya Watanzania na hata Waafrika hawana tena kile kiitwacho miiko iwe ile ya familia ama ya jamii nzima kwa maana ya kaya, kijiji, kabila na hata taifa kwa ujumla wake. Ni ajabu kwamba wakati tunapopigia kelele ongezeko la vitendo vya rushwa na kukosekana uzalendo miongoni mwa watendaji wa serikali, tunasahau juu ya ukweli kwamba familia zilizo chanzo cha watendaji hao ziko katika hali mbaya ya maadili ambapo familia zinaheshimu zaidi fedha kuliko utu hasa kwa vile thamani ya mwanafamilia inategemea kiwango cha fedha anayomiliki. Wakati baba anapojenga nyumba ya kifahari iliyo zaidi ya mshahara wake tena kwa kipindi kifupi tu, si mkewe, wane, wala ndugu zake wanaohoji mzee wa familia amewezaje kufanya jambo hilo kwa hali ya uchumi wao, bali baba huyu anakuwa shujaa wa familia yake kwa vile ameikomboa katika umaskini. Si ajabu leo kwamba wakati vizazi kadhaa kabla yetu watu waliona haya kutuhumiwa kwa ukosefu wa maadili katika utendaji wao, leo watoto wa wahujumu uchumi wan chi yetu wanasoma shule moja na watoto wa wahujumiwa na hawazomewi mashuleni kwao, familia hizi zinasali kwenye makanisa na misikiti ya jamii yao na hakuna anayewanyooshea vidole na watu hawa wanaishi kama miungu watu kwenye jamii yao na hakuna anayewaadhibu hata kwa kuwanyooshea vidole tu kwa vile hilo halina msingi tena. Wako ambao wanakumbuka nyakati zile ambapo jamii ilikutana na kujadili matatizo yake kama wizi, na kadhalika kwenye jamii hiyo na hata ushahidi wa kutosha ulipokosekana kumchukulia mtuhumiwa hatua za kisheria, bado kula za wananchi wa eneo husika zilitosha kumwadhibu mtu huyu kwa kumpa ama shughuli fulani ya kijamii kama adhabu ama kumtenga kwa kipindi fulani na kadhalika. Sishauri kwamba turudi huko, lakini kwamba kama jamii na hata mtu mmoja mmoja ni lazima tujichunguze ni kwa kiasi gani tumechangia ama kutorithisha taratibu nzuri zilizokuwa sehemu ya mila na desturi zetu katika kusimamia maadili ya watu wake.
Madhara ya kiafya yatokanayo na jando na unyago yamefanya mambo haya kuwa haramu katika jamii, labda kwa vile ni ukweli kwamba sehemu ya mafunzo yake imekuwa ikihamasisha ngono katika umri mdogo na hivyo kusaidia kuenea kwa magonjwa kama ukimwi, lakini najiuliza ni kwanini pamoja na ajari nyingi za barabarani hatujaacha kutumia magari bali tumekuwa tukitafuta mbinu mbadala za kuboresha miundombinu yetu na hata kuwafundisha wataalamu wetu kwenye maeneo hayo jinsi ya kuwa salama zaidi, lakini tumeshindwa kama jamii kuzilinda sehemu nzuri za tamaduni zetu ambazo zilikuwa na faida kwa vijana wetu na sasa kila mmoja anaona ufahari kujifananisha na wamagharibu tukiwa sote tunajaribu kuishi angani huku tukiwaza baharini!?.
Si ajabu kwamba leo vijana wa kitanzania wanaonea fahari dini zao kuliko utaifa wao. Nakumbuka mmoja wa marafiki zangu kwenye mtandao wa kijamii alipochangia kwenye makala ya udini Tanzania akisema; “…dini ndiyo halisi, taifa kitu gani, taifa ni michoro ya wazungu ambao walikuja kutibia tu mali zetu….” Na kwa sehemu nadhani nakubaliana na huyu ndugu, lakini anasahau pia kwamba Waafrika kwa miaka dahali walikuwa na jinsi yao ya kuabudu na ilivyokuwa na matokeo chanya siyo tu kwenye masuala ya kiuchumi bali hata kimaadili. Wakati mvua zilipogoma kunyesha kwenye jamii nyingi za kiafrika, watu walikusanyika chini ya mti na kufanya matambiko na mvua zikanyesha na binafsi naamini Mungu alijibu maombi ya watu hao kwa kadri walivyojisogeza kwake kwa njia walizozijua wao. Lakini pia ikiwa watu fulani walivunja kanuni fulani ya kimaadili katika jamii, mfumo wa imani za kiafrika ulihakikisha jamii nzima inapata adhabu na hivyo kulazimika kujichunguza na kuwapata wakosaji ambao waliadhibiwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za imani ya jamii husika na mabalaa yakakoma. Kanuni hizi pamoja na ukali wake, lakini zilikomesha mimba za utotoni, zilikomesha watu kuvunja ndoa bila utaratibu na kadhalika na hivyo watoto walilelewa kwenye taasisi ya familia iliyo chanzo cha jamii na taifa linalojitambua.
Moja ya athari kubwa za dini za kigeni ni ukweli kwamba watu wamekuzwa na dini hizi kuamini kwamba “unaweza kufanya dhambi kwa kadri uwezavyo ila utapata hukumu siku ya mwisho” na kwa vile siku ya mwisho iko mbali sana ama hakuna aliyewahi kushuhudia matokeo ya watu waovu hiyo siku, basi tumekuwa kizazi cha watu wanafiki tunaojazana misikitini na makanisani nab ado jela zetu zimejaa akina John na Juma nab ado ati tunajisifia dini na kudharau utaifa wetu. Dini hizi zote mbili kubwa barani Afrika yaani Ukristo na Uislamu zililetwa kwetu na wakoloni na wote hawakutenda yale waliyofundisha na ushahidi upo, nashindwa kuelewa ni kwanini hadi sasa tuko tayari kubaguana sisi kwa sisi tukitukuza upuuzi tuliolishwa na wakoloni wa babu zetu?. Ndiyo, wakati wakoloni wa kizungu walio mazao ya uenezaji wa ukristo waliwaua babu zetu kwa kuwanyonga hadharani huku wakitufundisha juu ya amri ya Mungu isemayo “Usiue”, wakoloni wa Kiarabu waliwauza babu zetu utumwani wakiwatesa na kunyanyasa vibaya huku wakitufundisha juu ya upendo wa ndugu wenye imani ya mwenyezi na kadhalika. Ni aibu iliyoje leo, kijana mwenye uelewa na mwenye akili nzuri kukubali kudhuru maisha ya mtu, kumfungia mtu milango ya mafanikio ati kwa misingi ya dini yake? Tunapokuwa tukifanya hivi, tunajiuliza wanetu baada yetu watakuwaje au ndiyo tunawaza kwamba sisi tutakuwa mbinguni ama peponi na vyovyote upendavyo wewe kuita huku dunia ikiwa imefikia mwisho?. Kama itakuwa haijafika mwisho vizazi saba kuanzia sasa unadhani wanetu watakuwa watawala wa maisha yao ama watakuwa watumwa tena na sisi tukiwa tumechangia kuwarudisha wao kule ambako babu zetu walimwaga jasho na damu kututoa sisi?.
Uhuru wa vyombo vya habari ulio sehemu ya utandawazi, umeruhusu kwamba sasa vyombo vya habari hasa redio na magazeti yanafundisha vijana wetu maadili mabovu ya watu walioharibika akili zao. Mitandao ya internate isiyo na udhibiti inaruhusu watoto wetu kuona yale wasiyopaswa kuyaona walau kwa umri fulani na kadhalika na si taasisi za serikali wala familia na mtu mmoja mmoja anayefanya juhudi za kutosha kuzuia madhara ya mitandao hii kwa kizazi kijacho baada yetu, uzembe huu utatugharimu sana.
Wakati tunaporuhusu watu wengine kutuamria aina ya Demokrasia na tafsiri yake na kwamba demokrasia yoyote haiwezi kuwa Demokrasia mpaka kwanza ifikie viwango vya wamagharibi na wakoloni wale, tunapoteza mwelekeo na ndipo tunaposhuhudia watoto wetu wakienda halijojo na sisi hatuna la kufanya juu ya hilo. Walau kwa siku za karibuni taasisi za kijamii na baadhi ya wanaharakati wameanza kulielewa hili, lakini tunakumbuka wote miaka saba hadi kumi nyuma ambapo vyombo vyote vya habari vilijaa matangazo ya “haki ya mtoto” kutoka kila kona na ufadhili wa matangazo haya na harakati hizi ukitokea kulekule kwa watafsiri wetu wa demokrasia. Sikatai kutetea haki za watu, lakini najaribu kuelewa ni kwanini watu wazima na akili zetu waliamua kwa makusudi kuwekeza fedha, muda na rasilimali watu kufundisha watoto msururu wa haki zao bila kuwafundisha hata moja ya wajibu wao?. Hivi walichokuwa wakijaribu kufanya wanaharakati hawa ni kutueleza kwamba watoto wanaujua wajibu wao kwa asili ila haki zao ndizo hazijulikani ama lah!?. Hakuna mahala popote ambapo haki inatolewa bila wajibu na hilo linajulikana na watu wote, nisichofahamu ni ikiwa wachezaji wa michezo hii ya hatari wanafahamu madhara ya michezo yao na ndipo ninalazimika kujihoji ikiwa kweli tunaiwaza kesho ya watoto wetu ama tunajifikiria sisi tu na kudhani kesho ya wanetu itajitengeneza yenyewe?.
Mwandishi: Godfrey M. Kamenge
Cell: +255 785 66 88 59.
E-mail: kamengez@hotmail.com
Next Post Previous Post
Bukobawadau