Waliokutwa na maiti yenye mihadarati wapata dhamana
Dar es salaam. Polisi Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya juzi limewaachia kwa dhamana watuhumiwa wawili wanaodaiwa kukutwa na maiti iliyokuwa na dawa tumboni zinazodhaniwa ni za kulevya.
Mkuu wa Kitengo hicho, Kamanda wa Polisi Godfrey Nzowa, aliliambia gazeti hili jana kuwa katika upelelezi wao wameshindwa kuwabaini moja kwa moja watuhumiwa hao kama wanahusika na tukio hilo au la.
“Watuhumiwa hawa wapo nje kwa dhamana na kwamba kama upelelezi wetu ukikamilika watu hawa wakakutwa na hatia basi watafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Nzowa.
Tukio hilo lilitokea Septemba 22 mwaka huu jioni maeneo ya Tabata ambapo maiti huyo aliyejulikana kwa jina la Rajabu Kidunda (43) alikutwa amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha akiwa amelala kwenye godoro liliotandikwa sebuleni nyumbani kwa watuhumiwa hao.
Inadaiwa kuwa, Kidunda alifika kwenye nyumba hiyo akiwa mgonjwa akitokea wilayani Newala mkoani Mtwara alikokwenda kuchukuliwa na watuhumiwa hao kisha kuletwa Dar es Salaam.
Baada ya kupata taarifa hizo za kifo hicho cha utata makachero wa polisi walimchukua maiti huyo na kumfanyia uchunguzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) ambapo aligundulika kuwa na pipi 33 aina za Heroin zenye uzito wa gramu 561.
Kwa mujibu wa Kamanda Nzowa, taarifa za awali zilizothibishwa na Mganga Mkuu kutoka katika moja Hospitali wilayani Newala, zinaeleza kuwa baada ya kupata ahueni Kidunda alichukuliwa na watuhumiwa ambao mmoja kati yao anadaiwa kuwa ni mkewe.
Aliongeza kuwa, watuhumiwa hao wamepewa masharti ya kuripoti kwenye kituo cha polisi husika kwa muda waliopangiwa huku polisi wakiendelea kufanya upelelezi ikiwamo kubaini marehemu alikozitoa dawa hizo.