Zitto sasa aanika mshahara wa Rais
Igunga. Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe amesema sababu ya kutaja mishahara ya viongozi wakuu wa nchi ni kuzuia mianya ya watu wachache kuiibia nchi kutokana na usiri wa jambo hilo.
Zitto alitoa kauli hiyo jana mjini Igunga, wakati akitangaza mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mujibu wa Zitto, kwa mwaka kiongozi huyo wa nchi analipwa Sh384 milioni ambazo ni wastani wa Sh32 milioni kwa mwezi bila kukatwa kodi.
Hatua ya Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC), kutaja mshahara wa rais inakuja wiki moja baada ya kutaja mshahara wa Waziri mkuu kuwa ni Sh26 milioni kwa mwezi pasipo kukatwa kodi
Zitto alisema hoja ya msingi si kiasi wanancholipwa viongozi hao walioajiriwa na wananchi bali ni usiri unaofanywa juu ya kiwango hicho. Alisemaha ni jambo la kusikitisha kuona mwalimu anayelipwa mshahara wa Sh200,000 kwa mwezi ukikatwa kodi huku viongozi wa kuchaguliwa wakiwa wanapokea mishahara mikubwa pasipo kukatwa kodi.
Alisema katiba ya sasa Ibara ya 43(1), inaeleza kuwa rais atalipwa mshahara na malipo mengine huku ibara hiyo hiyo kifungu cha pili ikizuia mshahara na marupu rupu kupunguzwa, hali aliyoelezea kuwa ni muhimu katiba mpya ikabadilisha sheria hizo kwa manufaa ya nchi.
“Kwa hiyo hata kesho kama Dk Slaa akiwa Rais na akataka kupunguza mshahara wake kwa katiba hii hawezi na hili jambo si sahihi kwani viongozi wa ngazi hizi wanapata kila kitu bure kutoka Serikalini,” alisema Zitto.
Zitto alisema kuwa kitendo cha Serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, hakikuzingatiwa kulingana na uwazi uliowekwa kwa kuandika uwazi wa viwango vya mishahara.
Alisema kuwa waziri aliyehusika kufunguia magazeti hayo hakufikiria kwa makini kutokana na kuwa na uelewa mdogo na kuongeza kuwa hakuna kosa lolote linalopelekea kufungiwa magazeti hayo kutokana na ukweli ulioandikwa.
Mwananchi.