Bukobawadau

Kutimuliwa kwa Chiza ni Nape na ukomavu wa kisiasa

Na Prudence Karugendo
KATIBU  wa Itikadi na Uenezi wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi, Nape Nnauye, bado ni kijana kiumri, ila katika siasa anaanza kuonesha ukomavu uliouzidi wa wengi waliomtangulia kiumri. Hiyo imejionesha kutokana na Nape kuwatolea uvivu baadhi ya mawaziri wa serikali ya bosi wake, Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama anachokitumikia Nape, CCM.
Alichokifanya Nape cha kutaka mawaziri watatu, Mhandisi Christopher Chiza – Kilimo, Chakula na Ushirika, pamoja na naibu wake, Adamu Malima, na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, watimuliwe kazi mara moja, kinawashinda wengi akiwemo hata aliyewateua kushika nyadhifa hizo, Rais Kikwete mwenyewe.
Fikiria mtu anapewa nafasi ya kumsaidia rais wake katika kuyatafuta maendeleo ya nchi na wananchi, mtu huyo anaivurunda, lakini aliyemteua kushika nafasi hiyo anamuonea haya ya kumuondoa na kuwajaribu wengine ambao wako tele wenye uwezo na nafasi husika!
Kwahiyo kitendo cha Nape kusema kwamba mawaziri wanaovurunda nafasi zao watimuliwe kinapaswa kupongezwa bila kujali anayempongeza anafuata itikadi ya chama gani cha siasa.
Hiyo inaletwa na ukweli wa kwamba rais ni wa nchi nzima, sio wa CCM, Chadema, CUF wala chama chochote kingine cha siasa. Hivyo anayoyafanya ni kwa faida ya nchi yake na watu wake katika ujumla wao bila kuzijali itikadi zao za kisiasa. Rais  anapomteua mtu akamsaidie katika hilo anakuwa amelenga kwa faida wananchi wake wote kwa ujumla.
Lakini kwa bahati mbaya wapo baadhi ya watu, hususan wapenzi wa chama anachotoka rais, wanaokichukulia kama usaliti kitendo cha kuusahihisha uteuzi wa rais bila kuelewa kwamba kwa kufanya hivyo, kumsahihisha, ni kumsaidia rais vilevile.
Maana rais sio Mungu, ni binadamu kama tulivyo mimi na wewe. Rais anaweza akajiaminisha na ujuzi wa mtu katika mambo fulani na hivyo kuona anamfaa katika usaidizi, lakini hatahivyo ni vigumu kwake kuelewa mambo yatakuwaje pale mtu anapokuwa amenogewa na nafasi anayokuwa amepewa kumsaidia rais. Uwezo huo anao Mungu peke yake.
Ni kwa sababu hiyo nataka nimpongeze Nape Nnauye kwa ujasiri wake wa kutamka wazi kwamba mawaziri ambao mpaka sasa wamegeuka mzigo usiobebeka kwa mteuzi wao watimuliwe mara moja. Kwa kauli hiyo ni wazi kwamba Nape anampenda rais wake, nchi yake na wananchi wenzake. Hataki kuwaona wananchi wakiteseka kutokana na watu wanaojisahau baada ya kuaminiwa na bosi wao.  Huo ni ujasiri wa Nape uliotukuka.
Sio rahisi kujionesha kwamba unampenda rais wako na unamnyenyekea kwa kumuachia ahenyeke na mambo yanayotokana na maamuzi yake, uko ni kumkomoa rais wako wala sio kumpenda na kumnyenyekea. Anayempenda na kumnyenyekea rais wake atamsaidia kwa kumuonesha dosari zilizo kwenye maamuzi yake, kusudi rais azifanyie kazi dosari hizo na kujiondolea mzigo unaomuelemea ukitishia kumchonganisha na wananchi anaowatumikia. Hivyo ndivyo alivyofanya Nape.
Katika nchi zilizoendelea, ambazo tumejizoesha kuzichukulia kana kwamba zina ubia na Mungu, na hivyo kuziomba misaada ya kila aina kama vile bila zenyewe sisi hatuwezi kuwepo, huwa hakuna unafiki wa kisiasa.
Kule inapotokea jambo limeenda kombo katika uendeshaji wa nchi mhusika hasubiri kukumbushwa na bosi wake ili awajibike, mara moja anaamua mwenyewe kuachia ngazi. Hiyo ni moja ya jitihada za kumpunguzia bosi wake mzigo, anaonesha upendo kwa bosi wake. Na mambo yanapokuwa yamezidi hata bosi mwenyewe anaachia ngazi ili wananchi wakamtafute mwingine wa kuwa kinara wao. Huo nao ni upendo wa kinara wa nchi kwa watu wake.
Sielewi ni kwa nini katika nchi nyingi za kimasikini, hususan katika Bara la Afrika, mambo yanakwenda kinyume pasipo kugundua wala kuhisi kwamba unyume huo ndio unaotufanya tuwe dhalili mbele ya wenzetu!
Panapotokea mtu mwenye dhamana fulani anasababisha mambo yaliyo mustakabali wa nchi na wananchi yaende kombo, ama kwa bahati mbaya, kwa makusudi au kwa uwezo mdogo alio nao mhusika, lakini anaamua kufumba macho kana kwamba hakuna chochote kilichotokea, bosi wake naye anaamua kujikalia kimya hapo ni lazima pawe na hitilafu. Kibaya zaidi hata wananchi, ambao ndio waathirika, nao wanaamua kutulia tuli!
Wakitusema wanaotufadhili, ambao kwa njia moja au nyingine tunaamini wana ubia na Mungu, tunaanzisha malalamiko kwamba wanatudhalilisha! Hivi ni kweli wanatudhalilisha au tunajidhalilisha sisi wenyewe?
Kwa matiki hiyo, ndiyo sababu nimeona kuna umuhimu wa kumpongeza Nape Nnauye kwa ujasiri wake wa kuuweka wazi udhaifu unaojionesha katika mpangilio wa serikali iliyoteuliwa na bosi wake kichama.
Hata kama wapo watakaomuona Nape kaenda nje ya mstari, ila kiukweli yeye ndiye aliyeonesha msaada zaidi kwa bosi wake kuliko walio na nidhamu ya kinafiki ya kwamba “Mfalme kapendeza kwenye nguo isiyoonekana kwa wenye dhambi tu” kumbe mfalme yuko uchi!
Katika mawaziri watatu aliowasema Nape, mimi kwa hapa nitawagusia wawili tu, Chiza na Malima. Sio kwamba yule mwingine hana tatizo, analo tena kubwa sana, na wizara anayoisimamia ni nyeti mno. Ila nimeamua kuwaongelea hawa wawili, waziri na naibu wake, kwa vile nimekuwa nikiiandika wizara hiyo kwa muda mrefu kutokana na msukumo wa wakulima.
Pamoja na mambo mengine yanayolalamikiwa na wakulima, jambo kubwa ambalo limelalamikiwa na wakulima kiasi cha kukalibia kulifanyia matanga baada ya kuona kama limeshindikana kupatiwa ufumbuzi wa kulinusuru, ni ushirika. Ushirika unakufa nchini wakati waziri mhusika akiwa na kila nyenzo za kuunusuru ila akiwa anakosa utashi wa kufanya hivyo.
Kwa kutotaka kumsaidia bosi wao Waziri Chiza pamoja na Naibu wake, Malima, wako tayari kuuona ushirika ukiwafia mikononi wakiwa na uhakika kuwa atakayelaumiwa kwa kifo hicho ni Rais Jakaya Kikwete, kwa vile wananchi, wengi wao wakiwa ni wakulima, ndiye waliyemchagua ili,  pamoja na mambo mengine,  akawalindie maslahi yao, na wala hawakuwachagua mawaziri.
Kufuatia tatizo hilo nimeandika sana, tena mara nyingi, kumshauri Waziri Chiza aingilie kati na kuunusuru ushirika kwa kuyatumia mamlaka aliyopewa kikatiba, kwa vile ni yeye aliye waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Sababu haina maana mtu kuitwa Waziri wa Ushirika halafu ukakubali kuuona ushirika ukikufia mikononi ila wewe ukiendelea kunufaika tu na cheo hicho, ambacho kwa hilo kinakuwa hakina maana yoyote.
Nilijaribu kumtolea Waziri Chiza mfano halisi wa chama changu kikuu cha ushirika ninachokifahamu kwa karibu cha KCU (1990) Ltd.. Nilimwambia Chiza kuwa chama hicho kinakufa kutokana na uongozi wake uliopo kuupa kipaumbele ubinafsi, ambapo viongozi wa ushirika ndio pekee wanaojinufaisha na ushirika huo wakati wanaushirika, wakulima, hawaambulii lolote wala kuelewa ni kwa nini kuna kitu kinachoitwa ushirika.
Alichopaswa kukifanya Chiza ni kuwaelekeza walio chini yake, hasa Mrajis wa Vyama vya Ushirika, akautimue uongozi wote wa KCU (1990) Ltd. na kuwambia wanaushirika wakapange upya safu ya uongozi wa ushirika huo.
Baada ya kuona kuwa Waziri Chiza, kwa sababu anazozielewa yeye, hakuutilia maanani ushauri wangu, nikamgeukia Rais Kikwete, nikauliza kwa nini anamuachia Chiza aunyonge ushirika?
Sikuelewa Rais Kikwete alilichukuliaje swali langu hilo, ila kusema ukweli nimefarijika na kauli ya Nape Nnauye ya kwamba Chiza ni mmoja wa mawaziri walio mzigo kwa Rais Kikwete. Kauli yake ya kwamba mawaziri hao mizigo watimuliwe naiunga mkono kwa asilimia mia moja.
Naamini kwamba Nape anaenda sambamba na yanayojitokeza kwa wananchi. Anayaangalia matatizo yanayowapata wananchi na kuangalia yanasababishwa na nini na yanaweza kutatuliwaje.
Kwahiyo, kwa msaada wa Nape, Rais Kikwete anapaswa kupima uzito kati ya wakulima, ambao ndio wanaounda ushirika, na Chiza, waziri anayeusimamia ushirika, na kisha kuona ni upande gani wenye uzito zaidi. Sidhani kama rais anaweza kumuona Chiza ndiye mwenye uzito mkubwa  kuliko wakulima, walio pia wapiga kura wake,  kwahiyo akaamua kumbeba mtu mmoja na kuwatelekeza wakulima walio katika idadi ya mamilioni.
Kama Chiza hataki kuonesha upendo kwa bosi wake, kwa kuyatazama anayoyafanya na kuona kuwa  kavurunda sana na kugeuka mzigo usiobebeka hivyo kuamua mwenyewe kumuondolea mzigo huo bosi wake, basi bosi anaweza kuonesha upendo kwa msaidizi wake huyo na kumuweka pembeni ili akwajaribu wengine kutoka kwenye hazina kubwa aliyo nayo isiyopungua idadi ya watu milioni 45, ili wananchi wanaobaki waweze kuendesha maisha yao kwa uhakika na usalama zaidi.
Narudia kusema kwamba Nape Nnauye kaonesha ukomavu wa kisiasa ambao sikutegemea kama ungetoka kwa kijana wa aina yake.
0784 989 512 
Next Post Previous Post
Bukobawadau