Bukobawadau

Maruku Vanilla Waendelea na Zoezi la Kugawa Miche ya Vanilla

Kikao na Wakulima
Mkulima Akifurahia Miche
Mkurugenzi wa MVFP Ltd, Bw. Fadhil Omar akigawa miche ya Vanilla
Kampuni ya Maruk Vanilla Farming and Processing Ltd yenye makazi yake kijijini Maruku, Kanyangereko-Ntoma, Bukoba (V) imeendelea na jitihada zake za kulifufua zao la vanilla na kujidhatiti karibu na wakulima. Wiki iliyopita Wakurugenzi wa Maruk Vanilla waliwatembelea wakulima wa vijiji vya KIBONA na KATOJU KATA ya KASHARU. Katika ziara hiyo walipata kuzungumzia mambo mbalimbali ya kufufua zao la vanilla na kuboresha maisha ya wakulima. Pia waligawa miche ya vanilla kwa wakulima ili waikapande na kuongeza uzalishaji. 

Akizungumza na Bukobawadau Blog  ya habari za maendeleo, Mkurugenzi wa Masoko Bw. Fadhil Ibrahim Omar alisema kampuni yao inafanya kila jitihada ili kila mkulima walau awe na uwezo wa kuzalisha kilo 100 kwa msimu. Hii itamfanya aweze kunufaika na huduma za ziada zitolewazo na Maruk Vanilla baada ya mauzo. Bw. Fadhil aliifahamisha Blog hii kwamba mpango wao ni kumpatia kila mkulima wa vanilla Bima ya Afya ya mwaka mzima. Lakini ili haliwezekani kama mkulima hawezi kuzalisha mazao yanayofikia walau Kilo 100 kwa msimu. Hivyo jitihada ya pamoja inahitajika kuongeza uzalishaji. “Sisi MVFP Ltd tunatimiza wajibu wetu. Tumewapatia wakulima miche ili wapande. Lililobaki ni juhudi binafsi ya mkulima” alisema Bw. Fadhil.

Bukobawadau Blog  ilitaka pia kujua juu ya kuyumba kwa bei ya vanilla katika masoko ya Kimataifa na jinsi gani wakulima wa Bukoba watahathirika. Akijibu swali hili, Bw. Fadhil aliwahakikishia wakulima kwamba kuanzia mwaka jana bei ya vanilla imekuwa ikipanda bila kushuka katika masoko mbalimbali ya viungo ulimwenguni. Ni matarajio ya wadau kwamba hakuna dalili za kushuka kwa bei ya zao hili katika miaka mitano ijayo. Hii inatokana na kupungua kwa uzalishaji na kuanguka kwa ubora wa vanilla inayozalishwa nchini Madagascar. Pia mahitaji yameongezeka kutokana na watumiaji wengi kupendelea vanilla ya asili badala ya flavored au artificial vanilla. Akithibitisha juu ya bei na masoko, Bw. Fadhil alisema Kampuni yake tayari ina mikataba mitatu ya masoko ya uhakika kwa miaka minne ijayo lakini changamoto kubwa ambayo mara nyingi imewakabili ni kupata mazao ya kutosha kutoka kwa wakulima. Aliongeza kuwa katika msimu ujao, MVFP Ltd inakusudia kuongeza pato la mkulima kwa wastani wa kila kilo ya vanilla kwa TShs. 2,000-3000/= ili kutoa motisha ya uzalishaji.

Kutokana na suala la kilimo kuwa mtambuka kwa maendeleo na kuondoa umaskini, timu nzima ya Bukobawadau Blog itaandaa makala maalumu na endelevu juu ya zao hili katika jitihada za kuiunga mkono Serikali katika mpango wake wa Kilimo Kwanza. Iwapo utakuwa na taarifa kwenye sekta hii ambazo ungependa zitolewe au kuwashirikisha watanzania, unakaribisha kuziwakirisha mezani kwetu kupitia Bukoba Wadau kwa email yetu  bukobawadau@gmail.com

Next Post Previous Post
Bukobawadau