SIKU ZA ZITTO CHADEMA ZINAHESABIKA...
Ndugu zangu,
Kwa kuyachambua magazeti ya leo, na kwa kusoma katikati ya mistari, ni dhahiri, kuwa siku za Zitto Kabwe Chadema kama mwanachama nazo zinahesabika.
Tundu Lissu anaripotiwa na Mwananchi akisema; "Wamefukuzwa katika uongozi kutokana na kuandaa mpango wa mapinduzi uliopo katika waraka wa 'Mkakati wa Mabadiliko 2013," alisema Lissu na kuongeza:(P.T)
"Hawa wote hawakuvuliwa madaraka kwa sababu ya taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu ukaguzi wa hesabu za chama, suala la posho kwa wabunge wala kuuza majimbo ya uchaguzi mwaka 2010." ( Mwananchi, Jumatano , Novemba 27, 2013)
Tafsiri yangu;
Hapa kikubwa kinachokosekana ni IMANI. Pande mbili zilizo kwenye mgogoro haziaminiani tena. Kama ni ndoa hapa imevunjika.
Rhetorik ya pande zote mbili haionyeshi kuwa wanaweza tena kukaa meza moja na kuaminiana. Kila mmoja anamtuhumu mwenzake. Hakuna aliye tayari kukubali tuhuma. Kitakachookoa hali hii ni kwa pande mbili kukaa meza meza moja, kuzungumza kwa uwazi na kukubaliana kwa dhati kufutiana tuhuma na kufungua ukurasa mpya wa mahusiano.
Vinginevyo, Zitto Kabwe anaelekea kwenye kufukuzwa uanachama. Anaweza kubaki kuwa Mbunge kwa njia ya mahakama. Lakini, atabaki kuwa Mbunge-pori.
Na je, mgogoro utakuwa umekwisha?
Jibu: Ni mapema mno kusema, na itategemea na itakavyopokelewa na Wananchi wa mitaani na vijijini.
Na tusubiri tuone.
Maggid Mjengwa.
Iringa.
0754 678 252
Iringa.
0754 678 252