Bukobawadau

Wakenya tupo katika majuto


“Tulionywa na Amerika kabla ya uchaguzi kwamba tukiwachagua Uhuru na Ruto tungejuta na sasa tumejuta. Wakenya milioni sita walimchagua Uhuru. Kweli sikio la kufa halisikii dawa.
Dalili ya mvua ni mawingu. Mawingu yanayofunika anga la Kenya wakati huu yanaashiria kwamba mvua itakayonyesha itasababisha mafuriko katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.
Ni kwa sababu hii wote wanaojali hatima ya nchi hawana budi kujitokeza kimasomaso ili kuona athari za vitendo vya Serikali ya Jubilee kwa nchi na kutafuta jinsi ya kuepukana nazo.
Jukumu hili liko juu ya mabega ya vyama vya upinzani haswa Muungano wa CORD unaoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na wengine.
Ni wakati wa CORD kuonyesha kuwa haiwezi kusita kueleza na kuihakiki Serikali ya Uhuru Kenyatta pia ni dhabiti na kwamba viongozi wake watakuwa wanazungumza kwa sauti moja wanapoikosoa Serikali.
Wengi walitarajia kwamba viongozi wa Cord wangetengana baada ya uchaguzi mkuu, lakini Raila, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula bado ni wanachama wa CORD.
Historia ya vyama vya kisiasa nchini inaonyesha kwamba, viongozi huunda vyama kwa lengo la kushinda uchaguzi lakini baada ya miezi michache vyama hivyo husambaratika.
Kwa mfano, kiongozi wa United Democratic From (UDF), Musalia Mudavadi anajitayarisha kujiunga na Serikali ya Uhuru kama waziri. Gazeti moja la kila siku limenukuliwa likiripoti kwamba, Mudavadi hivi karibuni ataingizwa kwenye serikali.
Tatizo nini?
Upinzani umegundua kwamba Serikali ya Jubilee imeanza kuonyesha kucha zake miezi michache baada ya kujifanya kwamba inafuata sheria na kulinda Katiba. Ilifanya hivyo kwa kuteua Baraza la Mawaziri inavyotakiwa kisheria, lakini sasa mambo yamebadilika.
Uhuru na Makamu wake,William Ruto, wameonyesha kuwa hawajali lolote zuri linaloiweka Kenya kwenye jukwaa la mataifa yanayowalinda wananchi wake. Kwa wiki moja iliyopita, Upande wa Serikali bungeni umepitisha miswada miwili inayorudisha nyuma hatua nzuri zilizokuwa zimepigwa.
Kumekuwa na kilio kikuu kutoka kwa Wakenya kuhusu hatua ya Serikali kutaka kuzima uhuru wa wanahabari na pia kukata msaada kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka kwa mashirika ya maendeleo ya nchi za Ulaya na Magharibi.
 Si jukumu la upinzani kuisifu Serikali na kuchochea maendeleo. Huu si wakati wa kupakana mafuta kwenye mgongo wa chupa kwani mshuka ngazi na mpanda ngazi kamwe hawawezi kushikana mikono.
  Jukumu lake ni kuhakikisha Serikali inafuata mkondo unaofaa inapoendesha shughuli zake. Ni jukumu la kusukuma Serikali ili izingatie ahadi zake zote ilizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni na uchaguzi na hatimaye wakati wa kuapishwa kwake Uhuru na Ruto Aprili 9, 2013.
Kuna orodha ndefu ya mambo yasiyofurahisha wengi nchini, na chimbuko la haya yote ni Serikali ya Jubilee. Wakenya bado wanajiuliza maswali kuhusu jinsi mkuu wa majeshi alivyokuwa amekana kwamba kikosi chake hakikupora mali wakati wa mashambulizi ya Westgate.
Maji yalipozidi unga, Serikali ilikiri kwamba kweli, wanajeshi walikuwa wamepora. Kwanini Wakenya wachukuliwe kana kwamba ni majuha? Mbona Serikali haikukiri mara moja kwamba makosa yalifanyika badala ya kujaribu kuficha ukweli?
Muswada wa ushuru wa chakula na bidhaa nyingine muhimu ulipelekea kupanda kwa gharama ilhali mapato ya wananchi ni yale yale. Baada ya kilio kutoka kwa raia, Serikali ilitoa sababu kwamba haikuwa inalenga bidhaa muhimu kama vile maziwa na mikate walipoupitisha muswada huu.
Sote twafahamu ni kina nani wanaoshikilia sekta ya maziwa na wangefaidi kutokana na kuongezeka kwa bei ya maziwa na bidhaa nyingine.
Isitoshe, kuna maswali mengi kuhusu jinsi pesa za umma zinavyotumiwa. Tangu vikao vya kesi zinazomkabili Ruto ianze The Hague zaidi ya mwezi mmoja uliopita, wabunge na wafanyakazi wa umma wamekuwa wakimtembelea kiongozi huyu kila wiki ili kumpa moyo kortini.
Je, wabunge na wafanya kazi wa umma wanaosafiri kila mara kumtembelea Makamu wa Rais wanafanya hivyo kwa kujigharamia au fedha za umma ndizo zinatumiwa?
Pia, Waziri wa Masuala ya Nchi za Nje, Amina Mohammed amekuwa kiguu na njia tangu ateuliwe. Kazi ya kutumikia wananchi imewekwa kando badala yake kesi ya Uhuru imepewa kipaumbele.
Mohammed ametembelea nchi nyingi kutafuta uungwaji mkono kwa kesi hizi. Uhuru na Ruto walikuwa wamewahakikishia wananchi wakati wa kampeni na hata walipokuwa wakifanya kampeni kwamba, kesi zao ni za kibinafsi. Lakini sasa zimekuwa za kitaifa na hata kimataifa. Wakenya wangetaka kujua pesa hizo zote za nauli na kadhalika zinalipiwa na nani.
Shirika moja lisilo la kiserikali, Mars Group linaunga mkono juhudi za Upinzani za kutaka kujua jinsi safari hizi za kila mara zinavyogharamiwa. Mkurugenzi Mkuu wa Mars Group Kenya,  Mwalimu Mati anataka Uhuru aeleze ikiwa matumizi ya pesa kwenye shughuli za kibinafsi kama hizi zilijadiliwa kama muswada katika Bunge la kitaifa na kupitishwa.
Upinzani ungetaka kujua mfuko wa fedha unaotumiwa na Uhuru na Ruto kuzuru nchi mbalimbali za Afrika kukutana na viongozi wa kisiasa barani ili wawaunge mkono kuhusiana na kesi za Hague.
Next Post Previous Post
Bukobawadau