Bukobawadau

ASEMAVYO KIJANA DENICE ISHENGOMA

 
Tunapoelekea mwishoni mwa mwaka 2013, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru sana wazee wangu kwa maana ya mabibi na mabwana na vijana wote wa mkoa wa Kagera waishio ndani na nje ya mkoa wetu,ndani na nje ya taifa letu kwa jitihada walizozifanya katika kufanya mageuzi ya kielimu,kiafya,kisiasa na kiuchumi kwa manufaa ya mkoa wetu na taifa kwa ujumla.
Nakiri kwa uwazi kabisa kuwa palikuwepo na madhaifu mbalimbali katika kutimiza ndoto zetu za kuleta mageuzi chanya katika nyanja za kielimu,kiafya,kilimo,kisiasa na kiuchumi ndani ya mkoa wetu lakinini udhaifu huu haupaswi kupewa kipaumbele au kikwazo katika kuundeleza mapambano dhidi ya maadui walioko mbele zetu kwa maana ya ujinga,maradhi,siasa chakachuzi,njaa na umaskini.
Napenda kuwahabarisha kuwa bado tunao muda mfupi lakini unaotosha kufanya mageuzi chanya yatakayotoa majawabu ya matatizo ya mkoa wetu katika sekta tajwa hapo awali na haya yote yanawezekana kwa kukataa kabisa tabia ya kulewa pombe na kuketi kwenye virabu vya pombe kutwa nzima katika siku zote za juma,kukaa kwenye vijiwe vya kahawa,kupunguza utegemezi uliokithiri,tabia ya kudharau au kubagua kazi,tabia ya uchoyo,tabia ya kujikweza,(Emyesipanko)tabia ya majigambo,tabia ya kukumbatia umaskini,tabia ya ubaguzi katika koo zetu,tabia ya kudekeza ndoa za mitara,kukumbatia mbinu za kilimo zilizopitwa na wakati,kuchagua viongozi na wawakilishi wetu kwa njia ya rushwa,n.k.
Kwa kuwa tunaelekea ukingoni mwa tawala zilipo kwa sasa,ni wakati muafaka kufanya tafakari juu utendaji wetu au dhidi ya utendaji wa watu tuliowafanya vioo vyetu tuone kama walitusadia kufikia malengo ya maendeleo ya mkoa wetu au walikuwa chanzo cha kudidimiza uchumi wetu kuanzia mtu mmoja mmoja hadi ngazi ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Ikionekana tatizo ni sisi tunaoongozwa basi hatutakuwa na budi ya kujirekebisha ili tuwaunge mkono na kuwaongezea muda wa uongozi ili wazidi kutuonesha njia za kufikia maendeleo ya mkoa wetu na iwapo itathibitika waziwazi kuwa viongozi tuliowakabidhi dhamana zetu wao ndio wamekuwa mzigo kwetu basi hatutakuwa na budi kuwaweka kando katika muhula ujao.
Hata hivyo napenda kuwahasa vijana wenzangu sambamba na akina mama wa mkoa wa Kagera,kanda yetu ndio chachu ya kuleta maendeleo ya mkoa wetu,tusipende kukimbilia mikoani pasipokuwa na sababu za msingi maana fursa tunazozitafuta nje ya mkoa wetu ni zilezile zinazopatikana ndani ya Kagera hivyo tusidanganyike na kuanza kukimbilia mikoa jirani na kuacha rasilimali zetu zibakie tu pasipokuwepo na watu wa kuziendeleza.
Hebu tuamue na turudi nyumbani tukaujenge mkoa wetu na kwa kufanya hivyo tutaweza kuinua sekta zote zilizowahi kuinua uchumi si tu mtu mmoja mmoja bali hata mkoa wetu na taifa kwa ujumla mfano wa sekta hizi ni pamoja na KILIMO, ELIMU, AFYA, UTALII, BIASHARA, VIWANDA, UVUVI, n.k.
Pia tusipende kutoa dhamana zetu za uongozi kwa watu kwa kuangalia elimu ya juu waliyonayo,fedha walizonazo,ukaribu na viongozi wa ngazi za juu kitaifa walionao,ubora wa familia/historia ya familia walikozaliwa,vitenge na khanga walizotupatia,sukari,unga,mchele,pombe na vijisenti walivyotuletea au chama wanakotokea bali tuwachague kwa kuangalia sifa na sera walizonazo kama zitaweza kumkomboa mwana Kagera au zinaendana na malengo yetu kielimu,kiafya,kilimo na kiuchumi kwa ujumla.Tukitoa dhamana yetu kwa watu wenye mlengo wa kushibisha matumbo yao kwa njia za dezo utakuwa umeuza mkoa wetu na hilo ndio litakuwa kaburi la mkoa Kagera.
Ukombozi wa Kagera katika sekta ya elimu wala hauhitaji kichochezi (catalyst) aina ya pombe kutoka kwa wagombea na matajiri waishio ndani na nje ya mkoa bali unahitaji walimu mahili na wenye ubora wa hali ya juu,madawati ya kutosha katika shule zetu,vitabu vya kutosha na vinavyokidhi mahitaji ya vijana wetu,mahabara zilizosheheni vifaa vya kutosha,mabweni ya watoto wetu wa jinsi zote na lishe bora.
Ukombozi wa Kagera katika sekta ya uchumi hauhitaji kupewa zawadi ya pombe,khanga,sukari,unga wala vijisenti bali unahitaji kutoa elimu na mbinu za uzalishaji mfano badala ya kutununulia pombe na wagombea au matajiri,watufundishwe namna ya kutengeneza na kusindika pombe yetu katika mikoa yote na hata ikiwezekana tusindike pombe katika soko la Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya;badala ya kupewa unga, watufundishwe namna nzuri ya uzalishaji wa mahindi na tupewe mashine kupitia vikundi vyetu (SACOS) ili tusage mahindi yetu wenyewe na tupate unga wa kutosha kwa matumizi ya nyumbani na biashara; badala ya kupewa vijisenti tufundishwe namna ya kukuza mitaji yetu kupitia SACOS na kuweka akiba katika mabenki yetu, n.k.

Ninayo mengi ya kuongelea,sema tu muda umekuwa mfinyo mno ila panapo majaliwa tutakutana tena mwaka ujao wa 2014. Hata hivyo napenda kuwahasa wana wa Kagera waiishiyo ndani ya mkoa,nje ya mkoa hata nje ya nchi kuwa yatupasa kuunganisha juhudi zetu kurudisha taswira ya mkoa wetu,taswira iliyokwishapotea katika uso wa Tanzania (Tanganyika enzi hizo) na dunia kwa ujumla katika sekta ya elimu,afya,siasa,uchumi,n.k. Kagera tuliyonayo sasa siyo Kagera tuliyotunukiwa na Mwenyezi Mungu wala tuliyoirithi kutoka kwa mababu zetu.HIVYO TUNALO JUKUMU LA KUREJESHA KAGERA: ILIYOSHEHENI MAZIWA NA HASALI;YENYE UPENDO,UMOJA NA MSHIKAMANO; YENYE KAHAWA BORA; MATOKE na siyo ndizi mshale;ILIYOSHHENI “ORUBISI KURUGA OMULAMBA OGWOTULIKWETA OMUNENE AND NOT OMWANJULANE”;YENYE WATU WENYE HEKIMA,BUSARA,ADABU NA IMANI ILIYOTUKUKA.
Huu ni mtazamo wangu na ukiona unakugusa then LIKE IT/SHARE WITH YOUR FRIEND .Nawatakia sikukuu njema za NOEL (2013) NA MWAKA MPYA (2014).
Nawapenda wote wana Kagera.Mungu Ibariki KAGERA. Mungu Ibariki Tanzania
Asanteni kwa kuusoma waraka huu.
 
Wenu DENICE RWECHUNGURA ISHENGOMA
(0682 - 704214)
VIA BUKOBAWADAU BLOG
Next Post Previous Post
Bukobawadau