Bukobawadau

MAMA ANNA TIBAIJUKA ATAKA SOKO LA NDIZI MULEBA

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amewataka madiwani wa Halmashari ya Muleba, mkoani Kagera, kujenga soko la ndizi la kisasa kwa ajili ya mahitaji ya wananchi na kupanua ajira kwa jamii.
Tibaijuka alitoa kauli hiyo juzi mjini Muleba, katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Profesa Tibaijuka, ambaye pia ni mbunge wa Muleba Kusini (CCM), madiwani wa wilaya hiyo wanatakiwa kuweka mikakati ya ujenzi wa soko hilo, kwa kuzingatia zao hilo ni muhimu kwa wananchi wa Muleba na mkoa kwa ujumla.
“Naamini sisi madiwani wa Muleba tukijenga soko la ndizi itasaidia kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi wetu. Maana itawarahisishia wananchi kupata mahitaji eneo sahihi,” alisema.
Aidha, waziri  aliwataka madiwani kusimamia ardhi ya wananchi kwa umakini, na kuongeza kuwa diwani yeyote  haruhusiwi kugawa ardhi bali anatakiwa kusimamia kwa uangalifu rasilimali hiyo.
Diwani wa Kamachumu, Dunstan Mutagywa (CCM) aliunga mkono wazo la waziri huyo na kusema soko la ndizi linatakiwa kujengwa kwenye eneo ambalo wananchi watapata wateja.
Alisema endapo watajenga soko hilo sehemu nzuri ambayo wananchi atafanya biashara, itasaidia katika upatikanaji wa huduma hiyo muhimu karibu na jamii yenyewe.
Next Post Previous Post
Bukobawadau