WASALITI DAWA YAO NI KUTENGWA
Na Prudence Karugendo
MSOMAJI mmoja wa gazeti hili ambaye hakutaka jina lake lijulikane, kanitumia ujumbe mfupi wa maandishi akinitaka nikishauri Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili kiwasamehe wale makada watatu waliovuliwa nyadhifa katika chama hicho.
Nilivyomuelewa mtu huyo, kama hakutumwa ayaseme hayo, basi atakuwa anaongelea kitu ambacho hakielewi akiwa anasukumwa na mapenzi (ushabiki) binafsi yaliyozingirwa na upofu. Yaani mtu kupenda kitu bila kuwa na uwezo wa kujieleza kwa nini anakipenda.
Kwa ufupi nilimweleza mtu huyo kwamba binafsi nakubaliana kabisa na uamuzi uliochukuliwa na Kamati Kuu ya Chadema wa kuwavua nyadhifa makada hao. Tena mimi naenda mbali zaidi na kutaka watu hao watengwe kabisa kwenye chama, kwa maana ya kuvuliwa uanachama.
Mtu huyo anayeitaka Chadema iwe na huruma bila kuelewa kwamba huruma nyingine inaweza kuwa kama ya mshumaa, kuwaangazia wengine huku wenyewe ukiteketea, nimemweleza kitu kimoja cha msingi, kwamba Chadema kikiwa chama kinachoundwa na wanadamu, kamwe hakiwezi kuwa na huruma kuliko Mwenyezi Mungu.
Sote wanaomwamini na kumcha Mungu, tunaelewa kwamba baada ya uumbaji wa Mungu walitokea baadhi ya viumbe wake wakamuasi na kumsaliti wakijiona wako sawa na yeye. Mwenyezi Mungu akawalaani na kuwatupa jahanamu. Ndio mashetani.
Je, kama Mwenyezi Mungu hakuwasamehe viumbe wake waliomsaliti, wakati ni yeye aliyewaumba, uko wapi uwezekano wa binadamu kumsamehe binadamu mwenzake aliyemsaliti wakati hakumuumba? Tena wakati msaliti akitegemea msamaha huo ili umwezeshe kukamilisha usaliti wake? Ina maana binadamu anaweza kuwa na huruma kuliko Mwenyezi Mungu? Kwa wanaomwamini Mungu wanapaswa waelewe kuwa msaliti anatakiwa atengwe kimwili na kiroho kama alivyofanywa shetani.
Tunatakiwa kuelewa na kuzingatia kwamba chama cha siasa ni mjumuiko wa watu waliokubaliana kuwa na malengo ya pamoja. Asiyekubaliana na malengo hayo yuko huru kujiondoa kwenye chama husika. Naamini kabisa kwamba hiyo ndiyo demokrasia kwa maana halisi. Mmoja kuwavuruga walio wengi hiyo haijawahi kuwa demokrasia. Ni vurugu tu za kishetani.
Mtu anayeng’ang’ania kwenye chama huku akitenda mambo yaliyo kinyume na malengo ya chama, na kibaya zaidi akionekana kutumiwa na wahasimu wa chama kukidhoofisha chama anachoking’ang’ania, huyo hawezi kuitaja demokrasia hata kidogo, moja kwa moja huyo ni msaliti sawa na alivyo shetani kwa Mwenyezi Mungu. Kumsamehe mtu wa aina hiyo ni sawa na kujichimbia kaburi.
Kwa watu wenye akili timamu, ni bora kutokuwa na chama, yaani chama kisiwepo kabisa, kuliko kuwa na chama kinachoendeshwa kwa nguvu za wahasimu! Chama hicho kitampinga nani na kitafanikiwaje wakati ambaye kingempinga ndiye anayekipangia kifanye nini!
Nitatoa mfano; sote tilishuhudia jinsi makada wa Chadema waliovuliwa nyadhifa kwenye chama hicho walivyopangiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari, mkutano ulionekana wazi bila kificho chochote kuwa uliandaliwa na wahasimu wa Chadema. Na kwa jinsi nilivyoona, mwanzoni nilidhani makada hao wa Chadema wangetangaza kujiunga rasmi na chama ambacho makada wake walionekana wakihangaika kuuratibu mkutano huo. Lakini kinyume chake wavuliwa nyadhifa hao wakatamka kwamba hawana mpango wowote wa kujiondoa Chadema!
Pengine yaliyolengwa katika usaliti hayajatimia! Mfano, majeshi ya Tanzania yalitumia kila mbinu kubaki nchini Uganda wakati wa Vita ya Kagera 1978 – 79, mpaka yalipohakikisha serikali ya Idd Amin imeondolewa madarakani, Amin kakimbia na majeshi yake yamepotea. Hilo ndilo lililokuwa lengo la Tanzania kuingia Uganda, bila hivyo inekuwa kazi bure.
Mbali na mkutano huo wa wavuliwa nyadhifa ndani ya Chadema na wanahabari, kote wanakokwenda watu hao kwa madai ya kuongea na Wanachadema, mipango yao yote ya kufanikisha maongezi hayo inafanywa na wahasimu wa Chadema! Kwa maana hiyo wabaya wa Chadema ndio wanaotaka waone demokrasia ikitendeka ndani ya chama hicho lakini si kwenye vyama vyao!
Tukumbuke kuwa kuvuliwa nyadhifa na hata uanachama sio jambo tunaloweza kusema kuwa limeanzia Chadema. Chama cha PAC cha Afrika Kusini kilitokana na ANC cha kulekule, baada ya baadhi ya makada ndani ya ANC kushindwa kuelewena na malengo ya chama hicho. Hilo halikuifanya ANC itetereke.
Hapa kwetu, Tanganyika wakati huo, baadhi ya makada wa TANU walivurugana na kushindwa kuelewana hivyo wengine wakaamua kuondoka na kuanzisha ANC. TANU haikutetereka.
Sasa ni kitu gani kinachowafanya watu hao waliovuliwa nyadhifa ndani ya Chadema kutokana na utovu wao wa nidhamu waonekane lulu kiasi kwamba baadhi ya watu wanaona wakiondoka chama kitatetereka?
Kwa upande wangu naona hata kama chama kitatetereka, kitu ambacho sikitegemei hata kidogo, bora na iwe hivyo, kuliko chama kuendelea kuwakumbatia watu ambao tayari wanaonekana wametumwa na wanafadhiriwa kukisambaratisha.
Tujiulize, kutetereka na kusambaratika kabisa kwa chama kipi kibaya zaidi? Tangu lini adui akakutengenezea mahali pema pa kukaa vizuri na kuendelea kumsakama?
Niliwahi kuona mtu ambaye alitokea kuwa maarufu na kujitengenezea ufuasi mkubwa wa wananchi, wengi wao wakiwa wameuchoka mfumo wa uendeshaji wa nchi uliokuwepo. Baadaye mtu huyo akadai kuuasi mfumo alioutumikia tangu utoto wake na kukivamia chama cha upinzani.
Wananchi wakamfuata kwa wingi wakiwa wamejawa na matumaini kwamba mtu huyo angewaonyesha njia ya kwenda Ikulu ili wao wamwezeshe aingie na kuufuta mfumo uliokuwepo wa utawala ambao ulishawachosha. Lakini mtu huyo badala ya kuyafanya waliyoyategemea akawavuruga akili wananchi na kuwapoteza “maboya” mpaka wakaisahau Ikulu!
Hilo ni fundisho ambalo wananchi hawatakiwi kulisahau. Wanapaswa wafumbue macho, waone na kutambua kuwa kinachopaswa kufuatwa ni mfumo na si mtu. Mtu anaweza akahongwa na wanaopinga juhudi za wananchi na hivyo yeye akaishia kuwapotosha tu wananchi, kitu ambacho hakiwezekani kwa mfumo.
Yupo msomaji mwingine wa gazeti hili aliyejitambulisha kwa jina la James Kiemi wa Isamilo Mwanza, yeye anasema kwamba Dk. Kitila Mkumbo, mmoja wa makada wa Chadema waliovuliwa nyadhifa, anaonekana kuendeleza siasa za kuwataka watu washabikie mtu badala ya kuupenda mfumo.
Kiemi anasema kwamba Mkumbo, katika moja ya makala zake, kamtaja Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kama mmoja wa watu waliopitia katika misukosuko ya kidemokrasia mpaka akaupata urais.
Msomaji huyo anauliza ni Zuma yupi anayeongelewa na mkumbo? Anasema kama ni Zuma huyu anayezomewa na wananchi kila anakopita nchini mwake basi Mkumbo ajielewe kuwa ana matatizo. Akauliza kwamba Mkumbo hakuona jinsi Zuma alivyozomewa hata kwenye mazishi ya Mandela?
Kiemi anasema kwamba Mkumbo, kama msomi wa kiwango cha shahada ya uzamivu, alipaswa kuelewa kuwa wananchi wa Afrika Kusini tayari wameishagundua kosa lao walilolifanya la kumshabikia mtu badala ya kuufuata mfumo, na kwamba sasa wanajuta. Kwahiyo eti kwa hapa Mkumbo asingemtumia Zuma kama mfano sahihi.
Msomaji huyo anaendelea kuhoji kwamba iwapo Dk. Mkumbo anajitambulisha kama mtetezi wa kweli wa demokrasia, je, kufanya vikao vya siri ndani ya chama cha upinzani kwa lengo la kuupindua uongozi wa upinzani kwa manufaa ya chama tawala ndiyo demokrasia?
Bila kusita wala kufanya unafiki wa aina yoyote, kwangu mimi msaliti ni sawa na muovu mwingine yeyote. Sina namna yoyote ninayoweza kukaa na kupatana na msaliti. Hiyo ni kwa sababu siwezi nikawa na uhakika msaliti atashindwaje kunisaliti mimi kama ameishawasaliti waliomtoa kusikojulikana na kumfanya ajulikane. Sitegemei kama msaliti anao uwezo wa kusema kwamba kwa kiwango hiki cha usaliti hapa panatosha.
Msaliti, kama alivyo shetani, sitarajii awe na rafiki. Atakuwa nao marafiki wa mashaka ila wakati wa matamanio ukifika ni lazima atawasaliti ili kukithi matamanio yao yake. Msaliti dawa yake ni kutengwa.
0784 989 512