Bukobawadau

CAG KUANIKA UFISADI BUKOBA

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amesema wiki ijayo atakwenda mkoani Kagera kuweka wazi yaliyobainika katika ripoti ya ukaguzi wa tuhuma za ufisadi zinazoikabili Halmashauri ya Bukoba.
Akizungumza na Tanzania Daima ofisini kwake jana, Utouh alisema ukaguzi huo umekamilika na wanakwenda Bukoba kuweka wazi kile waliochokibaini.
Alisema kwa utaratibu wa ukaguzi, lazima kifanyike kikao cha awali kabla na baada ya ukaguzi ili kuweka hadharani walichokibaini.
“Kabla ya kukabidhi ripoti hii ni lazima kwanza twende Bukoba kufanya kikao ili kuwaeleza tulichokibaini katika ripoti hiyo, na baada ya kumaliza kikao hicho ndiyo utaratibu wa kukabidhi utafuata.
“Hiyo inafanyika kwa utaratibu na sheria za ukaguzi zinavyohitaji,” alisema.
Katika uchunguzi huo timu ya wakaguzi ilifanya kazi kwa kuegemea hadidu 14 za rejea huku wakijikita kwenye maeneo husika kwa mwaka wa fedha 2010/11 hadi 2012/13.
Kwa mujibu wa Utouh, hadidu hizo ni kuchunguza usahihi wa utaratibu uliotumika kumpata mwekezaji wa kituo cha kuoshea magari, Kampuni ya ACE Chemicals Ltd.
Kuchunguza uhalali wa nyaraka na kiasi kilichowekezwa cha sh milioni 297 kwenye mradi huo, kuchunguza tatizo na sababu za viwanja 800 kutogawiwa kwa wananchi waliochangia gharama za upimaji, mradi wa upimaji wa viwanja 5,000, mradi wa ujenzi wa soko na mradi wa kujenga kitega uchumi.
Aliongeza kuwa nyingine ni mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi, ujenzi wa chuo cha ualimu, kituo cha maarifa na ujenzi wa bwawa kwa ajili ya utalii.
Yalikuwepo pia masuala mengine ya matumizi ya fedha yanayoashiria ubadhirifu na wizi au ufujaji wa mali za halmashauri na kutoa ushauri kwa serikali kuhusu namna bora ya kuimarisha usimamizi wa mapato katika halmashauri hiyo.
Ukaguzi huo pia umegusa mradi wa maji wa Benki ya Dunia kwa ajili ya Kata ya Nyanga, kiwanja cha Shule ya Msingi Kiteyagwa, barabara ya kupitia Kagondo Kaifu hadi Kagondo Karagulu, ujenzi wa Soko Kuu la Manispaa ya Bukoba na Ilani ya Uchaguzi.
Ofisi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ilimuomba CAG kufanya uchunguzi wa halmashauri hiyo ili kumaliza mgogoro uliodumu miaka miwili hatua iliyosababisha wananchi wa halmashauri hiyo kushindwa kupata maendeleo.
Timu ya wakaguzi ilianza kazi Septemba 30, mwaka jana.
VIA; TANZANIA DAIMA
Next Post Previous Post
Bukobawadau