HOTUBA YA MKUU WA MKOA MHESHIMIWA KANALI (MSTAAFU) FABIAN I. MASSAWE AKIFUNGUA KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI MKOA (RCC) TAREHE 16 JANUARI, 2014
“Kagera Amani na Maendeleo,
Amani na Maendeleo Kagera”
Kwanza
kabisa nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na asili
ya mema yote kwa kutulinda mwaka 2013 na kutuwezesha kuingia mwaka mpya wa 2014
tukiwa wazima. Sambamba na hilo
namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuhudhuria kikao cha leo ili tuweze
kujadili mambo kadhaa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa mkoa wetu. Aidha, nachukua fursa hii kuwakaribisha
kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kinachofanyika leo hii.
Ndugu Wajumbe,
kikao cha leo ni cha kwanza katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, cha muhimu sana
na cha kihistoria katika mkoa wetu.
Aidha, katika kikao hiki pamoja na agenda zingine tutapokea na kujadili
taarifa utekelezaji wa mfumo mpya wa ufuatiliaji na usimamizi miradi ya
maendeleo wenye kuleta Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN), taarifa ya
Programu ya usambazaji umeme vijijini na hali ya umeme mkoani Kagera, taarifa
ya hali ya ukuaji wa uchumi katika Kanda ya Ziwa Viktoria, taarifa kuhusu
mchango wa taasisi za kifedha katika maendeleo na ustawi wa mkoa na Mapendekezo
ya kuongeza vijiji na Vitongoji kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa
mwaka 2014. Aidha, tutapokea taarifa ya
utekelezaji wa Bajeti ya Matumizi ya Kawaida na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka
wa fedha tunaoendelea nao wa 2012/2013, 2013/2014 (Julai hadi Septemba) na
Mapendekezo ya bajeti na mpango wa fedha kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Wajumbe
Ndugu Wajumbe,
tofauti na ilivyozoeleka huko nyuma mwaka huu Serikali imeamua kubadilisha
mzunguko wa kuandaa, kujadili, kupitisha na kutekeleza Bajeti ya Serikali. Jambo hili linatugusa moja kwa moja na hivi
leo kikao chetu kitapokea, kujadili na kupitisha Bajeti na Mpango wa Maendeleo
wa Mkoa wetu wa mwaka wa fedha 2014/2015.
Aidha, nichukue nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wetu, kuitetea
kwa nguvu zenu zote Bajeti ya Mkoa wetu katika Bunge la Bajeti linalotarajia
kuanza mapema mwezi Aprili, 2014.
MFUUMO MPYA WA UFUATILIAJI
NA USIMAMIZI WA MIRADI – MATOKEO MAKUBWA SASA
Ndugu Wajumbe,
Mfumo wa tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) ni mfumo mpya wa
ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo ambao umeanzishwa na serikali ili
iweze kuleta matokeo ya haraka ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wetu.
Ndugu Wajumbe,
napenda kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu mfumo huu wa Matokeo Makubwa Sasa
kutokana na mkanganyiko wa kiuelewa juu ya dhana na malengo yake kwani baadhi
ya watu wanautafsiri kuwa ni mpango huku wengine wakiutafsiri kuwa ni programu.
Napenda ieleweke wazi kuwa serikali inao mpango wa miaka mitano mmoja wa
2011/2012 hadi 2015/2016. Hivyo, katika kuhakikisha kwamba malengo ya mpango
huu yanafikiwa kwa wakati seriakali imeanzisha mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa.
Ndugu Wajumbe, kwa
kuanzia serikali inatekeleza mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa katika sekta za
Kiwizara sita (6) ambazo ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara
ya Kilimo Chakula na Ushirika, Wizara ya Maji, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya
Nishati na Wizara ya Fedha. Katika Wizara ya Elimu na Mafunzo serikali imelenga
kuongeza ubora wa elimu kwa kushughulikia changamoto zinazohusiana na masuala
yanayohusu walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, usimamizi wa mfumo wa
elimu, tathmini ya ubora wa elimu na masuala mtambuka.
Aidha,
kwenye Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika katika mkoa wa Kagera unalenga
kuendeleza kilimo cha kibiashara kwa zao la miwa katika shamba la Kitengule
lenye ukubwa wa hekta 16,500 liliko wilaya ya Karagwe. Katika mfumo wa Matokeo
Makubwa Sasa mkoa wetu unalenga kuongeza wa uzalishaji wa sukari tani 50,564
kwa kipindi cha 2013/2014 – 2015/2016 kwa kushirikisha Kiwanda cha Sukari cha
Kagera.
Ndugu
Wajumbe, chini ya mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa serikali imelenga kuongeza
upatikanaji wa maji kwa wananchi wetu. Kama inavyofahamika ni kwamba hali ya
sasa ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo ya vijiji ni asilimia 55.3,
upatikanaji wa maji katika Manispaa ni asilimia 79 na kwenye makao makuu ya
wilaya upatikanaji wa maji ni asilimia 69. Napenda kutoa wito kwa viongozi na
watendaji mbalimbali wa wilaya kusimamia kikamilifu miradi ya maji inayoendelea
kujengwa ili ikamilike na kutoa huduma kwa wananchi wetu. Vivyo, hivyo
usimamizi ufanyike katika sekta za uchukuzi, nishati na Wizara ya Fedha ili
halmashauri ziweze kuongeza mapato yake ya ndani.
USAFI WA MAZINGIRA
Ndugu Wajumbe,
kutokana na ufanisi katika kuyatunza mazingira yetu na kuyaweka katika hali ya
usafi, naendelea kuwapongeza viongozi na wananchi wote tunaoshikamana pamoja
katika kuuweka Mkoa wetu katika hali ya usafi.
Nichukue nafasi hii pia kuwapongeza viongozi na Watendaji wa Manispaa ya
Bukoba kwa kutunza mji wetu na kuufanya kuwa mshindi wa tatu (3) katika usafi
wa miji ya Manispaa Kitaifa, hii pia ni fahari kwetu wana Kagera. Aidha, niendelee kusisitiza kwa viongozi na
Watendaji wa Halmashauri zetu zote kupanda miti kwa wingi ili kukamilisha lengo
la Mkoa wetu la kupanda miti 13,479,000 kwa mwaka 2013/2014 idadi ambayo ni
ndogo kama tutaamua kwa dhati kufanya kazi hiyo muhimu. Ni matarajio yangu kuwa mnafahamu wazi suala
la usafi wa mazingira kuwa ni pamoja na kuhakikisha takataka zinakusanywa na
kuwekwa mahali panapostahili ili zichomwe au zifukiwe, utunzaji wa vyanzo vya
maji, kuhakikisha kila kaya ina choo na siyo bora choo bali choo bora na
kuyaweka majengo yetu katika hali ya kupendeza kwa kuyapaka rangi. Ni imani yangu kuwa maelekezo haya yatatiliwa
mkazo na miti itaendelea kupandwa kando kando ya barabara zote za Mkoa huu wa
Kagera. Haya ni maagizo ya Mheshimiwa
Makamu wa Rais ambayo hatuwezi kuyakiuka.
Mvua zinazoendelea kunyesha zitumike vizuri ili kuhakikisha malengo ya
upandaji miti yanafikiwa.
HALI YA CHAKULA MKOANI
KAGERA
Ndugu wajumbe,
Mkoa wetu kwa mwaka wa 2013/2014 ulilenga kulima hekta 721,597 za mazao
mbalimbali ya chakula zilizotarajia kuzalisha jumla ya tani 3,199,334 zikiwa
nafaka tani 337,562; kunde tani 148,799; ndizi tani 1,506,020 na mazao ya mizizi
tani 1,231,611. Wakati huo huo eneo
lililolengwa kulimwa mazao ya biashara ni hekta 74,120 kwa lengo la kuvuna
jumla ya tani 68,450 zikiwa kahawa za maganda tani 58,030; majani mabichi ya
chai tani 7,845; pamba mbegu tani 1,575 na tumbaku tani 1,000. Pamoja na kwamba mwaka huu mtawanyiko wa mvua
kwa kipindi cha mvua za vuli haukuwa mzuri sana kwa maeneo kadhaa hata hivyo
hali halisi kwa mavuno mashambani inaridhisha na tathmini inaonesha kuwa mkoa
mzima hadi hivi sasa tuna ziada ya chakula.
Kwa pamoja tuzidi kujishughulisha katika kilimo cha kisasa na chenye
tija kwa kufuata kanuni za kilimo.
Aidha, hali ya chakula kwa mkoa ni nzuri, hata hivyo nichukue nafasi hii
kuwataka wajumbe waalikwa na wadau wengine kwenye mkoa wetu kuendelea
kuhamasisha wananchi ili wazitumie mvua hizi za masika kwa kulima mazao yetu ya
kawaida bila kuacha yale yanayokomaa kwa muda mfupi ili kuepuka kupatwa na njaa
na ituwezeshe kuzalisha chakula cha ziada na tusaidie maeneo ambayo yatakuwa na
upungufu wa chakula. Sehemu mbalimbali za nchi kuna taarifa za njaa. Kwa bahati nzuri mkoa wetu hauko katika
orodha ya mikoa ambayo iko katika hali hatarishi ya njaa.
Ndugu wajumbe,
pamoja na mkoa kutokuwa na tatizo la upungufu wa chakula bado inatakiwa
tuongeze mbinu za uzalishaji ili tupate ziada itakayowezesha wakulima kuuza
mazao na kujipatia kipato zaidi. Hivyo
matumizi ya pembejeo za kilimo na hasa mbolea na mbegu bora ni muhimu kwa watu
wetu. Matumizi ya zana za kilimo
yatumike mfano matrekta n.k. tuachane na jembe la mkono. Aidha, kwa mwaka 2012/2013 wakulima 25,000
walinufaika na mbolea za ruzuku katika Wilaya za Biharamulo, Missenyi, Karagwe
na Ngara. Idadi hii imepungua
ikilinganishwa na wakulima 53,192 kwa mwaka 2011/2012. Hii ni kwa sababu Wilaya ya Chato iliyokuwa
kwenye mpango huo imehamishiwa Mkoa wa Geita na wakulima kadhaa wamemaliza
miaka ya mkataba wao wa miaka mitatu (3) ya kupata mbolea za ruzuku.
Ndugu Wajumbe,
imani yangu ni kwamba kwenye mkoa wetu pia tuna mifugo inayoweza kutupatia samadi
ya kutosha kama wananchi wetu wataelimishwa, kutahamasishwa na
kushirikishwa. Ninasisitiza jamii zetu
zihamasishwe kutumia samadi itokanayo na mifugo yetu, pasipo kusubiri mbolea za
ruzuku tu ili zijiongezee uzalishaji.
HALI YA ELIMU
Ndugu wajumbe,
kwa mwaka 2013 Mkoa wa Kagera ulisajili wanafunzi 43,154 kufanya mtihani darasa
la saba. (Wav.20,257 na Was. 22,897) hawa ni 75% ya watoto 57,779 (Wav. 28,405
na Was. 29,374) walioandikishwa darasa la kwanza 2007, asilimia 25 kutomaliza
elimu ya msingi si swala la kujivunia bali tunatakiwa tulilaani kwa pamoja na tupambane
na sababu zote zinazofanya watoto wetu kutomaliza darasa la saba ambazo ni
pamoja na utoro 418, mimba 16, vifo 13 n.k.
Kati
ya wanafunzi waliosajiliwa kufanya mitihani ya darasa la saba, waliofaulu ni 24,546
(Wav. 11,919 na Was. 12,627) sawa na 58.1% ya wote waliofanya mitihani. Katika mwaka huu wanafunzi wote waliofaulu
mitihani ya darasa la saba wamepata nafasi za kujiunga na masomo ya kidato cha
kwanza. Kipekee ninachukua nafasi hii kuipongeza Halmashauri ya Wilaya
Biharamulo kwa kuwa ya kwanza kimkoa ikiwa imefaulisha kwa asilimia 85.59 na
Manispaa ya Bukoba asilimia 80.74 ambazo zimechangia mkoa wetu kuwa nafasi ya 7
Kitaifa. Vile vile nichukuwe nafasi hii kuziagiza Halmashauri za wilaya za
Karagwe/Kyerwa (50.99%), Muleba (52.87%), Bukoba (53.41%) na Missenyi (58.59%)
kuongeza bidii zaidi ili mwaka unaofuta ziweze kufaulisha kwa kiwango cha juu. Aidha,
nichukuwe fursa hii kuwapongeza ninyi viongozi na watendaji mbalimbali kwa
kusimamia kikamilifu ujenzi wa miundombinu ya madarasa inayotosheleza mahitaji.
Kipekee niwashukuru wananchi wote wa mkoa wa Kagera kwa kutoa michango yao ya
nguvu na fedha ambayo imechangia kukamilika kwa miradi mbalimbali ya maendeleo
hususan vyumba vya madarasa. Aidha, napenda kuwaagiza viongozi na watendaji
wote wa serikali kuhakikisha mnasimamia na kushauri juu ya ukamilishaji wa
ujenzi wa miundombinu ya maabara kwa kila shule ya sekondari ili kuongeza wigo
wa watoto watakaosoma masomo ya sayansi.
UTEKELEZAJI WA OPERESHENI
KIMBUNGA
Ndugu wajumbe,
Mkoa wetu ni miungoni mwa mikoa ya pembezoni ambako zoezi la kuwaondoa
wahamiaji haramu kutoka nchi za jirani linatekelezwa. Operesheni hii ilianza
kufanyika kuanzia mwezi Oktoba, 2013 kwa kushirikisha wilaya na idara za
serikali, hivi sasa operesheni inatekelezeka kwenye awamu ya nne ambapo katika
awamu hii wananchi wanatoa taarifa kuhusu hali ya uhamiaji.
Aidha,
napenda kuchukua fursa hii kuipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kuwaondoa
wahamiaji haramu katika ardhi ya mkoa Kagera ambao pamoja na athari zingine
walihatarisha usalama wa wananchi wetu, uharibifu wa mazingira na kupokonya
ardhi bila kufuata taratibu. Kipekee napongeza viongozi na wananchi kwa kutoa
ushirikiano wa dhati wakati wote wa zoezi hili. Napenda kuwaagiza viongozi na
watendaji wote wa wilaya kuendelea kushirikiana kwa kuwafichua wahamiaji na
kuwachukulia hatua pale wanapoingia, tusisubiri wajenge himaya katika maeneo
yetu. Aidha, tuendelee kutoa elimu kwa wananchi wetu ili wafahamu athari za
uhamiaji hivyo washiriki kikamilifu katika kutoa taarifa zinazohusu wahamiaji
haramu.
Ndugu wajumbe,
kama mnavyofahamu katika mwaka wa fedha wa 2013/14 mkoa wetu uliidhinishiwa kiasi cha fedha cha
shilingi 174,925,757,000 kwa ajili ya
matumizi ya kawaida ya mishahara na
matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo. Na hadi kufikia mwishoni mwa Oktoba, 2013
tulikwishapokea kutoka Hazina shilingi 49,924,168,457
sawa na asilimia 28.54. Katika kikao hiki tutapokea taarifa ya utekelezaji
ya matumizi ya fedha hizo.
Katika
utekelezaji wa bajeti ya 2013/2014 Mkoa ulijiwekea malengo ya kukusanya mapato
ya ndani kwa Halmashauri zetu ambayo ni shilingi 13,737,670,000/=. Hadi Desemba, 2013 Halmashauri zilikuwa zimekusanya
shilingi 4,541,794,736.5 sawa na asilimia 34.73,
kwa mchanganuo ufuatao:-
NA.
|
HALMASHAURI
|
MALENGO
KWA MWAKA
|
MAKUSANYO
HADI DESEMBA, 2013
|
ASILIMIA
|
1
|
Biharamulo
|
1,581,375,000
|
699,836,231.68
|
46.54
|
2
|
Bukoba
|
1,403,896,000
|
509,000,772.68
|
36.3
|
3
|
Manispaa
|
2,576,167,800
|
590,566,367.77
|
32.4
|
4
|
Karagwe
|
1,675,359,600
|
746,084,055.12
|
54
|
5
|
Kyerwa
|
1,798,538,040
|
550,219,015.00
|
31.18
|
6
|
Missenyi
|
1,090,000,000
|
365,093,020.60
|
34.12
|
7
|
Muleba
|
3,298,495,283
|
783,220,119.24
|
24.4
|
8
|
Ngara
|
1,577,130,001
|
297,775,154.41
|
18.9
|
|
JUMLA
|
13,737,670,000
|
4,541,794,736.5
|
34.73
|
Napenda
kupongeze uongozi wa Wilaya za Karagwe kwa kuvuka lengo la asilimia hamsini
(50%). Wilaya hii inaonesha kuwa inaweza
kufikia malengo waliyojiwekea, kwa Wilaya zilizobakia hali ya makusanyo sio ya
kuridhisha ni vema kikao hiki kikajiridhisha ni kwanini Halmashauri hizo
makusanyo ya ndani bado yako chini.
BAJETI NA MPANGO WA
MAENDELEO WA 2014/2015
Ndugu Wajumbe,
Kikao chetu hiki kitapata nafasi ya kujadili na kupitisha Bajeti na Mpango wa
maendeleo wa Mkoa kwa mwaka ujao wa fedha wa 2014/2015. Mkoa unakusudia kuomba
kuidhinishiwa kiasi cha shilingi 252,349,563,967 kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na miradi ya maendeleo kwa Halmashauri zetu na Sektretarieti ya Mkoa
kipindi cha mwaka wa fedha 2014/15.
Ni
matumaini yangu kwamba bajeti na mipango ya maendeleo kwa kila Halmashauri
imejadiliwa na kupitishwa na vikao husika katika ngazi ya Wilaya. Nachukua nafasi hii kuwataka wajumbe kupitia
kwa makini Bajeti ya matumizi ya kawaida na maendeleo ya mkoa kwa ajili ya ustawi
wa maisha ya wananchi wetu na maendeleo ya mkoa wetu.
Natumaini
kuwa Waheshimiwa Wabunge wetu wataendelea kutetea bajeti ya Mkoa wetu katika
Kamati za Bunge na kwenye kikao cha Bunge la Bajeti kilichopangwa kufanyika
mwezi Machi, 2014.
Ndugu wajumbe, na
waalikwa Mabibi na mabwana baada ya maelezo hayo natamka rasmi kwamba kikao
chetu kimefunguliwa na nawatakia majadiliano mema.
“KAGERA.....
AMANI NA MAENDELEO, AMANI NA MAENDELEO........KAGERA”