JK KUKATAA KUITUA MIZIGO ANAMKOMOA NANI?
Na Prudence Karugendo
BINADAMU tumeumbwa na hulka tofautitofauti, katika
hulka hizo kuna watu wameumbwa na hulka za unafiki na wengine si wanafiki.
Pamoja na
kwamba watu hatupaswi kujisifia lakini naamini kabisa kwamba mimi sikuumbwa na
unafiki, na ninauchukia sana
unafiki.
Hakuna kitu
kibaya na cha hatari duniani kama unafiki.
Nadhani ndiyo maana Wahaya wakabuni usemi kwamba ni heri ukawa na jirani
jambazi kuliko kuwa jirani na mnafiki. Wahaya wanaamini kwamba jambazi unaweza
ukamkabili kwa kujiimarishia ulinzi kitu ambacho hakiwezekani kwa mnafiki.
Mnafiki
ataingia mpaka chumbani kwako akijidai ni rafiki na mtu mwema kwako
anayekutakia mema kumbe mambo ni kinyume chake! Atachukua siri zako zote bila
wewe kushtuka aende kuzifanyia maovu
yenye mpango wa kukuangamiza! Mnafiki ni mtu mchafu sana .
Kwahiyo
kutokana na kuuchukia unafiki nakuwa muwazi kwamba naipenda sana nchi yangu, na hivyo kuuombea uongozi
wake uliopo Mungu aujaze hekima za kuiongoza vyema nchi yetu. Pia nampenda rais
wangu na kumtakia kila la kheri nikielewa kuwa kazi aliyo nayo ni mzigo mkubwa
unaohitaji msaada wa kila mwananchi ili aweze kuubeba salama bila kuchoka
katika kipindi chote anachokuwa madarakani kwa mujibu wa kanuni za nchi yetu.
Lakini pamoja
na kumtakia mema rais wangu, hasa katika kumpunguzia uzito wa mzigo alioubeba,
inaonekana kuna watu walio karibu zaidi na yeye wanaomweleza kwamba kwa nyenzo
alizopewa hapaswi kuujali uzito wa aina yoyote katika mzigo ulio kichwani
kwake!
Watu hao ni
wanafiki wanaojifanya kumpenda sana ,
lakini kiukweli ni kwamba hawamtakii mema yeye binafsi, nchi yake pamoja na
watu anaowaongoza. Wao wanaangalia tu nafsi zao zimekaa katika nafasi gani, na
zitaendelea kukaaje ndani ya mzigo ulio kichwani kwa rais. Hawaujali uzito wake
hata kidogo, ila nafasi zao tu basi.
Kama nilivyosema, kutokana na kuipenda nchi yangu nampenda vilevile rais wangu bila unafiki wowote.
Akishakuwa rais siangalii katoka chama gani cha siasa, isipokuwa kumtakia kila
la kheri ili aweze kuwa na hekima za kuongoza vizuri kwa mustakabali mwema wa
nchi yetu.
Kwa sasa
tunaye kiongozi wetu mkuu ambaye ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete, aliyetokana na
Chama Cha Mapinduzi, chama tawala. Kwa vile chama hicho ndicho kinachotawala
tulitegemea kwamba kingempa rais msaada wa kila aina kusudi kada wake huyo
kileyemuamini na kumnadi kwa wananchi ili akabidhiwe mzigo wa kuiongoza nchi
asiweze kuuona uzito katika mzigo huo.
Lakini
badala yake, rais aliye pia mwenyekiti wa chama hicho, wakati fulani akatoa
kauli iliyoonekana kukisuta chama chake. Akasema chama kinapaswa kujivua gamba!
Sidhani kama angeona kwamba chama chake kina msaada kwake akatamani kijivue
gamba. Bilashaka kauli hiyo ilitokana na kuuona uzito wa mzigo alioubeba
unazidi kumkandamiza yeye peke yake pasipo kuuona msaada wa chama chake.
Hatahivyo
gamba aliloliona mwenyekiti lilishindikana kuvuliwa huku baadhi ya makada
wakibeza kwa jeuri kwamba gamba limekwamia kiunoni na wenye uwezo wa kulitoa ni
lazima watafute mashoka!
Lakini
pamoja na hiyo yalifanyika mabadiliko katika chama hicho yaliyomleta mtendaji
mkuu mpya, Katibu Mkuu, Abdulrhaman
Kinana, huku katibu mwenezi akibaki ni yuleyule Nape Nnauye.
Kusema
ukweli mimi ni mmoja wa wasiokubaliana na sera za chama tawala, hasa baada ya
chama hicho kukiuka misingi yake kwa kiasi kikubwa. Lakini pamoja na hilo nimewakubali kabisa
watu wawili katika chama hicho tawala kwamba ni majembe ya uhakika. Hao ni
wanasiasa kwa maana halisi. Watu hao ni Katibu Mkuu, Abdulrhaman Kinana na
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Kilichonifanya
niwakubali watu hao wawili ndani ya CCM ni hatua yao waliyoichukua ya kujitenga na wanafiki.
Wameamua kufanya kazi yao
kwa maana halisi ya chama tawala wakiwa wamelenga kumpunguzia rais uzito katika
mzigo alioubeba.
Ni kwamba viongozi
hao wa juu wa chama tawala wamezifanyia tathmini kero zote za wananchi na
kugundua matatizo yalikolalia. Wakaona ndani ya kinachoitwa usaidizi wa rais
ndimo kuna uzito zaidi. Hivyo wakaamua kutaja hadharani kuwa fulani na fulani
ndio wanaosababisha kero hizo na kumzidishia rais uzito kwenye mzigo alioubeba.
Na kwa vile mzigo huo ni wa rais na chama tawala, viongozi hao wa chama
wakapendekeza kwa rais kuwa mizigo isiyo na chochote ndani yake ni bora ibwagwe
chini.
Ni wazi
kwamba kama rais angesikiliza ushauri huo na
kuamua kuibwaga chini mizigo inayoleta usumbufu mambo mawili yangetokea kwa
wakati mmoja. Moja ni kwamba chama tawala kingepata umaarufu na ushawishi
zaidi, na pili yeye rais angeiona kazi hiyo nzito, uongozi wa nchi, kuwa ni
nyepesi akiwa amejinufaisha na faida ya kuwa na chama tawala nyuma yake.
Lakini
bahati mbaya sivyo ilivyokuwa. Badala yake rais kaamua kuubwaga chini ushauri
wa chama chake na kubaki na mizigo yake kichwani! Hapo ndipo ninapojiuliza, kwa
kufanya hivyo rais kamkomoa nani? Kaukomoa upinzani, kakikomoa chama chake au
kajikomoa yeye mwenyewe?
Zipo tetesi
kuwa rais kaamua kubaki na mizigo yake kichwani ili isije ikaonekana kaitua
mizigo kwa kushurutishwa na walio chini yake kimaamuzi. Najiuliza tena, ni lipi
ni rahisi kwake, kuonekana ameibwaga chini mizigo isiyo na faida yoyote na
inayoleta kero kwake na kwa wananchi kwa kushurutishwa na walio chini yake
kimaamuzi au kuendelea kubaki nayo kichwani na kuonekana ameshurutishwa na
mizigo yenyewe kufanya hivyo?
Sababu
inaonekana walio kwenye mzigo wa rais wanapenda waendelee kula uhondo wakiwa
wamebakizwa kwenye mzigo unaomsumbua rais kwa uzito wake hata kama
kubaki uko hakuna faida yoyote kwa rais, aliyebeba mzigo, kwa wananchi wala kwa
nchi zaidi ya kumsababishia rais wetu uchovu usio na mpangilio!
Kama watu
hao, wanaoitwa mizigo, wangekuwa na
mapenzi ya dhati kwa rais wao wasingesubiri kupigiwa kelele, wangechukua uamuzi
kama aliochukua aliyekuwa waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki , wa
kujiondoa wenyewe kwenye furushi lililo kichwani mwa rais.
Lakini
kitendo cha watu hao, mizigo, kukaa kimya huku rais akipigiwa kelele za
kumnusuru na wanaomjali wakimuonea uchungu kwa mizigo aliyoibeba, sioni kama
kinaweza kuwafanya watu hao waonekane wana mapenzi na yeye hata kama yeye mwenyewe atakuwa anaichukulia hivyo.
Tatizo kubwa
ninaloliona katika jamii yetu ni mazoea. Tunafika mahali mazoea tunayachukulia
kama sheria pasipo kujali kama mazoea hayo
yanatuathiri au la! Hapo ndipo rais naye anapoiangalia jamii yake jinsi
ilivyozama kwenye mazoea ikamwia vigumu kuchukua maamuzi ambayo pengine anaona
yanaweza yakakinzana na mazoea ya jamii yake na hivyo yeye kuonekana ni wa
ajabu!
Sababu mpaka
sasa wapo watu wanaomsema Rais Kikwete kwa mshangao kwamba kwa kipindi cha chini
ya miaka 10 kawa na maziri wakuu wawili. Watu hao wanasemea mazoea waliyoyapata
kwa rais wa awamu ya tatu, Mkapa, aliyekaa na waziri mkuu mmoja tu, Sumaye, kwa
kipindi chake chote cha miaka kumi bila kueleza hilo lilikuwa na tija gani kwa nchi.
Wanaosema
hivyo hawataki kuangalia nyuma na kuona jinsi mambo yalivyokuwa hasa katika
awamu ya kwanza. Mwalimu Nyerere alifanya mabadiliko mara tano katika nafasi ya
waziri mkuu katika kipindi cha miaka 10 kati ya mwaka 1975 – 1985.
Alimbadilisha
Mzee Kawawa na kumuweka Marehemu Sokoine, baadaye akaja Mzee Msuya na baadaye
Sokoine tena, kisha Dk. Salimu.
Sasa
wanaomshangaa Kikwete kwa kufanya mabadiliko mara moja katika nafasi hiyo kwa
kipindi cha karibu miaka 10 wameyasahau hayo, hawayajui au wanashangaa kitu
gani?
Hapa inabidi
tuyaelewe mambo mawili, kwamba mazoea hudumaza na mabadiliko ni chachu ya
maendeleo. Kisichobadilika kawaida hudumaa.
Nimalizie
kwa kutoa mifano ya nchi mbili ambazo zinayapenda sana mabadiliko, na tuziangalie jinsi zilivyo kimaendeleo. Nchi
hizo ni India
na Japan.
India ni nchi isiyojali mtu kakaa kwa
kipindi gani madarakani ila kafanya nini akiwa pale. Iliwahi kuwa na waziri
mkuu aliyeitwa Gulzarilal, alikaa madarakani kwa siku 26 tu, Charon Singh kwa
siku 170, Chandra alikaa kwa siku 223, H. D. Deve Gowda alikaa kwa siku 324 na
I. K. Gigral alikaa madarakani kwa siku 332. Katika hao hakuna aliyefikisha
hata muda wa mwaka mmoja kwenye madaraka!
Japan nako
mambo yako vilevile. Sanjo Sanetomi alikaa madarakani kwa siku 60 tu,
Higashikuni Naruhiko alikaa kwa siku 53, Katsura Taro siku 61, Tsutomu Hata
siku 63. Ni mawaziri wakuu wengi katika nchi hiyo ambao hawakufikisha hata
mwaka madarakani.
Pamoja na
nchi hizo kuwa na mabadiliko ya mara kwa mara katika serikali zake ni kipi
tunachoweza kusema kuwa walau tunazikaribia kimaendeleo sisi tunaoyaogopa
mabailiko?
Mwisho
kabisa ni kwamba wanafiki ni watu wachafu sana .
Hawa waliwahi kumtembeza mfalme akiwa uchi wakidai amevaa nguo isiyoonekana,
kwamba wenye dhambi tu ndio waliomuona mfalme kuwa yuko uchi. Wanafiki hao
walifanya hivyo kutimiza matakwa ya mfalme, ambaye kwa ulevi wa madaraka
alitaka ashonewe nguo isiyoonekana!
Kinana na
Nape wamejitenga na wanafiki, wametamka wazi kuwa Rais Kikwete kabeba mizigo isiyo na maana, wakamshauri aibwage chini ili
mambo yamuendee salama. Inavyoonekana Kikwete kawapuuza, bilashaka baada ya
kuwasikiliza wanafiki.
Nafasi za
Kinana na Nape ni kubwa na nzito katika uendeshaji wa chama tawala, kupuuzwa
kwao ni kuzito vilevile, kunawafanya nao waonekane ni mizigo. Kwahiyo ili
wasionekane ni mizigo wangefanya kama alivyofanya Mzee Edwin Mtei, wakati wa
serikali ya awamu ya kwanza, pale
alipokwenda na mgeni toka Benki Kuu ya Dunia nyumbani kwa Mwalimu Nyerere,
Msasani, Nyerere akawaacha sebuleni na
kwenda zake nje kupunga upepo na kusoma kitabu.
Akufukuzaye
hakwambii toka. Alichokifanya Mzee Mtei ni kwenda ofisini kuandika barua ya
kujiuzulu. Kinana na Nape mnasubiri nini? Lindeni heshima yenu.
0784 989 512