WARIOBA:KATIBA YA TANGANYIKA INAWEZEKANA KWA MIEZI MITATU
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Katiba ya Tanganyika inaweza kuandikwa ndani ya miezi mitatu tu kwa kuwa maoni mengi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyozinduliwa Jumatatu, kwa kiwango kikubwa yametoka kwa wananchi wa upande huo wa Muungano.
Warioba alisema hayo jana wakati akizungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kwenye Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.
“Kutunga Katiba ya Tanganyika siyo kazi ngumu, ukisoma rasimu hii sura ya kwanza mpaka ya tano, sioni kama Katiba ya Tanganyika itakuwa tofauti na maoni yaliyomo katika sura hizo,” alisema na kuongeza:
“Misingi iliyopo katika utangulizi wa rasimu hii imetokana na maoni ya wananchi hao. Wakati wa kukusanya maoni, Zanzibar walijikita zaidi kwenye Muungano, maoni mengine kwa kiwango kikubwa yametoka kwa Watanzania Bara na katika kuandika Katiba ya Tanganyika sioni kama watabadilisha chochote kuhusu misingi hii ambayo ni; tunu za taifa, maadili, malengo na haki za binadamu.”
Alisema kuhusu kubadilishwa kwa mihimili ya Serikali na vyombo vingine vya kitaifa, kikubwa kinachoweza kuguswa ni muundo wa Bunge la Tanganyika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Baraza la Mawaziri.
“Kuhusu taratibu za kufanya kazi; iwe ni madaraka ya Rais, utaratibu wa kufanya kazi katika Bunge, Mahakama na Serikali sioni kama litakuja suala jipya kwa sababu mambo hayo yameshatolewa maoni. “Kilichobaki ni madaraka kwa umma tu, kwa maana ya Local Government (Serikali za Mitaa). Hata hili la madaraka kwa umma watakaolishughulikia watumie taarifa za wananchi waliotoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya. Wananchi walitoa maoni kuhusu jambo hili ambayo yapo wazi kabisa.”
Uchaguzi Mkuu 2015
Kuhusu uwezekano wa Katiba Mpya kutumika katika Uchaguzi Mkuu 2015, Jaji Warioba alisema Tume hiyo ilipewa muda mfupi wa kuandaa Rasimu ya Katiba kwa sababu ilielezwa kuwa uchaguzi wa mwaka 2015, utafanyika kwa kutumia Katiba Mpya.
“Katiba hii ilitakiwa iwe imekamilika Aprili mwaka huu, maana yake tungekuwa na mwaka mmoja na nusu wa kufanya mambo mengine ya kuwezesha itumike kwenye uchaguzi wa mwaka 2015,” alisema.
Alisema ndiyo maana katika rasimu hiyo, Tume imeweka masharti ya mpito ya miaka minne, kuanzia siku inapopatikana Katiba Mpya hadi Desemba 28, 2018.
Alisema ndiyo maana katika rasimu hiyo, Tume imeweka masharti ya mpito ya miaka minne, kuanzia siku inapopatikana Katiba Mpya hadi Desemba 28, 2018.
Alisema rasimu hiyo imefafanua Baraza la Mawaziri na Bunge vitakuwaje… “Sasa hivi tuna Serikali na Bunge. Katiba Mpya itapatikana mwaka huu, lakini Bunge letu litaendelea kuwapo kwa msingi wa Katiba ya sasa mpaka ufike wakati wa uchaguzi, hiyo inafanyika kwa ajili ya kulinda uongozi wa Bunge na Serikali.”
Alisema ili kuwepo na Uchaguzi Mkuu kwa Katiba Mpya ni lazima itungwe Katiba ya Tanganyika, kwamba wamependekeza miaka minne ya mpito ili kutoa nafasi ya kubadilishwa kwa mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuundwa upya Tume ya Uchaguzi itakayoendesha uchaguzi kwa msingi wa Katiba Mpya.
“Siyo lazima kila kitu kikamilike baada ya miaka minne, kuna mambo yanaweza kubadilishwa kwa miezi sita au mwaka mmoja. Kila tulipobadili Katiba tulifanya jambo hili.
“Mfano ni mwaka 1984 tulipofanya mabadiliko makubwa ya Katiba ambayo ilileta ukomo wa Rais, haki za binadamu, waziri mkuu na mambo mengine makubwa. Kipindi hicho ilitungwa sheria mpya ya uchaguzi ambayo inatumika hadi sasa.”
Gharama Serikali tatu
Kuhusu hoja kwamba muundo wa Serikali tatu ni gharama, Jaji Warioba alisema hautakuwa na gharama kubwa kama inavyotafsiriwa na watu wengi.
Alisema kwa kulitambua hilo, ndiyo maana Tume ilipunguza ukubwa wa Serikali, ikiwa ni pamoja na kupendekeza idadi ya wabunge 75 na mawaziri wasiozidi 15.
“Hata uwepo wa Serikali mbili bado hautaweza kupunguza gharama. Katika hili ni muhimu kukubaliana na mawazo ya wananchi juu ya muundo wa Serikali tatu ambazo zimepunguza gharama. Tumependekeza Serikali ya Muungano kuwa na chanzo chake cha mapato ambayo ni ushuru wa bidhaa, mapato yasiyo ya kodi, michango kutoka nchi wahisani, mikopo na mapato mengine.”
“Wapo watu wanataka kugawa mikoa, wapo wanaopendekeza Jiji la Mbeya ligawanywe, wapo wanaotaka Songea igawanywe, hizi zote ni gharama… Sasa iweje kugawa mikoa isiwe gharama, Serikali tatu iwe na gharama? Hata kijiji ninachotoka zamani kilikuwa kimoja, sasa vimegawanywa vipo vitatu!”Alisema Tanganyika ilipopata uhuru kulikuwa na majimbo manane tu, lakini sasa ipo mikoa 25 na wilaya, tarafa na vijiji zimegawanywa.
Alisema gharama za Serikali ya Muungano zitakuwa katika Wizara ya Ulinzi na Usalama pamoja na Mambo ya Nje, taasisi ambazo tayari zipo, “Inashangaza kuona watu wakisema kuwa Tume kupendekeza Serikali tatu ni kwenda kinyume na mawazo ya Mwalimu Julius Nyerere.”
Kumsaliti Nyerere
Alisema hata Mwalimu Nyerere hakuwa na mawazo mgando. Alikuwa anatambua mabadiliko na mara kadhaa alibadilika kulingana na mahitaji ya wananchi na wakati.Alitoa mfano akisema Mwalimu Nyerere alikuwa muumini wa mfumo wa chama kimoja, lakini mwaka 1992 baada ya Ripoti ya Jaji Francis Nyalali, alibadili mawazo na kuukubali mfumo huo licha ya asilimia 80 ya Watanzania kuupinga.
Alisema: “Maoni ya msingi yaliyomo katika rasimu hii yametokana na maoni ya wananchi, lakini vyombo vya habari vimejikita kuzungumzia mambo yanayohusu uongozi, hasa mambo ya kisiasa,” alisema Warioba huku akisisitiza kuwa Katiba hiyo siyo mali ya Tume wala kundi fulani katika jamii.
Alisema wananchi wamezungumzia matatizo ya kilimo, usafiri, afya, hifadhi ya jamii, maadili katika taifa na haki za binadamu… “Mambo haya katika kutoa habari hayakupewa kipaumbele, lakini mambo kuhusu kugombea urais, ubunge yalipewa kipaumbele kikubwa.”
Ukomo na uraia
Alisema tume hiyo inafanya kazi yake kwa kufuata sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba itamaliza muda wake itakapowasilisha rasimu hiyo katika Bunge Maalumu la Katiba.
Kuhusu uraia wa nchi mbili alisema: “Tulipopendekeza suala hili tulikuwa na maana kuwa isiwe lazima Mtanzania akipata uraia wa nchi nyingine awe amepoteza hadhi yake. Ndiyo maana tukasema katika rasimu kuwa atakuwa na hadhi maalumu.”Alisema nchi nyingi duniani hutoa uraia kwa watu kutoka mataifa mbalimbali lakini hawawezi kugombea urais, kuingia katika jeshi la nchi husika, kwamba sheria lazima ifafanue juu ya Mtanzania kutopoteza haki zake za msingi.
VIA MWANANCHI