ZITTO AIBUKA KIDEDEA MAHAKAMANI
Dar es Salaam. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ameshinda maombi yake dhidi ya chama hicho mahakamani.
Katika maombi hayo namba 1 ya mwaka 2014, Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, aliiomba Mahakama Kuu, Kanda
ya Dar es Salaam kuizua Kamati Kuu (CC) ya Chadema kumjadili au kuchukua
uamuzi wowote kuhusu uanachama wake.
Zitto kupitia kwa Wakili Albert Msando alikuwa
akiiomba Mahakama itoe zuio hilo la muda hadi kesi yake ya msingi
itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika uamuzi wake jana, Mahakama Kuu ilikubaliana
na maombi na hoja za Zitto na kutoa zuio kwa Kamati Kuu ya Chadema na
au chombo chake chochote cha uamuzi kumjadili na kutoa uamuzi wowote
kuhusiana na uanachama wake, hadi kesi yake ya msingi itakaposikilizwa
na kuamuliwa.
Awali, Mawakili wa Chadema wakiongozwa na
Mwanasheria Mkuu, Tundu Lissu na Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za
Binadamu, Peter Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi
matakwa ya kupewa zuio la muda.
Katika uamuzi wake, Jaji John Utamwa alikubaliana
na hoja za Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya
kupewa zuio hilo.
Matakwa hayo ni pamoja na kuwapo kwa mgogoro baina
ya pande mbili, hasara au madhara yasiyoweza kufidiwa na usawa katika
athari kwa pande zote.
Jaji Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando
kuwa iwapo Mahakama haitaingilia kati na kutoa zuio hilo, mtoa maombi
ataathirika zaidi kuliko wajibu maombi.
Akijibu hoja ya Wakili Lissu aliyepinga hoja ya
mtoa maombi kuathirika pamoja na wananchi wa jimbo lake kwa kukosa
uwakilishi bungeni, kuwa hata akipoteza ubunge kwa kuvuliwa uanachama
utaitishwa uchaguzi mdogo, Jaji Utamwa alisema uchaguzi mdogo huwa
unachukua mchakato mrefu.
Baada ya kurejea vifungu mbalimbali vya sheria,
kanuni, amri na uamuzi wa kesi mbalimbali za Mahakama Kuu, Mahakama ya
Rufani na za nje, Jaji Utamwa alisema anakubaliana mtoa maombi.
“Kwa hiyo ninatoa zuio la muda kwa Kamati Kuu ya
Chadema na au chombo chake chochote cha uamuzi kwamba kisimjadili na
kutoa uamuzi wowote dhidi ya mleta maombi kuhusiana na uanachama wake
kusubiri kusikilizwa na kuamuriwa kwa kesi yake ya msingi,” alisema Jaji
Utamwa.
Kabla ya kufikia uamuzi huo, Jaji Utamwa
alitupilia mbali hati ya kiapo kinzani ya Chadema iliyotolewa na Wakili
Kibatala baada ya kuwekewa pingamizi na Wakili Msando ambaye alidai kuwa
katika hati hiyo, kuna taarifa za kusikia ambazo hakueleza alipozitoa.
Huku akirejea vifungu vya sheria, kanuni, amri na uamuzi wa
Mahakama mbalimbali, alisisitiza kuwa ingawa wakili anaweza kuapa kwa
niaba ya mteja wake, lakini anapaswa kueleza chanzo cha taarifa
anazozitoa katika kiapo hicho.
Baada ya kutupilia mbali kiapo hicho, Jaji Utamwa
alisema hata vielelezo vya wajibu maombi vinakufa kifo cha kawaida na
kwa hali hiyo, maombi ya mtoa maombi yanabaki bila kupingwa na kwamba
hakuna haja pia ya kujadili hoja za upande wa wajibu maombi.
Baada ya Jaji kutoa uamuzi huo, Zitto, aliwafuata
mawakili wa Chadema na kupeana nao mikono kisha akaongozwa na walinzi
wake kutoka nje ya Ukumbi wa Mahakama akipitia mlango maalumu unaotumiwa
na jaji.
Kabla ya hukumu
Zitto aliyekuwa amevalia suti ya kijivu na shati
la michirizi myeupe na ya kijivu aliwasili mahakamani hapo saa 7:45
mchana akiongozana na walinzi wake binafsi (mabaunsa), wapambe na wakili
wake.
Baada ya kufika alikwenda katika chumba maalumu
ambako alipumzika hadi saa 9:45 alasiri alipoingia katika ukumbi na
kukaa katikati ya wapambe wake huku nyuma yake wakiwapo walinzi wake.
Jaji Utamwa aliingia mahakamani saa 9:56 alasiri
na kuanza kusoma uamuzi wake akianzia na pingamizi la Zitto kwenye hati
ya kiapo kinzani cha Chadema kisha akamalizia na uamuzi wa maombi ya
msingi. Hukumu hiyo ilimalizika kusomwa saa 11:10 jioni.
Baada ya hukumu
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Wakili Msando
alisema wameupokea kwa furaha uamuzi huo wa mahakama na kwamba hiyo ni
hatua mojawapo ya haki akisema anaamini kuwa mteja wake atapata haki
anayoitafuta.
Hata hivyo, Lissu na Kibatala kwa nyakati tofauti walisema kuwa ingawa wanakubaliana na uamuzi huo, hajawaridhika.
Maombi hayo ya Zitto yaliyotolewa uamuzi jana
yanatokana na kesi ya msingi aliyofungua mahakamani hapo Januari 2,
mwaka huu, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa
Chadema.
Katika kesi hiyo anaiomba Mahakama izuie chama
hicho, wakala wake na vyombo vyake vya uamuzi kumchukulia hatua zozote
wala kumjadili kuhusiana na uanachama wake, hadi hapo rufaa anayokusudia
kuikata Baraza Kuu la Chadema kupinga kuvuliwa nyadhifa zake
itakaposikilizwa.
Kesi hiyo ya msingi imepangwa kutajwa Februari 13, 2014.
Mapambano tena
Wafuasi wa Chadema wanaomuunga mkono Zitto na wale
wa uongozi wa juu, jana walipambana tena mahakamani kwa ngumi na mawe
kisha kusababisha watu wawili kujeruhiwa.
Vurugu hizo zilitokea saa 7.55 mchana muda mfupi baada ya Zitto kuingia mahakamani.
Katika vurugu hizo, mmoja wa wafuasi hao ambaye
jina lake halikujulikana mara moja, aliumizwa kichwani baada ya kupigwa
na jiwe na mwingine alipigwa jiwe tumboni na kupelekwa hospitali.
Kutokana na vurugu hizo, polisi waliyatenganisha makundi hayo katika sehemu tofauti na kukaa katikati ili kuyatenganisha.
Wakati Zitto akiwasili mahakama hapo, wafuasi wake
walikuwa wakiimba `Zitto Zitto kama Mandela’ hali iliyowalazimu
wafanyakazi wa Mahakama kuingilia kati na kuwazuia.
Makundi hayo ya wafuasi wa chama hicho yalifika mapema saa 6:30 mchana mahakamani hapo kusikiliza uamuzi uamuzi wake.
Ulinzi katika eneo lote la Mahakama uliimarishwa,
makundi ya polisi wa kawaida na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU), waliokuwa na silaha pamoja na mabomu ya machozi walitanda
sambamba na askari wa kikosi cha mbwa, magari manane ya polisi na matatu
ya maji ya kuwasha.
Kama ilivyokuwa juzi, ni wafuasi wachache walioruhusiwa kuingia ndani ya chumba cha Mahakama.
Baada ya mahakama kutangaza uamuzi wake, wafuasi
wa Zitto walishangilia kwa nguvu na kuondoka wakiimba nyimbo za kumsifu
kiongozi huyo.
Mtei amwonyesha mlango Zitto
Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei amemtaka Zitto aunde chama chake au atafute kingine cha kujiunga nacho kwa kuwa kwa sasa hana nafasi.
KWA HISANI YA MWANANCHIMwasisi wa Chadema, Edwin Mtei amemtaka Zitto aunde chama chake au atafute kingine cha kujiunga nacho kwa kuwa kwa sasa hana nafasi.
Pia ameshauri kuwa kama ana ndoto za kuwania urais
ni vizuri akatafute vyama vingine kama CCM au CUF kwa kuwa ndani ya
Chadema kwa sasa hahitajiki.
Mtei alisema kuwa kama anataka kubakia na
uanachama wa Mahakama wao hawana shida... “Lakini huwezi kuwapeleka
viongozi wako kortini na bado ukaendelea kubaki kuwa mwanachama wetu.”
Alimtuhumu kwa kuwagonganisha viongozi mbalimbali
ndani ya Chadema na hata kuzua mitafaruku ya hapa na pale huku akisema
kwamba uamuzi wa Kamati Kuu ndiyo wa mwisho.