Bukobawadau

Changamoto ya Zao la Vanilla ni Soko au Uzalishaji?: Mtazamo wetu Maruk Vanilla Farming and Processing Ltd

Vanilla inapanda na kushuka kama zao mbadala la kibiashara mkoani Kagera. Historia ya zao hili mkoani Kagera inaenda nyuma kuanzia miaka ya 1940. Lakini ni miaka ya hivi karibuni ndipo vanilla imepata kutambulika na kulimwa kibiashara. Miaka ya 90, wakati bei ya mapodo ilipofika mpaka TZS 60,000 kwa kilo, watu wengi walihamasika kujiunga na kilimo cha zao hili. Baada ya soko la Kimataifa kufulikishwa na uzalishaji mkubwa kutoka Madagascar bei iliharibika sana. Katika nchi nyingi wakulima walikata tamaa na wengi waling’oa miche na kuhamia kwenye mazao mengine.

Mkoani Kagera, kwa muda mrefu MAYAWA wamejitahidi kuwa watetezi na mabalozi wa vanilla. Wamenufaika pia kwa kuwa wanunuzi pekee wa zao hili Kagera mpaka miaka ya hivi karibuni. Nje ya jitihada za MAYAWA na wadau wao wa maendeleo, bado mchango wa serikali haujatoshereza kuonyesha kutoa kipaumbele kwenye zao hili.

Ziko changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ndogo ya zao la vanilla. Kila mdau ana mtazamo wake juu ya ipi kweli ni shangamoto inayostahili kupewa kipaumbele kwa wakati huu. Wako wanaodhani soko ndiyo changamoto kuu na wako pia wanaoamini kuwa changamoto ni uzalishaji mdogo na usiokidhi viwango. Maruku Vanilla tunaamini katika hii ya pili na daima tumekuwa tayari kuonyesha jinsi uzalishaji ulivyo changamoto na namna gani unaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Imani yetu imejengwa juu ya uzoefu tuliokusanya awali kama wakulima, kisha wanunuzi na wasindikaji, na sasa wauzaji wa vanilla ndani na nje ya nchi.

Tukiwa kama wakulima tunatambua kuwa miche mingi kwenye mashamba ya wakulima ni mizee na haipati matunzo mazuri. Pia tunatambua kuwa baadhi ya wakulima wameng’oa miche mizuri na kuachana na zao hili kutokana na mifumo isiyo rafiki katika manunuzi. Mathalani mkulima kumkopesha mnunuzi kwa mwaka mzima tena bila riba! Kwa uchache hizi ndizo sababu za msingi za uduni katika uzalishaji. Kwa kuzitambua changamoto hizi, sisi kama MVFP Ltd toka mwaka jana tumekuwa katika Programme endelevu ya usambazaji wa miche mipya kwa wakulima wa zamani vijijini. Mpaka sasa tumewafikia zaidi ya wakulima 400. Tumeweza pia kuwaunganisha wakulima wapya na wazoefu ili kujifunza kwa vitendo. Ili kuhakikisha wakulima wanajenga mapenzi ya kudumu na hawavunjwi moyo tena na mfumo wa manunuzi, MVFP Ltd imekuwa na sera ya malipo ya papo kwa papo katika manunuzi ya vanilla. Sera hii imetekelezwa kikamilifu mfululizo bila kuvunjwa toka tulipoanza kujishughulisha na ununuzi takribani miaka mitatu iliyopita. Programme yetu na Sera yetu ya manunuzi tayari vimeonyesha kuleta matokeo chanya. Wakati programme itaonyesha matokeo makubwa baada ya miaka mitatu ijayo, Sera tayari imeonyesha kufufua moyo wa wakulima kulipenda, kulijali na kulithmini zao la vanilla.

Hatuamini kwamba tatizo la zao la vanilla ni masoko kwa sababu masoko yapo, ni mengi ila yana vigezo ambavyo kimojawapo ni usambazaji-stahimilivu. Na kwa bahati mbaya sharti la mwisho bado ni gumu sana kwa wazalishaji wa Kagera na Tanzania kwa ujumla. Mwaka 2011 MVFP Ltd ilishiriki maonyesho ya BioFasch Ujerumani. Mwakilishi wetu alikutana na wanunuzi na wauzaji mbalimbali wa viungo vya chakula (spices). Miongoni mwao ni magwiji wa uujuzaji wa vanilla kama Nielsen Massey. Sampuli za vanilla yetu ziliwavutia sana wanunuzi na kila mmoja alikwenda hatua moja zaidi kutaka kukamilisha Mkataba wa manunuzi na kampuni yetu. Kwa mnunuzi wa kiwango cha chini, tulihitajika pamoja na kukidhi vizego vingine (kama organic certification, traceability, n.k), kuthibitisha kwamba tutaweza kuwa tunapeleka tani 15-20 za vanilla kavu ya dalaja la I&II kwa mwaka kwa miaka mitatu mfululizo! Hii ni sawa na tani 100 za mapodo; uzalishaji ambao haujapata kufikiwa miaka ya karibuni mkoani kwetu hata kama MVFP Ltd ndiye angekuwa mnunuzi pekee. Kwa kuwa tulijitangaza katika maonyesho haya na tumeendelea kuonekana kwenye mitandao ya vyama vya Kisekta katika Taifa na Katika kanda ya Afrika na vilevile tunapatikana katika mitandao mikubwa ya Biashara ya mazao kwenye intanei, tumekuwa tukipata orders zilizothibitika kuwa za kweli kutoka kila pembe ya dunia kuanzia  Turkey, Dubai, German, Pakistan, South Africa mpaka Amerika. Changamoto inayotufanya tushindwe kunufaika na orders hizi imekuwa ile ile; UZALISHAJI DUNI. Uzoefu huu ndivyo msingi wa hoja yetu kwamba tatizo siyo soko bali uzalishaji. Katika masoko haya haya pia kunapatikana wanunuzi wadogowadogo. Lakini haina tija kwa muuzaji kutuma kilo 100 kutoka Tanzania mpaka labda Urusi. Itabidi muagizaji awe tayari kulipa bei kubwa maradufu ili muuzaji aweze kurejesha ghalama zake na kupata faida ya kawaida sana.

Kutokana na mtazamo huu, rai yetu kwa wadau na wale wote wenye mapenzi mema ya kukuza zao la vanilla ni kwamba tuunganishe nguvu katika kutatua changamoto ya uzalishaji duni. Kama ni masoko, MVFP Ltd siku zote tumekuwa tayari kugawa masoko na orders ambazo ziko nje ya Uwezo wetu. Na hakuna hata mmoja miongoni mwa wale tuliowapasia orders ameweza kupata mzigo wa kutosheleza mahitaji ya wanunuzi isipokuwa jirani zetu Uganda. Tunaamini kwamba katika sekta ndogo ya vanilla yapo maeneo tunapaswa kushindana na yapo pia yale tunayopaswa kushirikiana kwa ustawi wa sekta. Uzalishaji si eneo la kushindania bali kushirikiana. pia kwa sasa masoko siyo eneo la kushindania maana ni mengi kuliko uwezo wetu wa uzalishaji na usambazaji.

Imeandaliwa na:
Murshid Hassan,
Mwenyekiti,
Maruk Vanilla Farming and Processing (MVFP) Ltd,
P.O Box 1361, Bukoba
Mob: 0717972957/0684627030
E-mail: marukuvanilla@gmail.com
Next Post Previous Post
Bukobawadau