JAGUAR;MWANAMUZIKI MILIONEA ALIYEANZA KWA KUOSHA MAGARI
Zipo baadhi ya kauli za Wahenga wa Kiswahili ambazo siyo rahisi
kutimia au uhaliasia wake kuonekana kwa haraka katika maisha ya kila
siku.
“Hata mbuyu ulianza kama mchicha” Kauli hii
maarufu katika jamii hasa vijana wanaojihusisha shughuli ndogondogo huku
wakiamini kwa kazi hiyo ipo siku wao wapata utajiri kwa kidogo
wanachokipata na kuhifadhi.
Fikra hizo pia zilikuwa kichwani mwa Charles Kanyi
(Jaguar), mwanamuziki kutoka nchini Kenya ambaye sasa anatikisa Ukanda
wa Afrika Mashariki na Kati, kupitia nyimbo zake
mbalimbali,zinazoendelea kumpa umaarufu.
Jaguar aliye miongoni mwa wanamuziki matajiri
nchini Kenya kwa sasa alianza maisha ya kujitegemea kwa kufanya kazi ya
kuosha magari.
Msanii huyo nyota anayedhihirisha uwezo mkubwa
kifedha kwa kumiliki magari na vito vya thamani, anakiri kwamba alikuwa
na maisha magumu kiasi cha kulazimika kutegemea kazi ya kuosha magari
ili kupata mkate wake wa siku.
Pamoja na kuwa na uwezo mkubwa kimaisha sasa,
Jaguar anasema kuwa hapendi kujionyesha kuwa yeye ni tofauti na wengine
wanaomzunguka hivyo hupenda kujichanganya.
Anaeleza kuwa hali hiyo inatokana na maisha magumu
aliyoishi tangu alipokuwa mdogo, baada ya kifo cha mama yake ambapo
alijikuta akilazimika kulala katika daladala alizokuwa akiziosha.
Jaguar alikuwa akitembea mwendo mrefu kwenda
shule, lakini kutokana na mapenzi makubwa katika elimu alikuwa
akiwashawishi hata baadhi ya madereva wa daladala wammruhusu kupanda
bure magari yao ili kuwahi shuleni, pia kurejea nyumbani.
Changamoto alizopitia Jaguar, zinamfanya kupenda
kujiweka karibu na jamii yake licha ya utajiri na maisha ya juu
anayoishi nyota huyo kwa sasa.
Mara kwa mara Jaguar amekuwa akishiriki katika
shughuli na kampeni mbalimbali za kijamii kwa lengo la kuleta mabadiliko
na kuwasaidia wengine wanaopitia kwenye changamoto za kimaisha.
Katika Sikukuu ya Krismasi ya mwaka jana, Jaguar
alikwenda katika moja ya magerezani nchini Kenya na kusherehekea siku
hiyo pamoja na wafungwa.
Akiwa amevalia sare zinazolingana na wafungwa hao,
msanii huyo alishiriki chakula cha mchana na kundi hilo lililosahaulika
katika jamii.
Siku zote Jaguar amekuwa na imani kwamba kila mtu ana umuhimu
katika jamii, hivyo ni jukumu lake kuhakikisha anamsaidia kila anayeweza
kumfanyia hivyo kadiri ya uwezo wake.
Imeandaliwa na Elizabeth Edward