KAMATI KUU YA CHADEMA KUKUTANA KWA DHARURA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Kamati Kuu
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) itakutana kwa ajili ya kikao cha
dharura, Februari 14, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Katika kikao
hicho, Kamati Kuu itajadili na kufanya uteuzi wa mwisho wa jina la mgombea
ubunge wa CHADEMA katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa,
unaotarajiwa kufanyika Machi 16, mwaka huu.
Kikao hicho kitafanya
uteuzi wa mwisho, baada ya mchakato wa ndani wa kumpata mgombea ubunge wa Jimbo
la Kalenga kwa tiketi ya CHADEMA, kuwa umepitia hatua za awali, ambazo ni pamoja
na watu wote wenye nia ya kugombea, kuchukua fomu za uteuzi wa ndani tangu
Februari 5-10, mwaka huu.
Kama
ilivyoelezwa kwa umma kupitia vyombo vya habari, Februari 6, mwaka huu, fomu
hizo zilitolewa katika maeneo matatu, Ofisi za Makao Makuu ya Chama, Dar es
Salaam, Ofisi za Jimbo la Kalenga na kwenye tovuti ya chama, ambayo ni; www.chadema.or.tz.
Jumla ya
watu 16 waliweza kuchukua fomu za kuwania uteuzi huo, ambapo hadi siku ya
mwisho, watu 13 waliweza kurejesha fomu zao na kupita kwenye mchakato wa kura
za maoni, zilizofanyika Februari 12, mwaka huu.
Imetolewa leo Februari 13, 2014, Dar
es Salaam na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA