Bukobawadau

KONGAMANO LA WANAWAKE WA KIISLAMU WILAYANI NGARA


Wanawake wa kiislamu  wametakiwa kutambua umuhimu wao katika dini ikiwa ni pamoja na kulinda maadili kwa kuzingatia mafundisho ya Mwenyezimungu na mtume Mohamadi SAW 
Wito huo ilitolewa juzi na kiongozi wa waislamu wilayani Ngara mkoani Kagera Shekhe Rajabu Abdallah Msabaha wakati akifungua kongamano la  wanawake wa kiislamu linalofanyika  kwa siku tatu katika mtaa wa Benaco ulioko wilayani Ngara
Shekhe  Msabaha alisema kuwa  wanawake wanao wajibu wa kujifunza dini yao kwa kuhakikisha wanafuata na kuzingatia maadili mema ili kuweza kurithisha vizazi vinavyotoka katika migongo na matumbo yao
Alisema malezi na maadili mema katika familia yanategemea wanawake kwani ndio walimu wa kwanza kuwafunza watoto katika kufuata misingi inayokubalika katika jamii waliyomo na dini yao
 “Kwa asilimia kubwa akina mama ni walezi wa  watoto tunao wazaa hivyo mkipata elimu ya dini kwa hakika mtaisambaza  kwa familia na watoto kuwa na maadili ya kiislamu kisha  kupatikana nusura kutoka kwa Allah S.W”. Alisema Sheikh Rajabu
Kwa upande wake Imamu Athumani Abubakari Ally  kutoka  Msikiti wa istikama ulioko Ngara mjini  aliwahimiza wanawake hao kufanya ibada za dini yao bila kujivunia ibada zinazofanywa na waume  ama watoto walioko katika familia.
Alisema kuwa  wanawake wanatakiwa kupata elimu ya kufanya ibada  katika taratibu na misingi ya dini hasa kujua namna ya kusali sala mbalimbali na masharti yake ili kuepuka  kufuata matendo bila elimu inayotakiwa 
“Mafundisho ya Q’urani ambayo ni kitabu cha Allah na hadithi za Mtume SAW ni kuhakikisha wanawake na wanaume wanakuwa na maadili kwa misingi ya imani  ya dini pamoja na kuvaa mavazi ya kusitiri miili kiislamu”.Alisema Athuman Ally
Aidha mwenyekiti wa  wanawake wa kiislamu wilayani Ngara Bi Zaria Mohamudu alisema malengo ya kongamano hilo ni  kuwafunza wanawake  kuzijua  haki zao kidini na kwenye jamii na kuondoa vitendo vya kunyanyasika kwenye familia
Alisema kuwa jambo lingine ni kuhakikisha wanapata elimu ya ujasiliamali na kujikwamua kiuchumi kwa kutumia misingi inayokubaliwa na dini  ya kiislamu kwa kuepuka kutoa  na kuchukua mikopo yenye riba.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na wahadhiri wa kiislamu kutoka wilayani Ngara na wilaya nyingine mkoani Kagera  pamoja na  waliotokea Mwanza na Nairobi kwa kutoa mada za ndoa taraka na mirathi kwa wanawake na haki zao katika familia.
 Na Shaaban Nassibu Ndyamukama
Next Post Previous Post
Bukobawadau