MIZIKI YA INJILI NI BIASHARA NDANI YA HEKALU
Na Prudence Karugendo
MWANAMUZIKI mmoja, au niseme mwimbaji, kwa vile muziki wa
sasa, hasa huu unaoitwa wa kizazi kipya
au Bongo fleva, hauhitaji vyombo vya muziki zaidi ya waimbaji kupeleka mashairi
yao studioni na kutafutiwa sauti za kwenye kompyuta, kasema anaachana na muziki
huo wa kizazi kipya na kuugeukia muziki wa injili. Kwa uamuzi huo wapo walioona
na wengine kudhani kuwa mwanamuziki huyo kaamua kumgeukia Mungu kwa maana ya
kuokoka.
Niseme
kwamba, kwa mtazamo wangu, sioni kama kuna kitu kuokoka hapo kutokana na muziki
wa injili ulivyo, ambao unatamba kwa
sasa. Sababu muziki wa injili ulio sokoni kwa kipindi hiki umekaa kibishara
zaidi kuliko kiimani. Kusema ukweli muziki wa injili wa sasa umekaa kibiashara
kuliko hata muziki wa Bongo fleva!
Kwa mujibu
wa Injili, mwongozo wa imani ya Kikristo, kitu imani, maneno ya imani au ya
kutia imani, havijawahi kuuzwa mahali popote. Hata Yesu Kristo, aliyekuja na
injili na kuwa mwinjilishaji wa kwanza alikemea sana tendo la kutumia injili au
maneno ya Mungu kwa ajili ya kutafuta riziki. Ni kwa sababu injili inapaswa
kushibisha na kuneemesha roho, wala sio kushibisha na kuneemesha mifuko na
miili.
Lakini kwa
sasa injili inaonekana inavyotumiwa na baadhi ya watu kuzalisha kipato binafsi
kilichojitenga kabisa na maneno ya injili yenyewe! Hata mwonekano wa wale
wanaoitumia injili kujipatia kipato, kama walivyo wanamuziki wa injili,
unajionyesha usivyofanana kabisa na mwonekano wa wainjilishaji wengine, kitu
kinachoweka bayana kwamba wahusika hawajali wanachokinadi kinamwendea au
kumuingia nani, bali wanakijali tu kile kinachotokana wanachokinadi, pesa,
jambo linalotuleta kwenye majumuisho ya pamoja kwamba kinachofanyika ni
biashara kamili.
Katika
injili tunaona kwamba kulitokea kitu kilichokuwa kama kongamano la injili, watu
wakakusanyika toka mataifa mbalimbali, na Yesu Kristo akahubiri na kuponya.
Kutokana na wingi wa watu hao na umbali wa walikotoka wakajitokeza watu wa
kuwauzia huduma, lengo likiwa ni kufanya biashara kwa kujinufaisha na wingi wa
watu hao. Jambo hilo halikumfurahisha Yesu Kristo hata kidogo.
Kristo
aliona kwamba wauza huduma hao hawakuja kwa ajili ya neno la Mungu wala ukubwa
wa neno hilo, bali kulitumia neno hilo
kwa ajili ya maslahi yao binafsi ya kimwili yasiyokuwa ya kiroho. “Yesu
akaingia hekaluni, akawafukuza wote waliokuwa wakiuza na kununua hekaluni,
akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa”
Mathayo 21: 12.
Kilichomkasirisha
Yesu ni watu kutumia jina la Mungu kufanya biashara zao. Sidhani kama hilo
linaweza kugeuka anapowaona wanaoimba muziki wa injili kwa lengo la kujipatia
pesa wakidai wanamtukuza Mungu. “Akawambia, imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi” Mathayo 21 :
13.
Kama muziki
wa injili unamtukuza Mungu inakuwaje unauzwa pamoja na kutozya viingilio
unakochezwa? Ni lini tulimsikia au kumsoma Yesu Kristo akitozya viingilio kwa
ajili ya kuwahubiria watu neno la Mungu?
Maana yote
tuyafanyayo kuhusu injili mwongozo wake ni Kristo mwenyewe. Sasa unafanyaje
yaliyo tofauti na matendo ya Kristo halafu unadai unaitangaza injili?
Mwimbaji
mmoja wa muziki wa injili alialikwa kwenye usharika fulani, ambako kulikuwa
kunafanyika harambee ya kutunisha mfuko wa ujenzi wa kanisa. Baada ya mwimbaji
huyo kuimba wimbo mmoja alianza kudai alipwe pesa yake shilingi laki tatu! Eti
naye huyo tuseme anamwimbia Bwana! Anamwimbia au anamwibia?
Muziki wa
injili kwa sasa ni muziki kama ilivyo mingine yote, unachezwa kwenye maharusi,
kwenye baa na sehemu zote za starehe. Kibaya zaidi ni pale muziki huo
unapotumika kuchochea matendo aliyoyalaani Mungu badala ya kuyazuia huku
ukiendelea kutumia jina la Mungu na maneno yake! Kuna ushuhuda unaoonyesha kuwa
muziki huo unapigwa hata kwenye sehemu zote za kufanyia maovu!
Ajabu
hatujasikia hata mara moja wanamuziki wa injili wakililalamikia hilo la muziki
wao kupigwa kusikostahili. Wao wanachokijali ni mauzo ya muziki wao wakifurahia
kipato kinachotokana na mauzo hayo.
Nitoe mfano
wa Waislamu, imani ya Kiislamu inazingatia zaidi maadili yake. Haiwezekani
Waislamu wakavumilia kuona au kusikia chochote kinachohusiana na imani yao
kikitumika kusikohusika wakakubali kukaa kimya kwa kuutegemea ukimya huo
uwapatie kipato cha aina yoyote. Ni lazima watakomesha tabia hiyo mara moja.
Lakini sasa
muziki wa injili unaonekana unavyotumika kuhamasisha ngono, ufusika, ulevi na
uchafu wa kila aina bila ya wahusika kuchukua hatua yoyote ya kukemea jambo
hilo! Hiyo maana yake ni kwamba wanakubaliana na matendo hayo!
Nakubali
kwamba muziki una gharama kuutengeneza, lakini hatahivyo kama maneno yaliyomo
ni habari njema kwa wanadamu, Injili, basi ingetafutwa namna ya kukusanya pesa
ya kuutengeneza, kwa njia iliyo safi, kusudi ikibidi muziki huo usambazwe na
kugawiwa bure kwa watu ikiwa ni sehemu ya sadaka, kuliko kuonekana yanatumika
maneno ya Mungu kibiashara, yaani biashara hekaluni. “Pozeni wagonjwa, fufueni
wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure” Mathayo 10 :
8.
Siku za
nyuma tulizoea kuiona na kuisikia miziki ya injili kwa maana halisi ya injili.
Miziki hiyo ilikuwa ikipigwa katika maeneo ya kweli inakohubiriwa injili, yaani
makanisani na kwenye mikutano ya injili bila waimbaji kulipisha viingilio wala
kudai malipo ya ziada kwa ajili ya kazi hiyo ya kuimba nyimbo za kumtukuza
Bwana.
Namkumbuka
mzee mmoja aliyekuwa mahiri katika utunzi, uimbaji na uongozaji wa nyimbo za
injili katika Jimbo Katoliki la Bukoba, Marehemu Bernard Buberwa, wa Parokia ya
Mwemage, Ibwera Bukoba Vijijini. Mzee huyo alitunga nyimbo nyingi ambazo
nyingine bado zinaendelea kutumika
makanisani katika Jimbo la Bukoba.
Lakini mzee
huyo hakuwahi hata mara moja kutumia kipaji chake hicho kwa ajili ya biashara
zaidi ya kukitumia kumuimbia Mungu na kutangaza neno lake kwa njia hiyo. Huyo
ndiye hatuwezi kumweka fungu moja na wafanyabiashara hawa wa muziki wa injili
wanaoligeuza hekalu la Mungu kuwa pango la wanyang’anyi, kama alivyosema
Kristo.
Tunawaona
waimbaji wazuri waliojaliwa bure vipaji vya sauti na uwezo wa kuimba, lakini
kwa vile wanashindwa kutoa bure walivyopata bure ni mashaka makubwa kusema
kwamba wanachokifanya ni kwa ajili ya Mungu.
Naamini
kwamba ni dhambi kumhusisha Mungu na biashara. La sivyo wenye pesa peke yao,
matajiri, ndio pekee wangetarajiwa
kuingia mbinguni kama Mungu angekuwa anatoza kiingilio.
Lakini kwa
kuonyesha kwamba mali, pesa na utajiri ni vitu mbalimbali na utajiri wa
mbinguni, Yesu alipomtembelea tajiri mkubwa, aliyeona kwamba pamoja na utajiri
wake bado anataka awe na uhakika wa kuingia mbinguni, Yesu alimwambia agawe
mali zake zote na kisha amfuate yeye. Kwa maana ya kwamba unapoutamani utajiri
wa mbinguni hunabudi kuukana utajiri wa duniani. Soma Mathayo 19 : 16 – 26.
Ndiyo miziki
ya injili tunaipenda tukifurahia midundo yake, ila hilo lisitufanye tuwaone
wanaotoa midundo hiyo kuwa ni watu waliokolea kwa neno la Mungu wakiwa
wamedhamiria kulifikisha kwa wengine. Hawa wanalitumia tu neno la Mungu
kujipatia kipato binafsi, ni watu wanaofanya biashara kwenye hekalu na Mungu
bila kujali kuwa wanamchikiza Yesu Kristo.
Kama kweli
tunaizingatia injili hatunabudi kuwalaani