SIRI YAFICHUKA MAUAJI Z'BAR
Zanzibar Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji (KZU)
na Polisi wamefanikiwa kuvunja zege lililokuwa limejengwa kufunika
kisima walichotupwa raia wawili wa Ufaransa, baada ya kuuawa na kupata
sehemu za miili yao ikiwamo fuvu la kichwa.
Aidha, siri za mauaji hayo zimeanza kuvuja,
ikielezwa kwamba waliotekeleza unyama huo walilenga kupora nyumba na
kiasi kikubwa cha fedha.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi na
Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI) Yussuf Illembo, alisema kuwa hadi jana
mchana, mifupa miwili ya mapaja, fuvu la kichwa na miwili ya mbavu
imepatikana kutoka ndani ya kisima hicho.
Alisema kwamba Kikosi Kazi cha Uokoaji kinaendelea
kufanya kazi eneo hilo la Matemwe lililopo Shehia ya Kaskazini, Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
“Kazi bado ni ngumu, tunaendelea kuzamia ndani ya
kisima na itakapokamilika tutatoa taarifa. Tuacheni kwanza tufanye kazi
hii nzito na ngumu kwa wakati huu,” aliomba DCI Illembo.
Zoezi hilo lilifanyika huku likishuhudiwa na ofisa
mmoja wa Ubalozi wa Ufaransa nchini na kuelezwa kuwa marehemu hao
walinunua eneo la ardhi na nyumba kwa Sh150 milioni kwa kutumia jina
moja la mzawa wa Zanzibar, kutokana na sheria kutoruhusu wageni kumiliki
ardhi visiwani humo.
Watu hao, Francios Chererobert Daniel, aliyekuwa
mtumishi mstaafu wa ngazi za juu wa Serikali ya Ufaransa na mkewe
Brigette Mary, walipotea tangu Desemba 27 mwaka jana.
Baadaye taarifa za kupotea kwa watu hao
zilifikishwa Polisi ndipo msako wa kuwatafuta ulipoanza na baadaye
kugundulika kuwa, kuna watu wameuawa na miili yao kutupwa katika kisima
cha maji kilichopo ndani ya ua wa nyumba hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya waokoaji na mashuhuda wa
tukio hilo, waliliambia gazeti hili kwamba sehemu hizo za mwili
zinazosadikiwa kuwa za Wafaransa hao, zimefukuliwa baada ya kazi kubwa
ya kuvunja zege kwa kutumia mashine maalumu inayofanywa na Kikosi cha
Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wakazi wa eneo hilo.
“Tumefanikiwa kutoa sehemu ya miili, imehifadhiwa
katika Hospitali ya Mnazi Mmoja,” alisema mmoja wa mashuhuda aliyeomba
jina lake lisitajwe.
Alisema kuwa kazi ya kuvunja zege hilo ilikuwa ngumu, walilazimika kuwachukua vijana wengine raia wa kawaida ili kuifanikisha.
Akielezea mazingira waliyokutana nayo chini ya
kisima walichotupwa Wafaransa hao, alisema kuwa baada ya zege kuvunjwa
walikuta nguo nyingi zimejazwa chini yake na juu yake kujengwa zege hilo
kabla ya kumwagwa saruji isiyochanganywa kitu ili kufunika kisima kwa
lengo la kupoteza ushahidi.
Hata hivyo, vyanzo vya habari vinaeleza kuwa zoezi hilo
lililazimika kusitishwa kutokana na sehemu ya chini ya kisima kupita
mkondo wa maji ya bahari, hivyo kulazimika kutafuta mashine ya kuvuta
maji.
“Kazi hiyo ikiweza kufanyika ndipo tutakapoweza
kwenda katika kina kirefu zaidi cha kisima hicho ili kukusanya mifupa.
Tukipata idadi ya mifupa na mafuvu yote, tutaweza kujua waliouawa ni
wangapi,” kilieleza chanzo kimoja.
Sheha wa Shehia ya Matemwe Kusini, Denge Khamis
Silima alisema kuwa wanapata faraja kuona zoezi hilo limepata mafanikio
tofauti na siku ya kwanza na kwamba kazi hiyo inaendelea kufanyika kwa
umakini huku akiitaka Serikali kuwapatia vifaa waokoaji ili kufanikisha
kazi hiyo.
Siri ya mauaji
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa siri ya
mauaji hayo ni baadhi ya watu kutaka kupora nyumba, waliyokuwa wakiishi
Wafaransa hao pamoja na fedha zinazodaiwa walikuwa nazo raia hao wa
kigeni wakitaka kununua eneo la kujenga hoteli kwenye ufukwe wa Urowa.
Inelezwa kuwa kabla ya kuingia Zanzibar, Wafaransa
hao walifikia Nairobi nchini Kenya ambako inadaiwa kuwa mmoja wa
wanasiasa wakongwe nchini humo aliwashauri kwenda Zanzibar kuishi na
kuwekeza.
Taarifa zaidi kutoka ndani ya Jeshi la Polisi
zinaeleza kuwa mazingira ya tukio hilo yanaonyesha kuwa kabla ya watu
hao kuuawa, mbwa wao aliyekuwa akifahamika kwa jina la Allan, alipewa
chakula chenye sumu na kufa na kwamba sehemu ya mabaki ya chakula hicho
yaliliwa na mbwa wa jirani ambaye pia alikufa.
Aidha, mifuko mitupu ya saruji inayosadikiwa
kutumika katika ujenzi wa zege la kisima hicho, imeokotwa nyuma ya ukuta
wa nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi Wafaransa hao.
CHANZO MWANANCHI.
CHANZO MWANANCHI.