TOFAUTI YA VIPATO NDIO MWANZO WA UHALIFU NCHINI
Na Prudence Karugendo
Nitataja rushwa ili kurahisisha maelewano, lakini vinginevyo nilipaswa kutaja mabalaa
yote yanayohusu mambo ya fedha yanayoikumba jamii yetu ya Tanzania. Ujambazi,
ubadhilifu, udokozi, usaliti pamoja na rushwa yenyewe vyote hivyo vina sura ya
aina moja.
Isidhaniwe kuwa nataka
kuongelea mishahara midogo tu, la hasha. Nia yangu ni kuongelea juu ya tofauti
kubwa ya mishahara iliyopo miongoni mwa wafanyakazi wa sekta mbalimbali za umma,
lakini zaidi katika vyombo mbalimbali
vya serikali pamoja na serikali yenyewe.
Pamekuwepo tofauti kubwa ya
mishahara miongoni mwa wafanyakazi au
watumishi wa sekta mbalimbali katika nchi yetu kiasi cha kutia kichefuchefu.
Katika idara nyingine watu wanalipwa mishahara minono utadhani hawako katika
nchi masikini kama Tanzania lakini katika idara nyingine mishahara inayotolewa
haina tofauti na zawadi, kana kwamba mtu au asasi husika haina mchango wowote
katika uendeshaji wa nchi. Kwa vyovyote hii ni miongoni mwa sababu za msingi
zinazopelekea milipuko ya vitendo vya jinai kama vilivyotajwa hapo juu.
Angalia, asasi mbili tofauti,
zote zinamilikiwa na serikali. Nyingine zinapangiwa viwango vya mishahara na nyingine zinaruhusiwa kujipangia viwango
vya mishahara ya wafanyakazi wake. Matokeo yake afisa mmoja mkubwa sana wa
asasi moja analipwa mshahara sawa na
karani wa asasi nyingine. Mfikirie mfanyakazi wa kada ya chini wa asasi
inayoendeshwa na afisa huyu mkuu. Mwisho
wa siku wote wanasema tunaitumikia serikali tukufu ya Tanzania!
Kwa bahati mbaya hii
haihusiani na viwango vya elimu wala vyeo.Yaani, unachotakiwa kuomba Mungu kama
sio kupigania kwa jinsi yoyote ni kuajiriwa katika asasi fulani. Bila kujali
elimu yako, cheo chako au utendaji wako, maisha yako yatakuwa bora, saba wa
sabini wa rafiki yako ambaye wewe ulipofeli kidato cha nne yeye aliendelea
mpaka chuo kikuu. Kwa uvivu wake wa
kuomba Mungu au kutojua njia za kupita akajikuta anapata kazi za kutangazwa
magazetini katika asasi zile zinazopangiwa viwango vya mishahara. Matokeo yake
anapata jina kubwa mitaani lakini mfukoni hamna kitu. Kwanini usimkoge?
Mfano halisi ni Nyundo na
Shoka, majina ya kubuni. Wote wamemaliza
masomo pamoja Chuo Kikuu. Kozi moja,
shahada moja na viwango vya kufaulu
sawasawa.
Nyundo, anafanya mipango
anaajiriwa katika idara ya kukusanya kodi, mshahara wake ni shilingi milioni na
nusu kwa mwezi. Nasema amefanya mipango kwa vile nafasi aliyoipata haikuwahi
kutangazwa ili kutoa haki sawa kwa wote kuiwania. Shoka kahangaika mpaka
alipoona tangazo gazetini, Polisi inahitaji watu wa fani yake. Akaomba akapata.
Mshahara unatajwa kwa makeke, TGNP 05. Lakini ukweli ni shilingi tisini na tisa
elfu na mia saba ishirini kwa mwezi, kabla ya makato yoyote. Yaani mshahara wa
mwezi wa Nyundo ni sawa na mshahara wa mwaka wa Shoka. Hana la kufanya lazima
ajiunge na kazi hiyo.
Aidha mazingira yao ya kazi
ni tofauti sana. Wakati Nyundo anashughulika zaidi na wafanyabiashara na
wakwasi, Shoka yuko na vibaka, wavuta bangi na majambazi. Hata Kingereza chake
atakisahau baada ya miaka michache. Wakati Nyundo kila siku atafurahia takrima
za wakwasi kwa kuwafanyia kazi nzuri ikiwemo kuwawezesha kutolipa kodi sahihi,
Shoka akithubutu kuchukua alfu mbili za kibaka ili amuachie, kesho habari
zimeenea mitaani kote. Kibaka na ndugu zake, na aliyeibiwa na ndugu zake, wote
wanamshutumu Shoka kwa kupenda rushwa na kufuga uhalifu. Elfu mbili itakumbukwa
milele!
Mwisho wa siku si tu vijana
hawa wanasema wote wanaitumikia serikali ya Tanzania, lakini wanakutana mitaani
na wanatembeleana majumbani. Bado ni marafiki. Wakati Shoka anaishi katika
banda la mabati alilopewa na mwajiri wake, Nyundo ameshapata bangaloo
alilojengewa na mkwasi fulani. Shoka
analazimika kuwa mhimili wa urafiki wao. Kila siku yeye ndio atamtembelea
Nyundo nyumbani. Wataponda starehe kidogo kwa ubavu wa Nyundo halafu
atarudishwa mpaka kwake kwa usafiri
binafsi wa Nyundo. Pengine hiyo ni baada ya mwaka mmoja tu wa kazi.
Kwa mawazo ya kipumbavu
tutaamini Shoka hatamani maisha ya Nyundo.
Tutaamini yeye hapendi kutembelea gari au kuwa na nyumba nzuri. Hapendi
kula vizuri au kustarehe kama Nyundo. Tutaamini kwamba kila siku atakubali
kuendelea kuwa fukara huku akimuangalia rafiki yake waliosoma wote akizidi kutajirika. Tunasahau kwamba Shoka
huyu ndiye tunaempa silaha akalinde benki. Ndiye huyu tunayemtuma akapambane na
majambazi na vibaka. Kadhalika ndiye mwenye jukumu la kutuhakikishia usalama wa
raia na mali zao akiwemo rafiki yake Nyundo.
Hata hivyo hakuna upumbavu
usio na utetezi. Hata kama kwa sababu za kipuuzi. Shoka ataambiwa kazi yake ni
wito. Yeye ni mtumishi wa serikali wakati Nyundo ni mfanyakazi katika asasi
inayojitegemea japo inamilikiwa na serikali. Lazima ajitoe mhanga kwa ajili ya
mafanikio ya nchi au wananchi wenzake. Kadhalika si ajabu kusikia kwamba hawa
tunawapa mishahara mikubwa ili wasichukue rushwa au kwa vile kazi yao
inaiingizia serikali fedha nyingi. Hata hivyo hatujawahi kusikia sababu za
wengine kupewa mishahara midogo japo tunasikia kila siku umuhimu wao
ukihubiriwa.
Unaweza kujiuliza ni nini
tofauti iliyopo kati ya serikali na idara au wakala wa serikali hadi kuwafanya
watumishi wengine waishi peponi na wengine jehanamu ndani ya nchi moja huku wakipumbazwa na miito isiyo na maana. Jiulize, ni nini hasa maana ya wito? Wote tunaajiriwa
na vyombo vinavyomilikiwa na serikali ileile, sheria za kazi ni zilezile,
tunaitumikia jamii ileile. Basi kama kazi ya mwingine ni wito na ya huyu
mwingine inaitwaje?
Fikiria tena, unaelewa nini unaposikia huyu analipwa
mshahara mnono ili asichukue rushwa, eti kwa vile kazi yake inamuweka katika
vishawishi vingi vya rushwa? Hivi ni
kweli serikali inashindwa kudhibiti mtandao wa rushwa kiasi inalazimika
kuwabembeleza wala rushwa kwa kuwahonga ili wasichukue rushwa za wakwasi na
wafanyabiashara? Kuna faida gani basi ya kuweka TAKUKURU na vyombo vingine vya
usalama na upelelezi kama hongo ya aina hii ingetosha kuzuia rushwa?
Naiita hii ni hongo kwa vile
inaonekana wazi serikali inajua kwamba viwango vya mishahara yake ni vidogo
sana kulinganisha na maisha halisi. Ndio maana kwa zile idara inazohisi ni
nyeti, inaamua kuzihonga kupitia mishahara mikubwa ili wasitamani rushwa.
Lakini ni idara gani basi ambayo
serikali inadhani sio nyeti na wala haina nafasi ya kutawaliwa na rushwa? Au inadhani imefanikiwa kiasi gani kuzuia
rushwa katika zile idara au mamlaka inazozipa mishahara minono? Kila mtu anaweza kuwa shahidi wa yanayotokea
katika idara hizo.
Wachumi wanatuambia ni kanuni
ya pesa, kwamba kadiri zinavyokuwa
nyingi ndivyo zinavyohitajika zaidi. Hatuhitaji tena ufafanuzi wa wachumi
kuweza kulielewa hili hasa tukizitazama asasi hizi zinazopewa mishahara minono.
Mpe mtu mwaka mmoja tu wa kazi tayari anaweza kuwa na jumba la kifahari na
usafiri wa bei kali, achilia mbali matanuzi yake ya kila siku. Ni kweli
serikali inatuambia hilo ni zao la mishahara minono inayowapatia watumishi hao
pekee?
Upande mwingine ni umuhimu
wanaopewa watu wa idara hizo. Tunatakiwa kuamini kwamba wanapewa mishahara
mikubwa kwa sababu shughuli zao ni muhimu zaidi kwa serikali kuliko wengine. Wakati
fulani mheshimiwa rais aliwapongeza TRA kwamba wametoa mchango
mkubwa katika mafanikio ya serikali yake. Haikuwa muda mrefu sana tangu
serikali hiyohiyo ipambane na madaktari ikiwalazimisha kuwapunguzia kipato
kidogo walichokuwa wakikipata, ikatangaza kuwaongezea mishahara TRA kwa
asilimia hamsini! Ujumbe gani unawaendea madaktari wale? Ina maana madaktari
hawana umuhimu wowote mbele ya serikali yao!
Si lengo langu kupinga
umuhimu wa asasi hizo lakini ni lazima serikali ikiri kwa dhati kabisa kwamba
hakuna idara yake iliyo ya kipuuzi. Kila idara ilianzishwa kwa sababu na
madhumuni kamili na ina ulazima na umuhimu wa kuwepo. Na kwa bahati kila
mtumishi anaujua umuhimu wake mbele yake, kama sio serikali anayoitumikia basi
jamii anayoihudumia. Ni kweli watu wanahitaji barabara za Tanroad au huduma
nyingine zinazowezeshwa na kodi, lakini pia wanahitaji elimu, wanahitaji
matibabu, wanahitaji ulinzi na usalama
wao, wanahitaji mahakimu, nk. Haya yote yanatolewa na watu ambao nao
wanahitaji kuthaminiwa kama wenzao.
Nyundo na Shoka wanawakilisha
makundi mawili ya watumishi wa, ama serikali kuu au idara zake, ambao kwa kweli
tofauti zao kwa kiasi kikubwa hazitokani na umuhimu wa majukumu yao kwa
serikali wala kwa wananchi ila viwango vya malipo yao ya mishahara. Wote tunajua kwamba katika hali
halisi heshima ya mtu hujengwa zaidi na kipato chake. Hivyo elimu, madaraka na
hata umuhimu wa mtu kwa jamii utaonekana iwapo tu kipato chake kitafanana na
kiwango cha umuhimu au elimu yake. Vinginevyo hakutakuwa na haja ya kupasua
vichwa vyuoni kama kuna njia za mkato ya kuajiriwa na asasi teule.
Awali nimesema akina Nyundo na akina Shoka hawa wanaishi
katika jamii moja, na kwa bahati zaidi ni ama majirani, marafiki au ndugu.
Wanatembeleana na wanajuana. Kila linalotokea
upande mmoja upande wa pili unaliona. Kwa hulka za kiutu ni lazima akina Shoka
wanatamani mafanikio ya akina Nyundo, hivyo itawalazimu kufanya wawezalo
wayafikie. Na kwa bahati mbaya, kama tukiamua kuwa wakweli hakuna njia yoyote
ya halali inayoweza kumuwezesha Shoka kuyafikia maisha ya Nyundo. Matokeo yake
lazima uhalifu wa jinsi yoyote utokee.
Mara nyingi tunapenda kutoa
sababu au masuluhisho ya juujuu kwa matatizo yanayotukuta. Na zaidi huishia
katika kulaumu na kutumia nguvu nyingi katika kuadhibu bila kujali vyanzo vya
matatizo hayo. Sasa hivi ujambazi unanuka kila pembe ya nchi, rushwa na
ubadhilifu vimetawala kila ofisi ya umma, na uadilifu katika ngazi zote umebaki
huwa hadithi za kisiasa tu. Ni nini chanzo chake?
Si ajabu tena kusikia askari
kashiriki ujambazi. Bunduki aliyopewa akalinde zamu kaenda kufanyia ujambazi!
Kila siku mabenki na vyombo vingine vya umma vinaibiwa kwa mabilioni na kwa
kiasi kikubwa ni kwa mipango ya wafanyakazi wake! Hujuma na wizi katika
miundombinu vimetapakaa kila sehemu,
kwanini hatutafuti vyanzo vya hali hii.
Kila siku utasikia majibu
rahisi. Kama sio tamaa basi ni ukosefu wa uaminifu kwa wafanyakazi. Ni kweli
maelezo hayo ni sahihi lakini kwanini watu wasiwe na tamaa? Kwanini mtu awe
muaminifu kama kipato chake hakimtoshi hata kwa wiki akijibana? Au hata kwa siku kama atajaribu kuishi kama
jirani yake anayefanya katika asasi teule? Vipi mtu asiwe na tamaa wakati
anawaona wengine wanavyoishi katika pepo iliyomo ndani ya Jahanam? Kuna kosa
gani mtu kutamani pepo?
Tabia ya kutamani huletwa na
kuona vilivyomo katika mazingira mtu aliyomo. Huwezi kutamani kitu usichokiona
au kukijua. Tunatamani kula vizuri kwa sababu tunawaona wenzetu wanakula
vizuri. Tunatamani nyumba nzuri kwa sababu tunaziona mitaani. Tunataka kufanya
harusi za kifahari kwa vile wengine wanafanya hivyo. Mtu hawezi kutamani kuwa
na jumba kama la Michael Jackson au kutembelea Cadilac kwa vile havipo kwenye
upeo wake. Lakini vipi afisa muaminifu wa TAKUKURU kwa miaka kumi huku akipanga
pale Buguruni asitamani kuwa na jumba kama la mdogo wake wa TRA pale Tabata
alilolijenga baada wa miezi miwili tu ya utumishi? Jiulize kitakachofuatia.
Katika mazingira ya kawaida
si ajabu mtu wa kundi la Nyundo kuniona mnoko au fitina kwa kuongelea haya,
lakini huu ndio ukweli unaopaswa kusemwa hata kama hautaweza kuibadili hali
halisi. Hatuwezi kuzuia uhalifu katika mazingira yasiyo na uwiano wa kipato kama haya. Na huu ni moja ya ushauri wangu kwa
serikali hii na ijayo. Isiruhusu tofauti kubwa ya vipato miongoni mwa watumishi
wake au wa idara, mamlaka wala wakala
zake kama ilivyo sasa.
Kama kuna muujiza wa
kupandisha mishahara ya wote basi ipandishwe angalau tofauti isiwe kubwa kama
ilivyo sasa, na kama haiwezekani basi patafutwe mbinu ya kuifanya mishahara iwe na uwiano unaoeleweka. Hakuna
atakaeacha kazi BOT kwa sababu eti mshahara umepungua. Kwanza kwa vile hatakuwa
na pa kwenda lakini zaidi kutakuwa na uwiano wa vipato mitaani. Angalau hii
itakuwa njia ya mkato ya kupunguza uhalifu.
Vinginevyo hakuna atakaekubali kuendelea kuwa masikini wakati anamuona
jirani yake anachezea pesa, ilhali wote wanaitumikia serikali moja.
0784 989 512