TUNDA LA HAYATI DK MVUNGI KWA WATANZANIA
Dk Natunjwa Edmund Adrian Sengondo Mvungi
Dk Natunjwa Edmund Adrian Sengondo Mvungi, ni mzaliwa wa kwanza
wa aliyekuwa kingunge wa sheria, Dk Sengondo Mvungi (61) ambaye Oktoba
12, mwaka jana alivamiwa nyumbani kwake na kujeruhiwa kabla ya kufariki
dunia akiwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu.
Natujwa ni daktari katika taaluma ya sheria,
Mkufunzi na Mkuu wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Bagamoyo,
kilichopo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Daktari huyu wa sheria ni miongoni mwa wateule 201
wa Rais Jakaya Kikwete, wanaotarajiwa kuungana na Wabunge wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar, kuunda Bunge Maalumu la Katiba Mpya.
Kwa fursa hiyo, atashiriki kuboresha Rasimu ya
pili iliyoandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo hayati Dk
Mvungi, (baba yake) aliyekuwa mjumbe wa tume hiyo, mpaka anapatwa na
tukio lililosababisha kifo chake, alikuwa katika hatua za mwisho za
kushirikiana na wajumbe wenzake kuandika rasimu hiyo ambayo
iliwasilishwa kwa Rais, Desemba 30, 2013.
Katika mahojiano maalumu Dk Natujwa Mvungi,
anasema nafasi ya kuwakilisha Taasisi za Elimu katika bunge hilo,
ameipata baada kupeleka jina na taarifa muhimu zilizotakiwa kuelezea
sifa zake zikiwamo za taaluma na kwamba anaamini uteuzi huo wa Rais
umemtendea haki ambayo anastahili.
“Naamini nimeteuliwa kutokana na kuwa na vigezo
vilivyohitajika; nilipeleka jina na maelezo ya sifa zangu, nashukuru
nikateuliwa natarajia kuwa wajumbe sote tutatekeleza jukumu lililo mbele
yetu kwa kuzingatia mifano ambayo tayari imeoneshwa na viongozi
mbalimbali, kupitia mijadala inayoendelea ya mchakato wa mabadiliko ya
Katiba,” anaeleza.
Dk Natugwa mwenye umri wa miaka 32, anaamini
kupevuka kwake kitaaluma na kiwango chake cha kuifahamu jamii ya
Watanzania, vikikolezwa na malezi mazuri aliyopewa na wazazi wake,
atamudu kuwakilisha siyo tu kundi la jamii lililompa nafasi ya kuingia
katika Bunge Maalumu la Katiba, bali Watanzania kwa ujumla.
Anasema pamoja na masuala ya elimu kuwekwa katika
eneo la haki za binadamu ndani ya rasimu ya Katiba mpya, anaamini eneo
hilo bado linahitaji kuboreshwa zaidi kwa kuzingatia kuwa Katiba hiyo ni
ya Jamhuri ya Muungano na elimu siyo moja ya mambo ya muungano.
Anabainisha anavyovutiwa na ukomavu wa kizalendo
unaoendelea kuonekana miongoni mwa wanasiasa na viongozi wastaafu
nchini, anawataja Jaji Joseph Warioba, Profesa Phillemon Sarungi na
Joseph Butiku.
“Hata unapofuatilia wanavyojadili masuala ya
Katiba mpya, unabaini walivyokomaa kizalendo wanafaa kuigwa na sote
tutakaojadili rasimu ya pili ili kutoa Katiba inayopendekezwa, kazi hii
ndiyo kitovu cha utaifa wetu; siyo siri wameonesha mwanga ambao
tukiufuata tutaandika historia ya uzalendo duniani,” anaeleza Dk Natujwa
Mwananchi Jumapili: Una mpango wa kuwa mwanasiasa?
Dk Natujwa: Sina jibu la moja kwa moja. Kwa sababu
siasa ni maisha ya kila siku, mfano: kukitokea mgao wa umeme
nikafuatilia ili nijulishwe tatizo, nikashiriki kutafuta ufumbuzi tayari
nakuwa mwanasiasa. Kwa maana hiyo, hata sasa mimi ni mwanasiasa.
Lakini tukizungumzia uanasiasa wa kupanda majukwaani kufanya
kampeni na kuomba kura kwa wananchi, hatua hiyo bado sijaifikia. Ninazo
sababu nyingi zikiwamo za kifamilia; ni mzaliwa wa kwanza, baba
amefariki dunia akiwa ameacha ndoto nyingi ambazo sina budi kuhakikisha
zinafikia angalau kiwango alichotarajia.
Pia ninazo ndoto zangu hususan za kuhakikisha
jamii ya Tanzania inanufaika na taaluma yangu, kwa maana ya kuendeleza
Chuo hiki ambacho baba alikuwa miongoni mwa waasisi wake ili kuongeza
wasomi nchini na kutetea wananchi dhidi ya matukio mbalimbali
yanayofanywa na baadhi ya watu, kinyume na sheria za nchi.
Mwananchi Jumapili: Pamoja na kuwakilisha jamii
inayokupeleka bungeni, una ajenda gani binafsi ambayo umejiandaa
kuiwasilisha katika Bunge Maalumu la Katiba?
Dk Natujwa: Ajenda ninayotarajia kupelekea
wenzangu ili tuijadili kwa jicho la ziada, ni mfumo na taratibu
zinazotawala suala zima la umiliki wa ardhi, kuanzia ngazi ya mtu mmoja
mmoja mpaka taifa.
Eneo hili limekuwa na tatizo ambalo sasa
linaelekea kuwa sugu kwa kiwango fulani. Inatakiwa muda, watu wenye nia
thabiti, utayari, uelewa na umakini kulijadili ili kupata ufumbuzi wa
kudumu, unaoweza kuimarisha imani ya jamii kwa serikali.
Umiliki wa ardhi kwa kiwango cha mtu mmoja mmoja
natamani kuona kukiwa na utaratibu mzuri, usiyo na ukiritimba katika
kupata hati za kumiliki ardhi na kuweka udhibiti madhubuti dhidi ya
wanaopora haki za wanyonge kumiliki ardhi.
Imeandaliwa na Editha Majura