UCHAGUZI WA MADIWANI KATA 27 CHADEMA KIDUME!!
Na Prudence Karugendo
UCHAGUZI mdogo wa madiwani uliofanyika Jumapili
iliyopita katika kata 27 nchini umenifunulia kitu kimoja muhimu. Baada ya
kuutafakari uchaguzi huo mara moja nimegundua kwamba kumbe Chama Cha Mapinduzi
hakina tena ushawishi kwa wananchi pamoja na mambo yote kiliyonayo, utawala,
mabavu na kila kitu!
CCM kimebaki
kutumia kila kitu kilicho kwenye upeo wake kuhakikisha kinabaki kileleni bila
kujali mapenzi ya wananchi huku chini yakoje. Dalili zinaonyesha kuwa chama
hicho kiko kileleni kwa nguvu zake chenyewe, na sasa uchovu unakifanya kianze
kuteleza na kushuka taratibu pasipo kupenda. Kingekuwa kimeshikiliwa na
wananchi apana shaka hali hiyo isingekuwepo, kingebaki imara kileleni.
Badala yake
ni kwamba chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema, ndicho kimedhihirisha kuwa
ni chama dume kwelikweli! Sababu pamoja na nguvu ya ziada kinayokabiliana nayo
bado kinapanda, hata kama ni kwa mwendo wa kinyonga, wakati kilicho juu
kileleni kinashuka hata bila kupenda, utelezi umekizidi nguvu!
Hatahivyo
wapo wanaochanganywa na matokeo yanayoonyesha kuwa CCM kimeshinda kata 23,
Chadema kata 3 na NCCR Mageuzi kata 1, na hivyo kuchukulia kuwa CCM imepata
ushindi wa kishindo. Kumbe mambo hayako hivyo. Wanaoyachukulia mambo kwa
mtazamo huo ni wale wasioweza kuitafsiri hali halisi.
Kwangu mimi
matokeo hayo yananifanya niipongeze NCCR Mageuzi iliyopata kata 1 kuliko CCM
iliyopata kata 23. Ni kwa sababu kabla ya uchaguzi huo mdogo, tukiangalia
uchaguzi uliotangulia, CCM ilipata kata 25 kati ya kata 27 zilizofanya uchaguzi
huo mdogo, NCCR Mageuzi haikupata hata kata 1.
Lakini
katika uchaguzi huo wa juma lililopita CCM imepata kata 23, nafasi mbili kwenda
chini, na NCCR Mageuzi kata 1, nafasi moja kwenda juu. Tuseme NCCR Mageuzi
imepata kata 1 na CCM imepoteza kata 2. Sasa nani apongezwe, aliyepata au
aliyepoteza?
Tukija
upande wa Chadema tutaona kuwa chama hicho kilikuwa kinatetea kata 2 tu lakini
kikaja kupata kata 3, kimepanda. Sababu kupoteza ni kupoteza na kupata ni
kupata. Haijalishi umepoteza au kupata kiasi gani.
Huwezi
kufiwa na mtoto mmoja ukawaambia waombolezaji wasikupe pole eti kwa vile bado
unao watoto wengine 30! Na huwezi kukataa hongera ya kuzaa kwa vile umezaa
mtoto mmoja badala ya mapacha!
Hiyo ni
kwamba mimi nikiulizwa nasema CCM imepoteza kata 2 katika 25 ilizokuwanazo
kibindoni, na Chadema imeongeza moja katika kata 2 ilizokuwa imeziweka
kibindoni. Sasa nimpongeze aliyepoteza niache kumpongeza aliyeongeza! Hayo
yatakuwa ni mehesabu ya ajabu.
Mbali na
matokeo hayo tunapaswa kuangalia uchaguzi unafanyika katika mazingira ya aina
gani, kwakweli haya sio mazingira yaliyo sawa na huru hata kidogo.
Katika
uchaguzi hapa nchini vyama vya upinzani vinaonekana kukabiliwa na upinzani toka
kila upande. Vinakabiliwa na chama tawala, wakati huohuo vinakabiliwa na Tume
ya Uchaguzi, Polisi na wakati mwingine hata Jeshi!
Ikumbukwe
kwamba wakuu wa vyombo hivyo vyote wanateuliwa na rais ambaye ndiye mwenyekiti
wa chama tawala. Je, wakuu wa vyombo hivyo vya dola wangependa kumwangusha bosi
wao kwa kukiacha chama chake kishindwe katika uchaguzi? Hivi ni nani anayeyajua
makubaliano yao yakoje anapowateua wakashike nyadhifa hizo? Maana mpaka sasa
hakuna chombo chochote cha kuhahakiki uteuzi unaofanywa na rais, aliye pia
mwenyekiti wa chama tawala.
Katika nchi
nyingi ambazo utawala unajali zaidi umimi, kuliko maslahi mapana ya umma, hususan katika Afrika, niliyoyataja hapo juu
yanaadhiri chaguzi kwa mtindo huu: Mfano hapa kwetu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo muda wote
ipo kushughulikia masuala ya uchaguzi unapojitokeza haijionyeshi kama ni ya
kudumu. Tume hiyo inaonekana kufanya mambo yake kana kwamba inateuliwa kwa
dharura tu kila uchaguzi unapotokea!
Kama sio
hivyo kwa nini Tume hiyo inakubali kuendesha uchaguzi kwa kutumia Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililopitwa na
wakati? Katika daftari hilo ni wapiga kura wangapi wanaokuwa wamepoteza maisha
lakini majina yao yakabaki kudumu kwenye daftari hilo yakionyesha kuwa hao ni
wapiga kura halali? Na kwa upande mwingine ni wananchi wangapi wanaokuwa
wamefikisha umri wa kupiga kura na hawamo kwenye daftari hilo kutokana na
kukosa uboreshaji na kuonekana limepitwa na wakati?
Kwa nini
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura usiwe endelevu kama Tume yenyewe
ilivyo endelevu? Wakati usio wa shughuli za uchaguzi Tume hiyo inafanya kazi
gani nyingine inayoizuia kutambua nani kafikisha umri wa kupata haki yake ya
kupiga kura na nani kapoteza haki hiyo kihalali, kwa maana ya kupoteza maisha?
Sababu haki
za raia ni pamoja na uhuru wa kupiga kura, na uhuru huo, kwa mujibu wa Katiba
ya sasa ya nchi yetu, unaanzia miaka 18. Sasa ni milioni ngapi za wananchi
wanaofikisha umri wa miaka 18 kila mwaka tangu daftari hilo lifanyiwe
uboreshaji kwa mara ya mwisho? Kwa nini wananchi hao wanyimwe haki yao hiyo ya
msingi kwa uzembe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi?
Je, Tume
hiyo inafanya hivyo kwa kujiamria yenyewe au kwa kuelekezwa na walioiteua?
Kuna hoja ya
ajabu inayojitokeza ya kwamba Tume inakwepa gharama za kila wakati za
uboreshaji wa mara kwa mara wa daftari hilo! Lakini cha kushangaza ni kwamba
wafanyakazi wa Tume hiyo wanapata mishahara kila mwezi! Mbona hatujiulizi kwa
nini tuwalipe watu mishahara bila kazi yoyote wanayoifanya? Au gharama hizo
zinamwendea nani?
Tume ya
Taifa ya Uchaguzi ipo kuhakikisha haki ya kila raia ya kupiga kura inalindwa,
ndiyo maana wafanyakazi wa Tume tunawalipa mishahara. Sasa inawezekanaje
tuendelee kuwalipa mishahara ilihali wakilikwepa jukumu hilo muhimu
tulilowakabidhi la kuilinda haki hiyo ya kila mwananchi kwa kisingizio cha
kukwepa gharama? Kwa nini gharama isikwepwe kwenye mishahara yao ila tu kwenye
jukumu muhimu lililowafanya wao wakaajiriwa?
Tukirudi
kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani uliopita tutaona yafuatayo. Mfano, katika
kata ya Nduli mjini Iringa, karibu uongozi wote wa mkoa wa Iringa ulishinda
katika kitongozji cha Nduli, siku ya uchaguzi, ukiwa umejihami na kikosi cha
polisi cha kuzuia fujo kikiwa kimejikamilisha na silaha zake, wakati pale
hapakuwepo na fujo yoyote. Lengo lao lilikuwa ni kuhakikisha mgombea wa chama
tawala anaibuka mshindi hata kama hakupigiwa kura na yeyote!
Mara nyingi
fujo na vurugu hutokea mahali ambako haki inapindishwa. Kama hupangi kupindisha
haki huna haja ya kutegemea fujo na vurugu vitokee. Na kama haki imekwenda
mahali pake, kwa walio wengi, huna haja ya kuwahofia sana wachache, walioshindwa,
maana walio wengi wanaweza wakajilinda. Vinginevyo kulazimisha hofu mahali haki
inapotendeka ni kuleta vurugu na fujo ukiwa umelenga kuipindisha haki.
Kule Nduli,
Iringa, hakuna chombo chochote cha dola kilichowagusa viongozi hao wa mkoa ambao
karibu wote hawakuhusika na uchaguzi wa diwani, lakini alipojitokeza mbunge wa
Iringa Mjini, Mch. Peter Musigwa, aliyekuwa anahusika na uchaguzi ule, kwa vile
Nduli ni kata ya nyumbani kwake, mbali
na kuwa mbunge wa jimbo, akiwa anaangalia mwenendo wa uchaguzi, akashikiliwa na
polisi!
Yeye na
mawakala wawili wa Chadema walishikiliwa kwa muda usiopungua masaa matatu.
Wakati huo kura zikiendelea kuhesabiwa kwa kushuhudiwa na upande mmoja tu wa
CCM! Matokeo yake CCM ikaonekana imeshinda kwa mshangao wa kila mmoja!
Kule Sombetini, Arusha Mjini, mbunge Godbless Lema amepigwa
sana na polisi. Pamoja na kwamba mbunge ni mwakilishi wa wananchi aliye na
kinga ya kutofanyiwa upuuzi na vyombo vya dola, lakini yeye kapigwa! Kumpiga
mbunge ni sawa na kuwapiga wananchi wote anaowawakilisha. Ni heri akapigwa mkuu
wa mkoa lakini sio mbunge, sababu mkuu wa mkoa hamwakilishi yeyote pale zaidi
ya kuyasimika mamlaka, utawala.
Naamini
polisi waliofanya kitendo hicho cha kuwapiga wananchi bila huruma yoyote
kupitia kwa mwakilishi wao sio vichaa, walikikusudia walichokifanya. Na kwa
vile hatukuona tamko lolote toka serikalini la kuukemea unyama huo wa polisi,
kuwapiga watu wanaowalipa mishahara ili wakawalindie usalama wao, ni lazima
tuamini kwamba vijana hao walitumwa na serikali kufanya unyama huo.
Hivyo
tunalazimika kujiuliza, serikali isiyowajali wananchi wake kiasi cha kuwapiga
bila hatia yoyote, kwa vile yenyewe inayo mabavu ya kufanya hivyo, ipo kwa
manufaa ya nani?
Kwa mantiki
hiyo, matokeo hayo yanayoshangiliwa na wana CCM, wengi wao wakiwa hawaelewi
jinsi yalivyopatikana, yamewafanya baadhi ya wana Chadema wafikirie kwamba
ingebidi chama chao kibadili mbinu za mashambulizi ya kisiasa. Eti badala ya
mashambulizi ya hanga sasa kianze mashambulizi ya ardhini kuikabili CCM.
Kinachosahaulika
ni kwamba CCM imetumia njia hiyo ya ardhini kuwapofua wananchi kwa karibu miaka
60. Kwa maana hiyo mpaka Chadema ijiimarishe na kuweza kuwaondolea wananchi
upofu uliosababishwa na CCM kwa kutumia njia hiyohiyo ya ardhini si ajabu
ikahitaji muda usiopungua miaka 40!
Ninaposema
CCM na miaka 60 wapo wanaoshangaa wakiwa wanaamini kwamba chama hicho
kimezaliwa 1977! Ieleweke kwamba kilichozaliwa wakati huo ni jina wala sio
chama. Kwani mtu akibadili jina na umri wake unabadilika?
Pamoja na
kwamba ni muhimu Chadema kujiimarisha katika ngazi ya mashina kwa wakati huu,
bado mashambulizi ya hanga ni muhimu sana. Yamekifanya chama kiwafikie wananchi
kwa haraka sana kote nchini. Ndiyo maana hata CCM kimeanza kuiga mbinu hiyo ya
hanga kinapojaribu kujifufua.
Naipongeza
sana Chadema kwa ushindi wake ilioupata katika kata 3 kwa vile ni ushindi
uliopatikana katika mazingira magumu
sana. Sababu katika hali ya hofu na kukata tamaa Chadema isingeweza kupata hata
nusu kata, achilia mbali hizo kata 3, kulingana na nguvu za dola zilizotumika
dhidi yake. Kwakweli Chadema ni chama dume, Watanzania tukiunge mkono tukiwa
tumeutupilia mbali woga wa kila aina.
0784 989 512