UONGOZI KCU(1990) Ltd UNAUKOMBA NA KUUZIKA USHIRIKA?
WAKULIMA wanaounda ushirika wa KCU (1990) Ltd. mkoani
Kagera wameamua kupiga kelele bila kuchoka, hata kama kelele hizo hazionekani
kusikilizwa na yeyote kati ya wale waliolengwa kuzisikiliza. Wao, wanaushirika
hao, wana imani kwamba kama Paulo na Sila, wanaoongelewa kwenye Biblia,
walipiga kelele wakiwa kwenye kifungo cha kuonewa milango ya jela ikafunguka
yenyewe na wao kuwa huru, basi nao itakuwa hivyo.
Wanaushirika
hao wanasema kwamba kwa sasa ushirika wao hauna chochote cha kujivunia, kitu kinachoufanya ushirika wao uonekane kama
mkusanyiko au umoja wa mateso tu.
Eti zao
ambalo ushirika huo uliundwa kulishughulikia, kahawa, halina manufaa tena kwao
kwa vile ushirika wao ni kama umelitelekeza. Kahawa hainunuliwi tena KCU (1990)
Ltd. kwa sasa kwa madai ya ushirika huo kutokuwa na pesa! Wakati ikisemekana
kwamba hakuna pesa ya kununulia kahawa chama chao hicho kinayo madeni
yasiyosemeka.
Pamoja na
chama hicho kuwa na vitegauchumi lukuki lakini kinachozalishwa na vitegauchumi
hivyo hakionekani. Ndiyo sababu vitegauchumi hivyo haviwezi kukinusuru chama
hicho cha KCU (1990) Ltd. kwa kuyakwepa madeni yanayokikabili kwa sasa.
Inasemekana
kwamba kinachoonekana katika ushirika huo ni “matanuzi” ya viongozi wasioelewa
lolote kuhusu ukata unaoukabili ushirika wanaouongoza. Eti wakitazamwa viongozi
hao haiwezi kuonekana kwamba ni watu wanaoendesha ushirika unakaribia kukata roho! Kwamba viongozi wa KCU
(1990) Ltd. ni watu wanaopendelea kujiweka ngazi moja na watu wanaoendesha
taasisi zenye ukwasi wa hali ya juu sana.
Unatolewa
mfano wa safari ya Burundi ya hivi karibuni. Eti safari hiyo ambayo imegharimu
si chini ya shilingi milioni 23, tena zikiwa ni pesa za mkopo toka benki ya
CRDB, haikuwa na umuhimu wowote kama viongozi hao wangekuwa wanaujali ushirika
wanaouongoza kulingana na hali uliyomo kwa sasa.
Pia inasemekana
kwamba, pamoja na safari hiyo kutokuwa na umuhimu wowote kwa viongozi wa
ushirika, kwa vile tayari ushirika ulikuwa naye mwakilishi kule Burundi kwa
ajili ya matakwa ya kitaalamu.
Hatahivyo
inasemwa kwamba waliolipiwa kuingia kwenye mkutano wa Burundi, ingawa hawakuwa
na umuhimu wowote kwenye mkutano huo, ni watu watatu tu, wajumbe wengine wa
bodi walienda kutalii tu ikiwa ni sehemu mojawapo ya kuiongezea mzigo KCU
(1990) Ltd. bila sababu yoyote ya maana.
Baada ya
ujumbe huo wa KCU (1990) Ltd. kutoka kwenye safari hiyo ya kitalii nchini
Burundi vikaanza kufanyika vikao vya siri kutaka kujua ni mtu gani anatoa nje
siri za uongozi. Siri zenyewe ni kama hizo za uongozi kukihujumu chama hicho
kikuu cha ushirika!
Ieleweke
kwamba uongozi wowote unaofanya mambo yawe siri, hata kwa waliouweka madarakani
uongozi husika, hiyo inakuwa ni siri isiyokuwa salama. Mara nyingi siri za aina
hiyo zinakuwa ni siri za kifisadi.
Kinachoufanya
uongozi ufanye mambo kwa usiri ni pamoja na mambo kama hayo ya safari ya
Burundi iliyogharimu si chini ya shilingi milioni 23, pesa ya kuwapeleka
wajumbe wa bodi kutalii wakati ushirika wanaopaswa kuuangalia mienendo yake
ukiwa umekabwa koo na madeni.
Katika hali
ya kawaida Bodi inakuwepo ili kuhakikisha madeni ya kizembe, kama hayo ya KCU
(1990) Ltd. hayajitokezi, lakini jambo la kushangaza Bodi ya KCU (1990) Ltd.
ndiyo inayoongoza kuzalisha madeni hayo ya kizembe!
Katika
kutapatapa uongozi wa chama hicho cha ushirika ukitaka kujua ni nani anayetoa
nje kitu unachodai ni siri, lakini bila kueleza siri hiyo inamnufaishaje
mwanaushirika wa kawaida, uongozi huo unakisakama kitengo chake cha Moshi
Export kuwa ndicho kinachotoa nje siri hizo!
Ikumbukwe
kwamba kitengo hicho cha Moshi Export ambacho kimeamua kujiiendesha kwa
uadilifu wa hali ya juu, ndicho pekee kwa sasa kilichobaki kuushikilia uhai wa
ushirika huo, kikiteleza kidogo tu na kuanguka ushirika huo unazikwa kabisa.
Wanaushirika
wa KCU (1990) Ltd. wanashangazwa na juhudi zinazofanywa na uongozi wa ushirika
wao zenye makusudi ya kukiyumbisha kitengo hicho pasipo kujali kwamba juhudi
hizo ni sawa na za mtu anayehangaika kukata tawi la mti alilolikalia!
Lakini
hatahivyo uongozi huo haukijali kitu hicho, picha inayojitokeza ni ya kwamba
uongozi huo hauwajali wanaushirika waliouweka madarakani. Sababu uongozi ulio
makini ni lazima uwajali na kuwaheshimu walioupa madaraka.
Katika
kufanya hivyo, kuwajali wadau, haiwezekani pakajitokeza kitu katika uongozi
kinachoitwa siri katika utendaji wake, ambapo walioajiriwa au kuchaguliwa
kuwatendea kazi wadau wanaficha matendo yao, kikazi, yasijulikane kwa wenye
mali, waliowaajiri pamoja na kuwachagua.
Kutokana na
hali hiyo tete katika chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. baadhi ya
vyama vya msingi vimeanza kufikiria kujiondoa kwenye ushirika huo. Hizo ni
jitihada za kuwanusuru wanaushirika wake, hiyo ni baada ya kuuona uongozi wa
KCU (1990) Ltd. uliopo madarakani kwa sasa unavyokusudia kuuzika kabisa
ushirika huo mkuu hasa kwa kipindi hiki ambacho unaelekea kumaliza muda wake wa
kinachoitwa uongozi.
Kwa kuanzia,
chama cha msingi cha Magata, Muleba, Kagera, kimejiondoa rasmi kwenye ushirika
huo. Chama hicho kimeishafanya utaratibu wa kujisajili kama chama
kinachojitegemea. Kufanikiwa na kutofanikiwa
kwake
kutakuwa kumetokana na uongozi mbovu wa KCU (1990) Ltd..
Wanaushirika
wa Magata wanaeleza jinsi sekeseke lao ndani KCU (1990) Ltd. lilivyoanza. Eti
meneja mkuu, kwa utashi wake, aliamua kukipandisha hadhi chama chao cha msingi
na kukifanya kiwe cha kuuza kahawa inayotokana na kilimo cha asili, kwa maana
ya kahawa inayolimwa bila ya mbolea ya viwandani ambayo kitaalamu inaitwa “organic”.
Bei ya kahawa hiyo iko juu kuliko kahawa ya kawaida inayotokana na kilimo cha kisasa
kinachotumia mbolea ya viwandani pamoja na madawa yenye kemikali.
Lakini
hatahivyo karibu kahawa yote inayolimwa mkoa wa Kagera inatokana na kilimo cha
asili, kwa maana ya karibu kahawa yote ya Kagera kuwa “organic”.
Wanaushirika
wa Magata wanaeleza kuwa baada ya wao kudai mambo fulanifulani katika chama
chao kikuu cha ushirika, mambo ambayo ni
sehemu ya haki zao za kiushirika, meneja mkuu, yuleyule aliyekipandisha hadhi
chama chao cha msingi, akachukia na kuamua kukishusha hadhi chama hicho kwamba
kahawa yao sio organic tena, kwamba itanunuliwa kwa bei ya kawaida!
Baada ya
uamuzi huo wa meneja mkuu wanaushirika wa Magata wakajiuliza ni kigezo gani
alichokitumia meneja huyo kuipandisha hadhi kahawa yao na ni kipi amekitumia
kuishusha hadhi na kuiona ya kawaida wakati alishasema ni “organic”. Sababu
wanasema, kiutaalamu, haiwezekani
malalamiko ya kitu kingine yakabadilisha aina ya kahawa.
Kufuatia
uamuzi huo wa meneja mkuu, wanaushirika wa Magata wakagundua kuwa anachokifanya
ni kutaka kuonyesha jeuri yake na mizengwe tu, wakaanzisha malalamiko.
Malalamiko hayo yalipozidi kukua meneja huyo akatishia kukifuta uanachama chama
chao cha msingi, ingawa kwa mujibu wa taratibu za ushirika, yeye kama mwajiriwa
hiyo sio kazi yake.
Kwahiyo
swali wanalojiuliza wanaushirika wa Magata, ni la kwamba inawezekanaje meneja
mkuu, aliye mwajiriwa wao, awe na mamlaka ya kuwafuta uanachama wao
wanaomwajiri! Baada ya kuona mizengwe hiyo ya ajabu ikiendelea kukua huku
wakiwa wameshindwa kupata ushirikiano wa Mrajis Msaidizi wa mkoa, wakaamua
kukitayarisha chama chao kianze kujitegemea.
Baadaye
wakaenda kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa na kupata kibali cha chama chao
kujitegemea. Lakini baada ya kuona mambo yanawaendea vizuri wanaushirika hao
kufikia kujiondoa kabisa katika ushirika wa KCU (1990) Ltd. ndipo Mrajis
Msaidizi wa vyama vya ushiria mkoani Kagera akaanza kuingilia kati eti akitaka
kuwasuluhisha na chama kikuu cha KCU (1990) Ltd..
Mrajis huyo
Msaidizi wa mkoa haelezi ni kwa vipi meneja mkuu wa kuajiriwa, mtu asiyekuwa wa
kuchaguliwa katika mfumo wa ushirika, awe na mamlaka ya kuwaamlia wanaushirika
namna ya kujiendesha huku akiwafukuza baadhi ya wengine kutoka kwenye ushirika
wa KCU (1990) Ltd. ambao kiuhakika ni mali yao. Wanasema “omushuma naita mukama
w’engemu” kwa maana ya mwizi kumuua mwenye mali!
Nimalizie
kwa kusema kwamba chama cha msingi cha Magata kimezigundua hujuma dhidi ya
ushirika, kimetangulia kuonyesha mfano wa kukabiliana na hujuma hizo. Na
pengine huo ndio mwanzo wa mwisho wa KCU (1990) Ltd.. Kilichochangia zaidi hali
hiyo ni uongozi mbovu usioweka mbele maslahi ya wanaushirika isipokuwa kukomba
kila kinachowezekana kukombwa na baadaye kukizika kabisa chama hicho kikuu cha
ushirika KCU (1990) Ltd..
0784 989 512