URAIS 2015:MBONA HATUMUANGALII JAJI BOMANI?
Na Prudence Karugendo
Tumeingia 2014 wakati homa ya urais ndani ya vyama vya siasa,
hususan CCM, ikiwa juu.
Nimeishaandika kwamba suala hili la wagombea kujulikana mapema,
kwa uzoefu tulionao hapa nyumbani, hata katika nchi nyingi za Kiafrika, suala
hili muhimu hufanywa kwa kushtukiza, hivyo kuwanyima wananchi fursa ya kutosha
kulijadili kwa kina.
Nadiriki kusema kwamba imekuwa balaa tupu tangu uchaguzi wa
kwanza uliorejesha mfumo wa vyama vingi hapa nchini, kutokana na watu
kutojitokeza waziwazi kwa namna ambayo kweli ingemsaidia mwananchi wa kawaida
kujua hatima yake.
Hii inadhihirisha namna ambavyo wagombea wengi watarajiwa hasa
ndani ya CCM, chama ambacho kimejirithisa kwa mabavu utawala wa nchi yetu,
wasivyokuwa na sifa zinazolingana na nafasi hiyo ya juu kabisa ya utumishi wa
umma. Pia inatupa picha ya kwamba wagombea hao kupitia chama tawala
hawasukumwi na kero au shida za wananchi, bali utashi wao katika kutimiza
ndoto zao.
Angalia, imefikia mahali hata Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anazungumzia kuoteshwa ndoto, badala
ya kutamka wazi namna anavyokerwa na hali ya baadhi ya mambo ilivyo hapa
nchini. Au ni namna nyingine inayotaka kuzoeleka ya kufuata mkumbo tu, hasa
ikizingatiwa kwamba Wizara hiyo imetoa Marais wawili sasa!
Ni wazi kwamba suala la maadili ya uongozi ni mgogoro kwa
sasa. Na inaelekea kuwa ni hatari ya kutisha haswa nikikumbuka mahojiano aliyowahi
kufanyiwa Marehemu Dr. Vedastus Kyaruzi, ambaye alikuwa ni miongoni mwa
waanzilishi wa chama cha TAA na baadaye TANU. Baada ya uhuru alikuwa balozi
wetu wa kwanza Umoja wa Mataifa, na
baadaye Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ulinzi, mpaka alipojiuzulu mwaka
1963 kwa kanuni za kimaadili na kuacha kabisa kufanya kazi serikalini. Hiyo ni
tofauti na kujiuzulu kwa kuwajibika.
Hapa namnukuu Dr. Kyaruzi: “Nyerere atabaki with no match (bila wa
kumlinganisha naye). Nyerere aliogopwa na kuheshimiwa na kila mtu. Marais
waliomfuatia hawaogopwi wala kuheshimiwa. Viongozi wa sasa wanajilimbikizia
mali kwa kutumia madaraka bila woga. “… halafu wanawakejeli wananchi, walipa
kodi…(hivi ni vijisenti)! Hawana woga na sheria haiwagusi! Hapa ndipo
tulipofikia baada ya miaka 50 ya Uhuru.” Anaendelea: “Mwl. Nyerere
aliweza kuwafanya watu waogope kufanya maovu, lakini si sasa. Tunaelekea
gizani, tena giza totoro. Nadhani watu sasa wako tayari kulala na mabinti zao,
hawana woga kabisa!”
“Katika hali hii ambayo viongozi wetu hawana woga tena,
hawamwogopi tena Mungu, wana jeuri ya kuwaambia walipa kodi kuwa
(nimefuja mali sasa mnasemaje?), njia pekee iliyobaki ni mabadiliko,
yatakayoongozwa na Mungu mwenyewe.”
Kama hali halisi inavyojionyesha basi ni wajibu wa kila mmoja wetu
kufanya jitihada za makusudi ili kuzuia mapinduzi ya namna yoyote. Kwangu,
tunavyoelekea uchaguzi mkuu, kipaumbele namba moja ni maadili, namba mbili ni
maadili na namba tatu ni maadili. Hii ni tofauti na elimu kama kipaumbele cha
kwanza, cha pili na cha tatu cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Nikirejea hoja ya Dr. Kyaruzi ya watu kuwa tayari kulala na
mabinti zao, mfano hai ni kitendo cha aliyekuwa Waziri awamu ya Mkapa na
Kikwete, Alhaji Prof. Juma Kapuya, kutuhumiwa kubaka msichana ambaye
pengine angeweza kuwa hata mjukuu wake!
Sina budi kusisitiza kuwa hili suala la maadili halina chama kwa
namna lilivyo muhimu kulitekeleza.
Tunakumbuka waliowahi kugombea nafasi hiyo kupitia upinzani jinsi
suala la maadili lilivyowasumbua na kuwapunguzia imani wananchi kwa kiasi fulani.
Baada ya kuonyesha jinsi gani maadili yalivyoporomoka nchini
katika uongozi wa nchi, sasa niende moja kwa moja kumzungumzia mtu ambaye
naamini anaweza kurejesha maadili ya uongozi na hivyo kulirejeshea taifa
heshima yake ndani na nje ya mipaka yake. Huyu si mwingine bali ni Jaji Mark
Bomani.
Hapa namwangalia mtu anayefaa kuwa rais wetu, kwahiyo msukumo
nilio nao ni wa kiuzalendo zaidi, usiofungamana na itikadi ya chama chochote cha
siasa. Najua wapo wengine kama huyu, wasiokuwa na tamaa ya nafasi hiyo adhimu
lakini wakiwa na uwezo nayo. Kuwataja na kuwajadili kwa manufaa ya nchi yetu
naamini sio dhambi. Aliye na jina lingine, mbali na waliokwisha tajwa, na
alilete tulijadili.
Leo nitajikita kumzungumzia Jaji. Kwa kweli hadithi ya Jaji Bomani
ni ndefu, kitaifa na kimataifa, na ni ya kutukuka. Ila havumi vizuri kwa
mazingira yenye mizengwe ya CCM.
Hivi karibuni, kwenye mahojiano na gazeti moja la kila wiki
kufuatia kifo cha Madiba, alionyesha kuyatambua kabisa matatizo yetu ya msingi
kiasi cha kutia moyo.
Mwandishi alimuuliza; “Unadhani, inaweza kuichukua muda gani
Afrika kupata viongozi wa aina ya Mwalimu na Madiba?” Alijibu;
“Unajua, viongozi wa aina ya Mwalimu na Mandela hawategemei kizazi. Tunao
hata leo, lakini hawapewi nafasi ya kuonekana na kutambuliwa na jamii,
wanafanyiwa mizengwe. Wapo wanaojitokeza kwa kusaka sifa kwa madhumuni yao
binafsi, na si kwa ajili ya kuwatumikia watu wao. Lakini wapo wachache
wanajitokeza kwa sababu ya kuona uchungu wa maisha ya watu wao. Tunao lakini hawapati
nafasi!”
Nadiriki kutamka kuwa Jaji Bomani anajizungumzia na yeye pia,
maana aliwahi kugombea Urais 1995. Ni bahati mbaya kwamba Mwl. Nyerere
alimwamini Mkapa kuwa angeweza kusimamia maadili kikamilifu kuliko
wagombea wengine wote.
Ukiacha suala hilo la Urais, Mwl. Nyerere alimwamini Jaji Bomani
kiasi cha kumuomba awe msaidizi mkuu wa usuluhishi wa mgogoro wa Burundi, na
kufuatia kifo cha Mwalimu, Mandela, aliyechukua nafasi ya Mwalimu kwenye suala
hilo, alimuomba kuendelea na nafasi hiyo mpaka mwisho. Si jambo la
kubahatisha kufanya kazi na mashujaa hao wawili wa Afrika.
Alilinda heshima ya taifa letu kikamilifu.
Tukirejea ndani ya nchi, niliwahi kuandika mwaka jana kuwa ni
jambo la kushangaza kidogo kwamba kwenye eneo alilobobea, haswa la sheria na
mambo ya katiba, ingetarajiwa kuwa angetumika katika Tume ya Katiba. Katika
kuonyesha sababu, hivi karibuni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
pale Maelezo, bila woga aliwaonya CCM kutoingilia maamuzi ya wananchi juu ya
Muungano wanaopendelea na vile vile kwamba yuko tayari ‘kufafanua mawazo yake
mbele ya chombo chochote, kiwe kikao cha CCM au kamati yoyote ya Bunge la
Katiba’. Huyu ni mtu anayeheshimu kanuni ya demokrasia na anaonyesha njia
sahihi ya kusonga mbele.
Na haishangazi kwamba
kufuatia mkutano wake huo, mwandishi Aidan Mhando, alitamka: "mimi
nimeguswa na maneno ya Jaji Bomani ambaye naweza kusema ni kiongozi shupavu
aliyeamua na kuthubutu kutoa ya moyoni kwa masilahi ya taifa."
Tunapoelekea kupata Katiba Mpya, ni vyema pia kunukuu maneno ya
msomi mahiri wa siasa kutoka Afrika ya Kusini, Tom Lodge, anaposema: “ In
new democracies the quality of political leadership matters more than in
established political systems, however carefully scripted the constitutional
safeguards may be against the abuse of power. Institutions are still fluid and
susceptible to being shaped by dominant personalities.”
Tafsiri isiyo rasmi: “ Katika demokrasia changa ubora wa uongozi
wa kisiasa una uzito mkubwa kuliko ndani ya mifumo iliyojengeka kisiasa,
pamoja na uangalifu wa hali ya juu wa Kikatiba kudhibiti matumizi mabaya ya
madaraka. Taasisi nyingi bado hazijakomaa na hivyo kukabiliwa na uwezekano wa
kufuata matakwa ya watu fulani.”
Hii inazidi kuniongezea sababu za kuamini nchi inamhitaji mtu
wa aina ya Jaji Bomani. Vilevile naamini atakuwa tayari kuondoa usiri wa mali
za viongozi, tatizo ambalo ni kilio cha muda mrefu kwa kuonyesha kwa vitendo,
maana hata ndani rasimu ya Katiba Mpya, ni suala lililopewa uzito
unaostahili.
Pengine kwa haraka niongeze kuwa viongozi wetu wengi hawana maisha
yanayoeleweka nje ya siasa. Hii inawapa wananchi wakati mgumu kuhusiana na
namna wanavyopata mali zao. Na matokeo yake ni nani wa kumfunga paka kengele.
Watanzania tunafahamu namna viongozi wetu wanavyojihusisha na njia
zisizofaa katika kuchuma mali. Mfano ni suala la biashara ya madawa ya kulevya
ndani ya Bunge letu tukufu. Sifa ya wazi kumhusu Jaji Bomani ni kwamba chanzo
cha mapato yake kinaeleweka, maana ni wakili wa kujitegemea, pamoja na mambo
mengine anayoyafanya kimataifa.
Kuhitimisha kwa uchache tu kuhusu Jaji Bomani, ni vyema kurejea
tena mahojiano yake na gazeti moja la kila wiki. Swali zuri sana aliloulizwa
mwishoni mwa mahojiano hayo ni: “Mandela ameondoka, Mwalimu Nyerere
ameshatutoka. Una lipi la kuwaambia Watanzania kuhusu Mandela na kuhusu sisi
Watanzania kama taifa?”
Alijibu, pamoja na mambo mengine kuhusu Tanzania; “Kwa
Tanzania na sisi Watanzania kama taifa, ni kwamba Tanzania lilikuwa ni taifa
linaloheshimika duniani kwa namna tulivyojitolea na kuwa kimbilio la wanyonge
na watu waliokumbwa na madhila katika nchi zao.”
“Heshima ile hatunayo tena. Leo tunaadhimisha miaka 52 ya Uhuru wa
nchi hii, lakini bado tunao baadhi ya wananchi wetu ambao Uhuru huu
uliwakuta wakiwa ndani ya nyumba za nyasi na udongo, leo baada ya miaka 52
wanaishi kwenye nyumba za aina ileile! Nini maana ya Uhuru kwa wananchi hawa?”
Anaendelea kusema; “Mimi nilidhani uhuru huu ungetuletea
mabadiliko ya kimaendeleo katika maisha ya wananchi wetu…”
Kauli zake zinaweka wazi msimamo wake juu ya usimamizi na matumizi
sahihi ya rasilimali za nchi kwa maendeleo na ustawi wa watu wake na
hususan vita dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Nihitimishe kwa kusema, Tanzania mpya bila kiongozi atakayesimamia
maadili kikamilifu ni sawa na safari ndefu iliyojaa kila aina ya bugudha. Jaji
Bomani unaijua njia ya safari yetu barabara, jaribu kutuepusha na hatari ya
Mapinduzi!
0784 989 512