WAHAYA NA ZAHAMA KWA KINAMAMA
Na
Prudence Karugendo
WAHAYA ni kabila maarufu linalopatikana kwenye eneo
la Bukoba katika mkoa wa Kagera, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Kabila hilo
ni moja ya makabila yaliyowahi kustaarabika na kuendelea, kielimu na kiuchumi,
tangu enzi za wakoloni wakati nchi hiyo ikijulikana kama Tanganyika, kabla ya kuungana na Zanzibar na kuwa
Tanzania.
Kutokana na
kabila hilo kuwa miongoni mwa makabila yaliyotangulia kupata elimu nchini
Tanganyika, Wahaya wakaanzisha usemi wa kiutani, kwa lugha yao ya Kihaya,
wakisema “inye nshomile” wenye maana ya kwamba “mimi nimesoma” yaani nimeenda
shule na ninaelewa mambo mengi. Na huo ndio ukawa mwanzo wa makabila mengine ya
Tanzania kuanza kuwatania Wahaya kwa kuwaita kina NSHOMILE.
Lakini
pamoja na kabila hilo la Kihaya kuonekana limeelimika ukweli ni kwamba bado
limeukumbatia ukandamizaji wa kijinsia wa tangu enzi na enzi, kina mama wakiwa
ndio walengwa wakuu wa ukandamizaji huo. Ingawa tunaweza kusema kwamba kwa sasa
ukandamizaji huo umepungua kwa kiasi fulani, lakini bado unaendelea katika
baadhi ya maeneo, hasa sehemu za vijijini, kutokana na kujifunga zaidi katika
utamaduni wa kabila hilo.
Mpaka sasa
katika mila za Kihaya ni vigumu kuwalinganisha mwanamume na mwanamke kama
binadamu walio sawa. Na inapotokea mwanamume wa Kihaya akataka kujiweka sawa na
mkewe kunajitokeza mambo mawili. Jamii nzima ya Kihaya itamshangaa mwanamume
huyo, tena ikimlaumu kwa desturi hiyo, inayoonekana kuupotosha utamaduni wake, au la
pili itamuona mke wa mwanamume huyo kama mchawi aliyemroga mume wake mpaka
akajisahau na kuanza kufanya mambo kinyume na utamaduni wake bila yeye kujielewa.
Kama ilivyo
ada kwa kila kabila hapa duniani, kuoana, mwanamume na mwanamke kuchukuana
kwenda kuishi pamoja na kuanzisha familia yao, ni jambo la kawaida na
lisiloepukika. Lakini jambo hilo inafaa litokane na makubaliano ya pande zote
mbili.
Lakini
katika mila za Kihaya sio lazima makubaliano hayo yawepo. Kipo kitu kinaitwa “okuleya”
ambapo kijana au mwanaume anaweza akamuona msichana akamtamani, bila msichana
kumfahamu kijana au mwanaume husika, mwanaume au kijana akaanza kufanya mipango
ya kumteka nyara msichana husika ili akamchukue kuwa mke wake! Jambo hilo
halina maelewano wala makubaliano, ila limehalalishwa kiutamaduni!
Wataandaliwa
vijana wenye mabavu na kumvizia popote msichana mlengwa na kumkwapua kwa nguvu,
huku wakimpa vipigo kama analeta ukaidi, kisha wanampeleka kwa yule anayetaka
kumuoa. Kesho yake asubuhi na mapema anatumwa mtu, mtu mzima, nyumbani kwao na
msichana aliyechukuliwa, kwenda kutoa habari
kwamba mtoto wao wasimtafute kwingine, yuko salama kaolewa na mtu fulani.
Badala ya
wazazi wa msichana kuja juu watanywea, ikiwa ni alama ya kuhalalisha kitendo
hicho cha kibabe na chenye kukiuka haki, ila watataka kiasi fulani cha pesa
kitolewe kama faini ya kufanya kitendo hicho. Na kwa upande wa mwanaume,
watenda kosa, faini hiyo inakuwa imeishaandaliwa tayari.
Katika
makala hii nitatoa mifano miwili ya unyama wa aina hiyo nilioushuhudia
mwenyewe.
Mfano wa
kwanza unamhusu dada yangu mwenyewe. Ilikuwa sikukuu ya Pasaka, jioni baada ya
kutoka matembezini dada akabadilisha nguo na kuingia jikoni kuanza maandalizi
ya chakula cha usiku. Mara wakaja Vijana wanne wanajifanya kuulizia kitu fulani.
Dada alipotoka nje ili awasikilize vizuri wakamdaka na kumfunika na makhanga na
kumbeba juujuu. Mdogo wangu wa kiume alipojaribu kumsaidia dada yake akapigwa
vibaya mno!
Kama kawaida
kesho yake asubuhi akatumwa mtu kuja kutoa taarifa nyumbani kwetu akiwa
ametayarisha faini tayari, na faini ikakubaliwa kama ishara ya kuhalalisha
kitendo hicho haramu! Dada yangu akawa ameolewa kwa mtindo huo.
Ushuhuda
mwingine ni wa binti ambaye hakuwa kwenye mpango wa kutekwa nyara ila alijikuta
anaagukia huko katika kutaka kumnusuru dada yake!
Dada yake
alikuwa na kijana ambaye alikuwa rafiki yake. Kijana akataka kutumia njia ya
mkato kuoa badala ya kusubiri taratibu za kuchumbia, ndipo kijana akatangaza
kijijini kwetu kwamba siku fulani anamleta mke. Kumbe habari hizo zikamfikia hata
yule binti aliyekuwa rafiki yake.
Siku ya siku
kijana akaenda, alipofika sehemu waliyozoea kukutana na rafiki yake huyo wa
kike, kijana akiwa ameambatana na vijana marafiki zake kwa ajili ya shughuli ya
kumbeba msichana, yule msichana mlengwa hakuonekana. Badala yake akaja mdogo
wake kuwaeleza wale vija, kama kuwakoga, kuwa dada yake hayupo katumwa sehemu
ya mbali kidogo. Alipowakaribia, bila
yeye kuwa wasiwasi wowote, wakambeba yeye na kumuingiza kwenye gari na kuondoka
naye!
Kwahiyo
ikabidi aolewe mdogo mtu, ambaye hakuwa kwenye mpango na wala hakuwa na urafiki
wowote na yule kijana zaidi ya kuonekana kama shemeji, aliyekuwa abebwe
akanusurika na mpaka sasa ndiye shemeji!
Tukiacha
ukandamizaji huo ambapo wanawake wanaonekana kuporwa haki zao za kujifanyia maamuzi
katika mahusiano, yapo mambo mengine ya muhimu na ya lazima kuyatekeleza kwa
mwanamke wa Kihaya aliyeolewa, ingawa mambo yenyewe yanaweza yakafanywa na
jinsia zote mbili, yaani mwanamke na mwanamume.
Mambo hayo
ni pamoja na kilimo cha musimu. Mwanamke analazimika kupanda maharage na
mahindi punje mojamoja, tena kwa mkono, kwenye shamba ambalo wakati mwingine
linaweza kuwa na ukubwa wa ekari kumi na zaidi.
Wanalazimika kupanda kwa mkono kutokana na mashamba yenyewe yalivyo. Ni
mashamba ya kilimo mseto “mixed farming” ambako haiwezekani kutumika kifaa
kingine chochote kurahisisha upandaji huo.
Hiyo ni kazi
ya mwanamke peke yake ambapo tamaduni za Kihaya zinamzuia mwanamume kujihusisha
na kazi hiyo hata kama ana hamu ya kumsaidia mkewe.
Mbali na
hiyo mwanamke wa Kihaya anapaswa kuwa na mashamba ya kilimo kingine cha musimu,
mashamba ya njugumawe na karanga, mazao ambayo kawaida hulimwa mbugani au
maporini, nje kabisa ya makazi ya watu. Inaweza ikawa hata umbari wa kilometa
10 na zaidi ambako mwanamke inambidi aende kila siku, kwa mguu, kwa karibu
mwezi mzina na zaidi kuyahudumia mazao hayo.
Mwanamke
asipolima mazao hao inaweza ikawa ishara ya kuharibu na kuvunja ndoa yake,
sababu itaonekana hamjali mume wake kwa kutomlimia mazao hayo ya musimu. Na kwa
tamaduni za Kihaya uko ni kukiuka majukumu ya mwanamke aliye kwenye ndoa.
Ikumbukwe kwamba mnufaika mkubwa wa mazao hayo ni mwanamume, ingawa karibu mara
zote hajihusishi na kilimo cha mazao hayo.
Mazao hayo
yanapokomaa, yakavunwa na kutayarishwa kupikwa kwa mara ya kwanza ni lazima
yapikwe rasmi kwa ajili ya mwanamume ikiwa ni sehemu ya kumuonjesha jasho la
mke wake. Vinginevyo itakuwa ni vurumai tupu ndani ya nyumba.
Pamoja na
ukweli kwamba anayehudumia mazao hayo mwazo hadi mwisho ni mwanamke kiasi cha
mazao hayo kuonekana ni mali yake, umiliki wake huo unaishia shambani tu. Mazao
yakishavunwa na kuletwa ndani umiliki unageuka, yanakuwa ni mali ya mwanamume!
Kitu kingine
kinacholeta sekeseke kwa wanawake wa Kihaya walio kwenye ndoa ni musimu wa
senene. Senene ni wadudu jamii ya panzi wanaotokea mara mbili kwa mwaka, mwezi wa
nne, Aprili, na mwishoni mwa mwaka. Wadudu hao waligeuzwa kuwa chakula cha
heshima cha Wahaya tangu zamani.
Katika miaka
ya nyuma ilikuwa ni mwiko kabisa wadudu hao kuliwa na wanawake, kama ilivyokuwa
kwa karibu vitu vyote vitamu ambavyo vilikuwa halali kwa wanaume tu. Isipokuwa
kazi ya wanawake ilikuwa ni kuwatafuta wadudu hao kwa ajili ya waume zao tu,
kuanzia usiku wa manane kila musimu wake ukifika.
Inagawa kwa
sasa baadhi ya wanawake wa Kihaya wanawala senene, lakini ulazima wa kuwatafuta
na kuwakamata umebaki ni kwa ajili ya wanaume tu. Na kwa mwanamke asiyefanya
hivyo aelewe anahatarisha ndoa yake.
Hayo na
mengine ambayo sikuyataja yanajionyesha kabisa jinsi yalivyowaweka wanawake wa
Kihaya majaribuni kwa kuwapokonya haki zao za kiubinadamu.
Hivyo pamoja
na Wahaya kujiita NSHOMILE hicho bado ni kitu kinachowapita pembeni pasipo
kuuangalia ukubwa wa madhara yake yanayoweza kujitokeza iwapo hawakuufanyia
marekebisho utamaduni wao.
Sababu mpaka
sasa bado ni jambo la kawaida kuwasikia wazazi wa Kihaya wakimhimiza kijana wao
ili aoe apate mtu wa kumsaidia kazi,
hasa za kulima mashamba, kana kwamba kuoa ni sawa na kununua trekta!
Nimalizie
kwa kusema kwamba mtazamo huo batili katika utamaduni wa Kihaya usipofanyiwa
marekebisho, kuendelea kujiona au kujiita NSHOMILE kutakuwa ni batili pia.
0784 989 512