Sumaye Akata rufaa kwa kutoridhishwa na uamuzi wa kumfungia mwaka mmoja CCM
Dodoma. Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amekata rufaa
Kamati Kuu ya CCM kupinga adhabu ya onyo kali aliyopewa na chama
kutokana na madai ya kuanza kampeni za urais mapema kwa ajili ya
Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza na gazeti hili mjini Dodoma jana,
Sumaye alisema kwa ufupi hakuridhishwa na adhabu hiyo na kuthibitisha
hilo, tayari amekata rufaa.
Hata hivyo, alisema hadi jana hakuwa amepata
mrejesho wowote kwa sababu kanuni hazielezi ni muda gani anatakiwa kuwa
amepewa taarifa kuhusu rufaa hiyo.
Sumaye na wanachama wenzake, Edward Lowassa,
Bernard Membe, Stephen Wassira, William Ngeleja na January Makamba
walitiwa hatiani kwa kuanza kampeni mapema, hivyo kupewa onyo
linalokwenda sambamba na kutowania nafasi yoyote ndani ya chama kwa
miezi 12.
“Siwezi kuwazungumzia wenzangu, nazungumza kwa
upande wangu, sikuridhishwa na adhabu hii na nimeshakata rufaa ingawa
sijapata majibu yoyote, naendelea kusubiri,” alieleza Sumaye.
Waziri Sumaye alikataa kuzungumzia hali ya
utekelezaji wa adhabu hiyo, akisema anachosubiri ni mwitiko wa rufaa
yake aliyoiwasilisha Kamati Kuu ya CCM, mwanzoni mwa mwezi huu. “Sina
kumbukumbu nzuri ilikuwa tarehe ngapi, lakini ni mwezi huu wa tatu.”
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alipoulizwa juu ya rufaa hiyo alisema hana taarifa zaidi ya habari hizo
kuzisikia kutoka kwa mwandishi.
Hata alipotakiwa kueleza nani anatakiwa kuwa na
taarifa hizo, alisema: “Mimi ndiye msemaji wa chama, hakuna wa
kuzungumzia suala hili zaidi yangu. Kwanza inatakiwa ijulikane, rufaa
hiyo imepelekwa ngazi gani ya uongozi kwa sababu kila ngazi ina muda
tofauti wa kufanya vikao vyake vya uamuzi.”
Nnauye baada ya kuelezwa kuwa rufaa ya Sumaye
imewasilishwa Kamati Kuu ya CCM, alisisitiza kuwa hana taarifa nayo na
kwamba haiwezekani rufaa ipelekwe kwenye kikao kilichotoa adhabu husika.
Hata hivyo, Sumaye alisisitiza kuwa rufaa yake ameiwasilisha Kamati Kuu kwa mujibu wa kanuni zinazohusika.
MWANANCHI
MWANANCHI