Bukobawadau

CHOZI LA SENDEKA NI LA KIUZALENDO AU LA MAMBA?

Na Prudence Karugendo
CHRISTOPHER ole Sendeka ni mmoja wa wabunge niliokuwa nikiwaona na kuwaamini kuwa wametawaliwa na uzalendo. Hilo,  pamoja na hulka ya watu wa kabila lake, Wamaasai, ya kutokuwa wanafiki, wakiwa wanaipenda na kuiheshimu haki pamoja na kuwa waaminifu, vilinifanya nimpende na kumheshimu mbunge huyo.
Lakini  sasa mambo yanayoendelea kwa wakati huu nchini mwetu yananifanya niukumbuke usemi wa Kiswahili wa kwamba usimcheke mamba kabla hujavuka mto. Nyakati zina mambo,  Sendeka anaonekana kabadilika!
Kwa wakati huu ambao kila mwananchi anahitajika kuonyesha uzalendo wa kweli kwa nchi yake tunapotafuta Katiba ya nchi, katiba isiyokuwa ya kichama, kikabila, kidini wala kikundi kingine chochote chenye malengo binafsi, Sendeka anaonekana  kuvutia upande wa kundi fulani analolipenda yeye akiwa amejitenga na Watanzania wote katika ujumla wao!
Katika michango yake inayoonyeshwa moja kwa moja na vyombo vya habari, Tv na redio, toka kwenye ukumbi wa Bunge, Dodoma,  Sendeka anaonekana anavyohaha kuhakikisha Katiba mpya inayotayarishwa haikumbatii matakwa ya wananchi katika ujumla wao, isipokuwa matakwa ya kikundi kidogo ambacho ni chama tawala, CCM!
Ni katika harakati hizo za Sendeka kutaka Katiba ya nchi iegemee kwenye kundi lake, ilipoandikwa kwenye vyombo vya habari kwamba mbunge huyo alimwaga machozi ndani ya kikao cha wabunge wa CCM akiwataka wabunge hao wa chama chake wakubaliane kutumia wingi wao kulazimisha kura ya wazi katika kuamua ni kitu gani kiingizwe katika Katiba na kipi kiachwe! Ni hilo linalonifanya nijiulize, machozi hayo ya Sendeka ni ya kiuzalendo au ni ya mamba?
Sababu kawaida ukali wa mamba unakuwa majini, nje ya maji mamba si mjanja sana. Anaweza akakiangalia kitu akitamani kiingie majini ili iwe nafuu kwake, isipotokea hivyo anaanza kutoa machozi. Ila machozi hayo sio kwamba anakionea huruma kitu hicho, ni machozi ya kusikitika kukikosa. Hayo ni machozi ya hatari. Je, Sendeka naye anataka tumuamini hivyo?
Ieleweke kwamba wajumbe wote wanaounda Bunge Maalumu kwa sasa majina yao wote yatabaki kwenye historia ya nchi yetu, kwa heshima au kwa kudharauliwa. Iwapo wataifanyia nchi yao kitu cha maana, kwa maana ya kuiandikia katiba nzuri kwa manufaa ya wananchi wote bila mizengwe, sio kwamba ni sisi tu tulio hai kwa wakati huu tutakaowaheshimu peke yetu, bali hata vizazi vijavyo. Lakini iwapo watafanya kitu cha ovyo, wakatoa katiba isiyotamanika, watadharauliwa mpaka mizimu yao na vizazi vijavyo.
Kwahiyo mtu anapotaka kujitengenezea heshima yake binafsi itakayoonekana hata kwa vizazi vijavyo, heshima isiyosahaulika kutokana na kutumia nafasi yake adimu ya wakati huu kuvitendea haki vizazi vijavyo miaka mingi mbele, kwa nini alazimishwe kufanya maamuzi kimkumbo kwa lengo la kuwanufaisha tu wanaojali faida ya sasa peke yake bila kujali kama kuna kesho?
Ni lazima kura ya wazi imekilenga kitu hicho tofauti na kura ya siri inayomfanya mtu atafakari kwanza kwa kuangalia miaka mingi mbele kabla ya kufanya uamuzi. Kura ya siri inajali leo na kesho, haiangalii mkumbo wa leo tu.
Kwahiyo mpaka sasa bado sijaelewa ni uchungu gani uliomminya Sendeka mpaka mwanamume mzima akamwaga machozi mbele ya wenzake. Hivi ni shabiki sana wa serikali mbili kiasi cha kuhisi kwamba kura ya siri itawafanya hata walio wana CCM wapigie kura serikali tatu kama ilivyopendekezwa kwenye Rasimu, kinyume na msimamo wa chama chake? Je, anadhani zikiwa serikali tatu atapoteza uhai?  Tuseme anaichukia Tanganyika au pengine  ni hofu tu ya kukikosa alichokuwa akinufaika nacho, au anachotaka kunufaika nacho binafsi,  katika serikali mbili?
Na kama ana mtazamo huo, mtazamo wa maslahi binafsi, huyo tunawezaje kumwita mzalendo wa kweli? Na kwa nini tumwamini na kumuachia nafasi ya kutuamria mstakabali wa nchi yetu mtu wa aina hiyo?
Sababu mzalendo wa kweli ni yule anayefanya mambo akiwa ametanguliza maslahi ya nchi yake na ya watu wake mpaka na ya vizazi vijavyo, mtu aliye tayari kuifia nchi yake akiwa hayaangalii hata kidogo maslahi yake binafsi.
Huwezi kusema kwamba mtu aliye tayari kuifia nchi yake anayajari maslahi yake binafsi, maana akishakufa ndio unakuwa mwisho wa maslahi binafsi. Mtu wa aina hiyo anafanya hivyo kwa kuyaangalia tu maslahi ya umma. Huyo ndiye mzalendo.
Kitendo cha mtu mzima kulia akishinikiza matakwa yake yaende kinyume na mapendekezo ya umma hakiwezi kuwa cha uzalendo hata kidogo. Uzalendo ni lazima uheshimu matakwa ya umma.
Kwa ufupi,  kitendo hicho cha Sendeka naweza kukiangalia sawa na mtu anayemkatia mwanae bima ya maisha halafu akafanya mbinu kusudi mwanae afe ili yeye akapate pesa ya bima! Hivyo ikitokea mtoto akaugua halafu akapona baadaye mzazi akaanza kulia ni nani anaweza kuitafsiri siri ya kilio hicho cha mzazi? Inaweza kuonekana anasukumwa na huruma kumlilia mwanae, lakini kiukweli hayo ndiyo machozi ya mamba. Machozi ya kukosa.
Tunaweza kuitumia Marekani kama mfano wa nchi kutofanya mambo kimkumbo, watu kufanya mambo na maamuzi kwa manufaa halisi ya nchi na vizazi vyake, kizazi kilichopo na kijacho.
Katiba ya Marekani inayotumika mpaka sasa iliandikwa na watu wasiozidi 10 wakipata ushauri toka kwa watu wasiozidi 63, mwaka 1787, na katiba hiyo kuanza kutumika mwaka 1788. Mpaka leo katiba hiyo ina umri wa miaka 226. Katika kipindi chote hicho yalipendekezwa marekebisho 33 lakini yakaridhiwa 27 tu.
Hiyo maana yake ni kwamba watu wote wa Marekani waliopata nafasi ya kuwa viongozi, katika kipindi chote hicho,  walifanya kazi ya uongozi bila  kutanguliza maslahi binafsi, waliangalia maslahi ya watu wote wa Marekani. Bila hivyo Katiba yao ingekuwa inabadilishwa kila mara kulingana na matakwa ya viongozi waliopo kwa wakati huo. Nadhani wangekuwa na mtu sampuli ya Sendeka angetengeneza bahari ya machozi!
Hapa jambo la kujiuliza ni kwamba pamoja na uchanga wetu na nchi yetu, hivi kweli tunaamini kwamba Wamarekani wanatuzidi akili kwa kiasi chote hicho? Yaani akili walizokuwa nazo Wamarekani mwaka 1787 hatujaweza kuzifikia hata baada ya miaka 226! Hata uzalendo waliokuwa nao kwa nchi yao bado sisi unatushinda!
Fikiria watu wasiozidi 10, mwaka 1787 walitayarisha utaratibu wa kuiendesha nchi yao milele yote, wakati sisi, zaidi ya watu 600,  bado hawaonyeshi dalili za kutengeneza utaratibu tunaoweza kuutumia walau kwa miaka 50 tu!
Wengi wanaopata nafasi za kutengeneza utaratibu wa kuiongoza nchi yetu wanatumia nafasi hizo kuangalia ni namna gani watajinufaisha nazo,  kama anavyojaribu kufanya Ole Sendeka!
Kwa upande mwingine nimemsikia mjumbe mmojawapo wa Bunge Maalumu akidai kwamba Katiba ya Marekani haikupata maoni ya wananchi. Nasema pamoja na mtu huyo, tena msomi, kuwa katika nafasi hiyo adhimu,  wazo lake hilo ni potofu. Marekani,  kama tunavyoifahamu,  itakosaje Katiba yenye maoni ya wananchi halafu  Katiba hiyo idumu kwa miaka 226? Na inawezekanaje Katiba isiyokuwa na maoni ya wananchi iliwezeshe taifa kuwa na mafanikio ya kutugeuza sisi wengine ombaomba wao wa kudumu?
Na je, kama kweli sisi tunayajali maoni ya wananchi  mbona maoni ya Watanzania yanayosema serikali tatu yanapigwa vita na chama tawala?  Hayo maoni ya wananchi ni ya nini yasiyotakiwa kuheshimiwa na chama tawala?
Mimi naamini kwamba wale Wamarekani 10 waliweka umimi pembeni na kuvaa roho za Wamarekani wote, waliokuwepo wakati huo mpaka waliopo sasa hivi, wakaamua kufanya kazi hiyo, tena kwa kujitolea. Hao ni tofauti na hawa wa kwetu zaidi ya 600 ambao kipaumbele chao kilikuwa ni kuongezewa posho kwanza pamoja na ukweli kwamba wanazopata ni kufuru tupu!
Zipo dalili za wazi kwamba mtindo wa kuendesha au kupitisha  mambo yanayowahusu wananchi na nchi kimkumbo  ndio unaoweza kutumika hapa kufikia  kuipitisha  Katiba Mpya. Mtindo huo unaoegemea kwenye wingi wa uwakilishi, unaweza kuwafanya baadhi ya wawakilishi wetu wafanye maamuzi kimkumbo wakiyaangalia  maslahi binafsi kwa muda uliopo tu!
Pengine ndiyo maana tunaona muda wa Bunge Maalumu unacheleweshwa makusudi bila yeyote kutilia maanani kuwa Watanzania wanatakiwa wamlipe kila mjumbe kiasi kisichopungua laki tatu kila siku! Hata hivyo wajumbe hao wanaona kiasi hicho bado ni kidogo,   walitaka,  na bado wengine wanataka, kiongezwe! Sababu wao wanaonekana wamepata fursa ya kuvuna, mambo ya Katiba Mpya ni mengineyo!
Wajumbe wa Bunge hili maalumu wametoka kwenye vyama vya siasa na makundi mengine mbalimbali, ila wote walishauriwa kuuvua ukada wa vyama vyao na umakundi na badala yake kuuvaa uzalendo.  Sasa haya yanayosemwa ya sera na itikadi za vyama yanatoka wapi? Mimi naamini kwamba wajumbe wote wa Bunge Maalumu ni wananchi wazalendo, au wanaopaswa kuwa wazalendo, hivyo tutengeneze Katiba yetu kwanza, sera na itikadi vije  baadaye.
0784 989 512 
Next Post Previous Post
Bukobawadau