JK anakubali kuiacha Tanzania kwenye maangamizi!
Na Prudence Karugendo
MHESHIMIWA Jakaya Mrisho Kikwete ni mtu mwema sana. Ndiyo
maana alipotangazwa kuwa rais wa nchi yetu kwa mara ya kwanza wananchi karibu
wote walishangilia, wa chama chake, CCM, na wa vyama vingine vya upinzani.
Ila sina
uhakika kama wote walioshangilia ushindi wake walimwelewa kiundani, inawezekana
wengine walisukumwa na muonekano wake kuushangilia ushindi huo wakiamini kwamba
wamepata rais bora. Tuliobahatika kumwelewa kwa karibu ndio tulioshangilia
tukikielewa tunachokishangilia. Nitajaribu kueleza.
Tangu kabla
ya JK kuwa rais alionyesha utu na wema ambao ni nadra sana kuonyeshwa na kila
mtu. Mfano, alionyesha kuwajali wafanyakazi wenzake waliokuwa chini yake, pale
alipokuwa waziri, akiwahangaikia kuliko hata ndugu zao wa damu pale walipokuwa
wanapatwa na matatizo yaliyo kwenye uwezo wake wa kuyatatua. Jambo hilo
lilikuwa halifanywi na kila mtu wa hadhi yake.
Hata baada
ya kuwa rais tunaona Kikwete aliyoendelea kuyafanya katika kuonyesha ukaribu
wake kwa jamii anayoingoza. Kuwajulia hali walio kwenye matatizo, wanaoumwa,
kuwahani waliofiwa na hata mwenyewe kushiriki mazishi, wakati mwingine, katika
sehemu mbalimbali, akiwa rais wa nchi, bila kujali umaarufu wa aliyekufa ukoje
katika jamii. Pia katika furaha, anajichanganya na wanajamii kufurahi nao
pasipo kujali uwiano wao katika jamii.
Kwakweli
hilo ni jambo la kushangaza na kujivunia, kuwa na rais wa aina hiyo. Rais
asiyeinyanyapaa jamii anayoiongoza, rais wa watu anayejihisi ni mmoja wa watu
hao. Kwakweli hicho ni kipaji chake ambacho hatunabudi kumsifia nacho. Sio
marais wote wenye kipaji cha aina hiyo.
Nikishamwangalia
hivyo rais wetu, yapo mengine yanayotatanisha sana, ambayo ndiyo yamenisukuma
kuandika makala hii. Mambo yanayoonyesha kana kwamba KJ anao mpango wa kuiacha
nchi hii katika maangamizi pale atakapoondoka madarakani katika kipindi cha
mwaka mmoja na nusu kijacho.
Ikumbukwe
kwamba Tanzania ni nchi iliyokuwa imezoea amani na utulivu, kiasi cha
kuichukulia hali hiyo kama mali yake ya urithi. Nchi ambayo wananchi walizoea
kuhitilafiana bila kukosana, kugombea bila kugombana, kuchukizana bila
kuchukiana, kupoteza bila kupoteana nakadhalika nakadhalika.
Mlezi wa
kwanza wa hali hiyo, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, katika kuikomaza
hali hiyo ya amani na utulivu, akaamua kuachia madaraka kwa hiari yake, bila
kubanwa na Katiba ya nchi wala kitu kingine chochote, huku wananchi wakiwa bado
wanampenda sana na yeye akiwa bado anazo nguvu zake kamili, akisema kwamba naye
anataka amuone kiongozi wake.
Nyerere
alikuwa haijui hali hiyo ya kuongozwa sababu tangu tunapata uhuru yeye alikuwa
kiongozi.
Pamoja na
mambo mengine aliyowahi kuyasema Mwalimu, kama yale ya cheo ni dhamana, pia
alitaka kuonyesha kwamba uongozi unaweza ukabadilishwa toka kwa mmoja kwenda
kwa mwingine bila chuki wala fujo.
Wakati
Mwalimu anaachia madaraka alikuwa na umri wa miaka 63 tu. Lakini katika nchi
nyingine wapo vikongwe wa miaka 90 na
bado wanatamani kuendelea kugombea wakijiona bado wana nguvu sana!
Nyerere
aliiacha nchi katika amani na utulivu. Watu walikuwa wanagombea nafasi
mbalimbali za uongozi kwa kushindanisha hoja. Hapakuwepo vitisho wala
vishawishi vingine tunavyoweza kuviita rushwa.
Sasahivi
hali hiyo imetoweka. Ushindani wa kisiasa umekuwa kama vita, au niseme ni vita
kamili. Sababu vita ni mapambano yanayosababisha vifo. Mara nyingi tunaona
jinsi chaguzi za wakati huu zinavyoambatana na vifo, kutekana, kujeruhiana na
mambo yote machafu yanayoashiria kuwa nchi yetu inaingia kwenye maangamizi.
Kwa leo
nataka niutumie uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, Iringa, kuonyesha ninachokisema hapa.
Yaliyojitokeza
Kalenga ni mambo machafu ya kutisha, ya kusikitisha, ya hatari na ya kukatisha tamaa,
yakionyesha ni jinsi gani nchi yetu inavyochungulia kuzimu!
Jambo la
kusikitisha na linaloshangaza kupita kiasi ni la kuwaona wanasiasa
wakishangilia na kufurahia kinachoitwa ushindi, kamwe watu hao hawaonekani
kutilia maanani ni mazingira gani yametumika kukipata hicho wanachokishangilia.
Hakuna anayejali kuwa kulikuwepo kutekana nyara, kuchomana visu, kutishiwa
kuuawa, kubakwa pamoja na kudhalilishana kulikovuka mipaka. Hayo yote
tunayasikia kwenye nchi zenye machafuko.
Wanasiasa
wanashangilia tu kinachodaiwa ni ushindi bila kujali kuwa kimepatikana katika
mazingira haramu. Kwa nini nasema hivyo? Hebu tuangalie.
Wananchi
waliojiandikisha kupiga kura Kalenga ni watu elfu 70. Waliopiga kura ni watu
elfu 28 tu, hata nusu haifiki! Kwa maana hiyo watu elfu 42 hawakupata haki yao
ya kupiga kura, na ndio walio wengi.
Mengi
yanasemwa, shahada za kupigia kura zilikuwa zinanunuliwa kama njugu, ushahidi
ni wa mtu aliyekamatwa na shahada za kupigia kura za watu mbalimbali zaidi ya
100. Kuna watu ambao majina yao hayakuonekana kwenye orodha ya wapiga kura
pamoja na kuwa na shahada zao halali walizopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Hao ni mbali
na idadi kubwa ya wananchi ambao Tume ya Taifa ya Uchaguzi imegoma kuwasajili
kama wapiga kura kwa kukataa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Katika hali
kama hiyo, ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi haitaki kuupima ukweli halisi wa
matakwa ya wananchi, unaweza ukapata wapi ujasiri wa kusema kwamba mgombea
fulani kashinda uchaguzi ilhali karibu robo tatu ya waliopaswa kumchagua au
kumkataa wamekoseshwa kwa makusudi haki yao ya kuonyesha wanachokitaka?
Tukiliacha
hilo, tutaona kwamba kila chama cha siasa nchini kina utaratibu wake wa kulinda
maslahi yake. Kutokana na Jeshi la Polisi nchini kuwa na majukumu mengi ya
kuulinda usalama wa raia na mali zao pamoja na mambo mengine ya ziada,
uwezekano wa jeshi hilo kuyalinda maslahi ya kila chama cha siasa kiukamilifu
unapungua.
Kwa
kulizingatia hilo, ndipo kila chama cha siasa kikabuni utaratibu wa kujilindia
maslahi yake. Huo ndio mwanzo wa vikundi vya Green Guard, Blue Guard, Red
Brigade nakadhalika. Vikundi vyote hivyo vinapaswa kuwa sehemu ya ulinzi
shirikishi kwa kusadiana na Jeshi la Polisi, kwa namna ya sera za jeshi hilo
zilivyo kwa sasa.
Lakini jambo
la kushangaza na kutia uchungu ni la kwamba Jeshi la Polisi linakitambua,
kukiheshimu na kukiogopa kikundi kimoja tu cha ulinzi wa vyama vya siasa, nacho
ni Green Guard cha CCM! Vikundi vingine vyote vinaonekana ni vya kihuni na ni
maadui!
Kivipi? Siku
moja kabla ya uchaguzi mdogo wa Kalenga, Kamanda wa Polisi mkoani Iringa,
Ramadhani Mungi, alitangaza kwamba jeshi lake limejiimarisha kulinda usalama
katika eneo lote la Kalenga wakati wa uchaguzi huo mdogo. Kwahiyo akasema
kwamba hatapenda kuvisikia vikundi vya Green Guard wala Red Brigade katika
kipindi hicho.
Kumbe
tangazo hilo lilikuwa kama la kutaka kuwaondoa Red Brigade kusudi Green Guard
wafanye uhalifu wao kiurahisi!
Sababu
baadaye tulisikia mbunge wa Chadema, viti maalumu, Rose Kamili, katekwa na
kufanyiwa kila vitendo vya kinyama, kihuni na kishenzi na kikundi cha Green
Guard. Lakini badala ya Kamanda Mungi kutueleza namna alivyowashughulikia
wahuni hao, akaonekana anakibariki kitendo walichokifanya kwa kusema kwamba
walimkamata mbunge huyo akitoa rushwa! Kauli yake ya kwamba hataki kusikia
Green Guard wala Red Brigade akawa ameisahau!
Sote
tunaelewa kwamba kazi ya kuwashughulikia watoa na wapokea rushwa ni ya watu wa
Takukuru, ni lini Mungi ameigeuza kazi hiyo na kuifanya iwe ya vijana wa Green
Guard?
Hata hivyo
hakuna sheria inayosema kwamba anayekamatwa akitoa au kupokea rushwa apelekwe
kwenye ofisi za CCM na kusulubiwa, kama alivyofanyiwa Rose Kamili. Sheria hiyo
ni ya Mungi na vijana wake wa Green Guards!
Shabiki
mmoja wa CCM anasema kwamba kitendo cha Green Guards kumteka mbunge kinalipiza
kisasi kitendo cha Red Brigade kumteka mkuu wa wilaya katika uchaguzi mdogo wa
Igunga.
Lakini ikumbukwe
hekaheka na hinyahinya zilizojitokeza kufuatia kitendo hicho cha Igunga. Mbona
hatukuona kitu kama hicho kule Iringa? Au tuseme polisi wanalinda usalama wa
wananchi wakiangalia itikadi zao ziko upande gani?
Je,
ingetokea yule mama wa Igunga akaingizwa kwenye ofisi ya Chadema na kufanyiwa
unyama kama aliofanyiwa Rose Kamili ndani ya ofisi ya CCM hali ingekuwaje?
Ofisi hiyo ya Chadema isingekuwa gofu sasa hivi?
Baada ya
tukio la kutekwa mbunge Rose kamili yakafuatia matukio mbalimbali ya kutekwa
vijana kadhaa wa Chadema kuhusiana na uchaguzi huo wa Kalenga. Vijana hao
wamefanyiwa unyama wa kila aina kama baadhi yao walivyotoa ushuhuda baada ya
kunusurika vifo.
Wakati
mwingine Kamanda Mungi alidai kuwa polisi inawashikilia vijana wawili kutoka
Arusha, kwamba walienda Iringa kwa ajili ya kufanya vurugu kwenye uchaguzi wa
Kalenga. Taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa, zinasema kwamba
vijana hao ndipo wamepatikana baada ya kupotezwa kwa siku karibu nne!
Lakini Mungi
hasemi lolote kuhusu vijana wa CCM waliosombwa
kutoka kila kona ya Tanzania na kujazwa Iringa, pamoja na vitendo vyao
kueleza kila kitu kutokana na unyama walioufanya kule.
Wapo
wanaosema kwamba yaliyotokea Kalenga yanatokana na amri ya mwenyekiti wa CCM,
Rais Kikwete, ya kwamba CCM wanapaswa wajilinde wenyewe na kujibu mapigo!
Lakini badala ya kujibu mapigo mbona wanashambulia?
Ni wazi
kwamba mambo hayo, yaliyo na baraka za mwenyekiti wa chama tawala na Amiri
Jeshi Mkuu, yanaifanya nchi yetu ichungulie kuzimu. Sababu sioni yataiepushaje
nchi isikumbwe na zaama kama zile za Anti-Balaka na Seleka kule Afrika ya Kati.
Je, hicho
ndicho anachopanga kutuachia Kikwete, tuliyemuona ni kiongozi bora, kama zawadi ya kumaliza muda wake madarakani?
0784 989 512