JK ATANGAZA KIAMA CHA MAJANGILI
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema
Serikali imenuia kumaliza kabisa ujangili nchini, ikiwa ni hatua ya
kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka katika hifadhi za taifa.
Hakusita kusisitiza kwamba, nia ya dhati ya
Serikali ni kuhakikisha mkakati huo unakamilika, japokuwa kumekuwa na
changamoto zinazotokana na ukubwa wa hifadhi hizo na uhaba wa vitendea
kazi pamoja na askari wa wanyamapori.
Akizungumza wakati wa kupokea magari 11 ya kisasa
kwa ajili ya kusaidia operesheni ya kupambana na ujangili kutoka kwa
Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) la Ujerumani, Kikwete
alisema tatizo hilo limekuwa la muda mrefu, lakini juhudi za kulikomesha
zinafanyika.
Alisema, pamoja na ukubwa wa tatizo hilo, bado
kuna tatizo la uhaba mkubwa wa wafanyakazi wanaotakiwa kudhibiti
majangili, ambapo kwa sasa kuna wafanyakazi 1,155 sawa na asilimia 24 tu
ya mahitaji halisi ya wafanyakazi 4,000 wanaohitajika.
“Mwaka uliopita, Serikali ilisimamia ajira ya wafanyakazi 449 na sasa kuna ajira ya wafanyakazi 500.
Kwa maana hiyo tutafikisha wafanyakazi wapya 949
na kufanya mahitaji ya wafanyakazi wapya kuwa 4,000 zaidi ili kuwezesha
utekelezaji wa majukumu kwa viwango vya kimataifa,” alisema.
Kwa mujibu wa viwango vilivyopo sasa, mfanyakazi
mmoja anasimamia eneo la kilometa za mraba 169 ikilinganishwa na viwango
vya kimataifa vya kilometa za mraba 25 kwa kila mfanyakazi mmoja.
Rais Kikwete alisema kwa sasa Serikali itaendelea
kuajiri idadi hiyo ya wafanyakazi kila mwaka kwa miaka mitatu ijayo ili
kuhakikisha pengo lililopo linazibwa.
Alisisitiza kuwa, kampeni dhidi ya ujangili ni
suala la kimataifa na Tanzania au nchi zilizoathirika hazitaweza
kulikabili bila ushirikiano wa kimataifa.
Alisema upo ulazima wa kuteketeza mitandao yote ya
ujangili na kuwawajibisha ipasavyo watakaonaswa, kwani kwa kufanya
hivyo kutasaidia kulinda urithi huo wa dunia.
Ukosefu wa vifaa
Akifafanua, Rais Kikwete alisema kuongeza idadi
hiyo ya wafanyakazi pekee haitakuwa na maana iwapo hawatakuwa na vifaa
maalumu vya kisasa vitakavyowawezesha kukabiliana ipasavyo na tishio la
ujangili.
Katika mkakati wa maboresho hayo, Kikwete alisema wanafanya
jitihada za kuongeza idadi ya magari, kuongeza vifaa vya kisasa kwa
ajili ya doria na vifaa vya mawasiliano, ambavyo vinahitaji uwezo mkubwa
wa kifedha ambao utaweza kutekelezwa na serikali kwa kipindi kirefu
iwapo haitapata msaada wa uwezeshaji kutoka kwa wadau.
Msimamo wa Wizara
Akizungumzia msimamo na mikakati ya Wizara ya
Maliasili na Utalii, Waziri Lazaro Nyalandu alisema kutokana na ukubwa
wa tatizo, wanahitaji vifaa vya kisasa zaidi, ikiwamo helikopta na ndege
zisizo na rubani kwa ajili ya kufanya doria kwenye maeneo yote ya mbuga
na hifadhi za taifa.
Aliwatahadharisha wafugaji wanaopenda kuingiza
mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi, akiwataka kuondoa mifugo yao mapema
kwa kuwa katika operesheni hiyo hakuna atakayeachwa.
“Katika operesheni hii, hakuna jangili wala mfugaji atakayeachwa iwapo atakutwa kwenye maeneo ya hifadhi,” alisema.
Alifafanua kwamba, msaada huo wa magari utapelekwa
maeneo tofauti, matano kanda nane za Selous, mengine matano Hifadhi ya
Serengeti na moja Hifadhi ya Maswa.
Mwaliko wa vyombo vya habari
Nyalandu alisema Wizara yake imevialika vyombo
vyote vya habari vya kimataifa kwa ajili ya kuja kupata taarifa sahihi
kuhusu kampeni dhidi ya ujangili zinavyotekelezwa ili kuepuka ripoti za
upande mmoja kwa ajili ya kuweka usawa.
Alisema hatua hiyo ilichukuliwa na wizara yake
walipokwenda kwenye mkutano maalumu na Rais Kikwete ulioandaliwa na
mtoto wa Mfalme wa Uingereza, Prince Charles kwa ajili ya kuangalia
namna ya kulinda wanyama walio hatarini kutoweka duniani, wakiwemo tembo
na faru.
MWANANCHI
MWANANCHI