KAULI ZILIZOVUTA HISIA YA WENGI BUNGE MAALUM LA KATIBA DODOMA
Dodoma. Ni vigumu kueleza matukio yote
yaliyotawala kauli na hisia za wengi kwa wiki nzima mjini Dodoma bila
kuangalia michango ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Michango hiyo ya mawazo katika mjadala kuhusu
rasimu ya kanuni zinazopaswa kuongoza kikao kwa siku 70 za kikao hicho,
baadhi yake zilikuwa kali.
Zifuatazo ni baadhi ya kauli hizo:
Mchungaji Christopher Mtikila
Mtikila, ambaye ni mwenyekiti wa Democratic Party
(DP), alitumia dakika tano kutoa somo kwa wajumbe wa Bunge hilo kuhusu
umuhimu wa kupiga kura ya siri badala ya ile ya wazi.
Anasema haki ya kupiga kura kwa siri haitofautiani
na haki ya mtu kuwa na miguu miwili na kwamba itashangaza akitokea
mtawala akaamuru kila mtu awe na mguu mmoja, halafu watu wakakaa
kujadili.
“Wote tutaonekana tuna matatizo ya akili,” alisema Mch. Mtikila.
Alisema Bunge Maalumu la Katiba litaingia katika
hatia na aibu kwa kujadili mambo ya msingi ya kidemokrasia ambayo pia
yameainishwa katika katiba ya sasa, likiwamo suala hilo la kura ya siri.
“Mwenyekiti (akimlenga Pandu Ameir Kificho)
tumekuchagua kwa kura ya siri siyo kwamba tulikuwa wajinga kuliko
wenzetu, hapana! Ni ‘democratic civility’ (ustaarabu wa kidemokrasia),”
alisema.
“Ni aibu waheshimiwa na hii nasema si jambo la
mjadala kuna vitu vya kujadili, lakini si haki ya kupiga kura kwa siri.
Hii ni haki ya msingi ya kidemokrasia,” alisema.
Bulaya, tofuti na wajumbe wenzake wengi kutoka
chama tawala (CCM), alionekana kutoa mchango uliogusa hisia za wengi
hasa pale alipoeleza bayana kuwa hayuko tayari kuona ukandamizaji
unafanyika kumlazimisha apige kura ya wazi.
Akirejea msimamo wa kura ya wazi unaoshabikiwa na wajumbe wengi wanaotokana na chama chake, alisema hawezi kupiga kura ya aina hiyo wakati anajua inamnyima uhuru wake.
Akirejea msimamo wa kura ya wazi unaoshabikiwa na wajumbe wengi wanaotokana na chama chake, alisema hawezi kupiga kura ya aina hiyo wakati anajua inamnyima uhuru wake.
“Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko. Ni
lini na wapi katika uamuzi mgumu kama huu kulifanyika kura za wazi kama
wengi wanavyotaka,” alisema.
Sheikh Hemed Jengo
Sheikh Jongo alishauri Bunge Maalumu la Katiba
kuwapa nafasi wajumbe wanawake watakaokuwa katika hedhi, waruhusiwe
kuapa bila kushika kitabu kitukufu, Quran.
“Siku nyingine kinamama wanakuwa katika siku
maalumu (hedhi). Ni haramu kwa mujibu wa dini kushika msahafu.
Atakapojieleza kuwa hali yangu si nzuri, basi aruhusiwe kuapa hivyo
hivyo kwa heshima,” alisema na kuongeza:
“Hata kwa wanaume wa Kiislaamu wakitaka kuapa
wachukue udhu kwa sababu kitabu chenyewe kinakataza kukishika bila ya
udhu. Ndiyo yamini. Ndiyo maana watu wengine hatuoni wanafanya vizuri
kule nje kwa sababu wanajua waliapa bila udhu na haikuwa yamini.”
Profesa Maghembe alifananisha upigaji wa kura kwa
siri kuwa sawa na ule uliofanyika nchini Marekani wakati wa kashfa ya
ufuska iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa rais wakati huo, Bill Clinton.
“Kule Marekani walikuwa wakipiga kura ya kumwondoa
madarakani Clinton kwa madai ya kushikwa ugoni. Walipiga kura ya wazi
kwa sababu lilikuwa jambo kubwa la kumwondoa mtu madarakani,” alisema.
Profesa Maghembe, ambaye pia ni Waziri wa Maji,
aliwasihi wajumbe kutofautisha upigaji kura wa mwenyekiti wa kijiji,
diwani, mbunge na rais ambao alisema wananchi hupiga kura za siri.
“Humu ndani tunatafuta sheria mama ya nchi.
Tumepewa jukumu hilo kwa niaba ya Watanzania wote. Wao watapata nafasi
ya kusema ndiyo au hapana. Sasa tunajificha ili iweje, tunamficha nani?”
alihoji.
Maria Sarungi Tshehai
Maria Sarungi Tshehai
Mwanaharakati huyo alitumia fursa aliyopewa kuwaponda wajumbe
wenzake waliokwenda katika Bunge hilo kwa ajili ya kuwasilisha masilahi
ya vyama.
“Hatuko hapa kwa ajili ya kuwasilisha vikundi mbalimbali. Tukianza hivyo itakuwa ni hatari sana katika Bunge hili,” alisema.
“Nianze kwamba kitu kilichonifanya nitoke nje
nilifutwa (na mtu ambaye hakumtaja jina). Aliniambia wewe mbona
unaonekana upo kwenye upande wa chama fulani.”
Profesa Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti –CUF Taifa)
Mwenyekiti huyo wa CUF alisema msingi wa kupiga
kura ya siri ni kujaribu kuwalinda wajumbe ambao wanaweza kupiga kura
kinyume na misimamo ya vyama vyao au makundi yao.
Akijenga msingi wa hoja yake, Profesa Lipumba
alisema hata Jaji Joseph Warioba katika taarifa yake alisema moja ya
taasisi zilizotoa maoni ni Baraza la Wawakilishi lililopendekeza
Serikali tatu.
“Tunadai kura za siri kusudi kuwalinda hawa
wenzetu ambao wametoa misimamo, wakija kupiga kura hapa inaweza kuwapa
matatizo huko walikotoka,” alisema.
Aliongeza : “Tunapolishabikia hili kuwa pasiwe na
kura ya siri inaonekana wazi pana ajenda ya kuwashughulikia
watakaokwenda kinyume cha msimamo.”
Richard Ndassa (Mbunge wa Sumve)
Yeye alionekana kukerwa na baadhi ya taarifa za
vyombo vya habari kuhusu suala la posho na kuvishtaki vyombo hivyo kwa
mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho.
“Wabunge wanachota milioni 129 kwa kikao cha
dakika 30” na kingine kikisomeka, “Wabunge walipwa milioni 130 kwa
dakika 25; Bunge la Katiba vipande vipande; wapewa posho kwa kusoma
magazeti,” alisema akikariri vichwa vya habari vya baadhi ya magazeti na
kudai vinamkera.
Pandu Ameir Kificho (Mwenyekiti wa Muda)
Naye Kificho, ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar, alionyesha kukerwa na baadhi ya vyombo vya habari hasa
vilipolishikia bango suala la posho.
“Kusema kweli, jamii tunaichanganya mpaka jambo
hili la kutupatia Katiba Mpya lionekane ni la mchezo au tumekuja kudai
posho. Nawataka wenzetu (wanahabari) wawe makini sana juu ya jambo hili
wasiupotoshe umma ili kazi hii isiingie dosari,” alisema.
“Vyombo vyote vya habari vizingatie kupata habari
kwa uwazi na ukweli kutoka kwa wanaohusika ili jamii yetu ya Watanzania
ipate habari za kweli na hilo la kupokea tu posho kwa kusoma magazeti
tunalikanusha kwa nguvu zote”.
Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini-Chadema)
Ndesamburo aliwataka wajumbe wenzake kuacha
ushabiki wa kisiasa na kutambua wanatengeneza katiba itakayodumu miaka
50 ama miaka 10 ijayo.
“Tusilete ushabiki. Nawaombeni sana tusilete
ushabiki katika jambo hili. Hili ni jambo zito. Hili ni jambo
tunalolifanya kwa niaba ya Watanzania milioni 45 na sisi tumepata bahati
tu; ni Mungu ametusaidia,” alisema.
Dk. Zainab Gama
Naye mwanasiasa mkongwe, Dk. Zainabu Gama
alikwenda mbali na kudai kuwa baadhi ya wanaotaka kura ya siri wametumwa
na watu ama wamekula rushwa ndiyo maana hawataki kupiga kura ya wazi.
“Hatukuletwa hapa kimchezo mchezo. Simama, sema mimi uamuzi wangu huu kila mmoja akuone,” alisema.
MWANANCHI
MWANANCHI