MRAJIS WA VYAMA VYA USHIRIKA NI KIKWAZO KWA USHIRIKA
Na Prudence Karugendo
BAADHI ya
wanaushirika nchini wanaichukulia, kwa tuhuma, nafasi ya Mrajis wa Vyama vya
Ushirika nchini kuwa ipo kuukwamisha ushirika na kuudumaza badala ya
kuustawisha na kuufanya ushamiri. Kwa sababu hiyo, wanajiuliza, nafasi hiyo ni
ya nini inayofanya mambo kinyume na makusudio ya kuanzishwa kwake?
Wapo
wanaodhani kwamba cheo cha Mrajis wa Vyama vya Ushirika kilianzishwa baadaye
kabisa, kama moja ya mikakati ya
serikali ya kuuboresha na kuuimarisha ushirika nchini, sasa wanashangaa kuona
mambo yanakwenda kinyume chake.
Wanaushirika
wanasema kwamba haileti maana yoyote kuona kitu kinasajiliwa ilmradi tu, kwa
maana ya ushirika, na kisha kinapotea bila kuonyesha manufaa yoyote yaliyochochea
kikasajiliwa, na hasa ikizingatiwa kwamba kitu chenyewe kinagusa maisha ya watu
walio wengi, wakulima, kwa maana ya kuwa
mhimili wa uchumi wao.
Katika
makala hii nataka niitazame nafasi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika nikiwa
upande wa Vyama Vikuu vya Ushirika vinavyoulinda uchumi wa wakulima, kwa
kukishughulikia kile wanachohangaika kukizalisha katika kujaribu kuuinua uchumi
wao sambamba na maisha yao.
Sio kweli,
kama yalivyo mawazo ya baadhi ya wanaushirika, kwamba nafasi ya Mrajis wa Vyama
vya Ushirika iliundwa baadaye wakati ushirika ukiwa umeishaanzishwa muda mrefu.
Mrajis wa kwanza nchini aliteuliwa tarehe 4 / 3/ 1932, muda mfupi baada ya
serikali ya kikoloni kupitisha Sheria ya Vyama vya Ushirika, tarehe 22 / 2 /
1932.
Kwahiyo
wakulima wanapoamua kuunda ushirika wao, wakafuata itifaki zote zinazotakiwa
kisheria, wanachokilenga ni kuziona juhudi zao katika kilimo zikiwalipa jasho
lao. Kuwainua kiuchumi na kuwaondolea ufukara. Sio jambo la kwenda tu kwa
Mrajis kuusajili ushirika wao na mambo kuishia hapo.
Kwa maana
hiyo Mrajis wa Vyama vya Ushirika anapaswa kuwa kichocheo cha wakulima kutamani
kuanzisha ushirika. Sababu ushirika unaposhamiri kwa upande wa wakulima kilimo
nacho kinashamiri sawia, pia maana ya kuwepo kwa Mrajis inajionyesha mara moja
na kuwavutia wakulima.
Mrajis wa
Vyama vya Ushirika anapofanya kazi yake kadiri inavyotakiwa ushirika unapanuka
haraka kutokana na wananchi wengi kutamani kuanzisha vyama vya ushirika,
watafanya hivyo kwa vile watakuwa wanayaona mafao yake yalivyo manono.
Mrajis wa
kwanza hapa Tanganyika, pamoja na kazi hiyo ya kusajili vyama vya ushirika, alikuwa akifanya kazi nyingine vilevile.
Lakini ilipofika mwaka 1945 ilibidi aache kazi nyingine ili atumie muda wake
wote wa kazi kwenye shughuli za vyama vya ushirika. Huo ni umuhimu wa ushirika
ulioonwa na wazungu, wakoloni!
Hata
serikali ilipotengeneza cheo cha Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Ushirika
mwaka 1951, ilibidi cheo hicho kiunganishwe kwa mtu mmoja kwa vile madhumuni
yake hayakutofautiana sana na ya Mrajis. Kwahiyo kati ya mwaka 1951 – 1971,
kazi zote mbili zilikabidhiwa kwa mtu mmoja, Mrajis wa Vyama vya Ushirika.
Kutokana na
serikali kuuona umuhimu wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika, pamoja na umakini
uliokuwa ukionyeshwa na Mrajis wakati huo, ndiyo maana ushirika ulishamiri sana
nchini kiasi kwamba katika kipindi cha karibu miaka 40, kati ya mwaka 1932 –
1971, idadi ya vyama vikuu vya ushirika nchini ilifikia 1854!
Idadi hiyo
ni tofauti kabisa na idadi ya vyama vikuu vya ushirika vilivyoanzishwa, kama
kweli vipo, katika kipindi chamiaka 40 iliyofuatia, kati ya 1970 – 2010.
Kutokana na
mabadiliko ya sera za nchi yaliyochangia mabadiliko ya mara kwa mara katika
Sheria za Vyama vya Ushirika nchini, na hivyo umakini kutoweka na uzembe
kutawala katika nafasi ya Mrajis, tumeweza kushuhudia maangamizi ya vyama vya
ushirika yaliyovifanya vyama vikuu vibaki 44 tu nchini kote ilipofika mwaka
2004.
Na si ajabu
ninapoandika makala hii vikawa vimebaki vyama vikuu visivyozidi 5 nchi nzima.
Navyo vilivyopo ninaonekana kuchungulia kaburi.
Pamoja na
idadi ya vyama vikuu vya ushirika nchini kupungua kwa kiasi hicho cha
kusikitisha na kutia majonzi, huku vyama vilivyobaki vikionekana kuchechemea
kama mgonjwa aliye mahututi, pasipo na jitihada za wazi za kuvinusuru, nafasi
ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika ndio kwanza inaanza kushamiri! Swali
linalojitokeza ni la kwa nini nafasi hiyo ishamiri wakati madhumuni
yaliyoifanya ikaanzishwa yamenyauka?
Wakulima
wanaounda vyama vya ushirika wanawezaje wakajivunia nafasi hiyo ya Mrajis wakati
wakiuona ushirika wao ukifa kifo cha kizembe? Au tuseme malengo ya nafasi hiyo
yamebadilika, yamekuwa ya kuunyonga ushirika badala ya kuutengeneza na
kuuendeleza?
Mbali na
hilo la Mrajis kutovijali vyama vya ushirika, linajitokeza lingine la nafasi
hiyo kuvichukulia vyama hivyo kama mkusanyiko wa watoto wenye mtindio wa
ubongo, watoto wasioweza kujiamria lolote bila kuelekezwa la kufanya, tena kwa
usimamizi wa karibu!
Utaraibu wa
kwamba vyama vikuu vya ushirika haviwezi kufanya baadhi ya mambo yake bila idhini
ya Mrajis ni jambo linaloleta utata katika vyama hivyo. Sababu kama watu wazima
wanaweza wakaamua kuunda ushirika wanaouona una manufaa kwao kutokana na
wanachokizalisha, inawezekanaje pale wanapotaka kupanua manufaa yao mtu
mwingine, tena asiyekuwa mnufaika kwa lolote katika ushirika husika, awaamurie
ni kipi cha kukifanya na kipi cha kukiacha? Hapo ndipo Mrajis anapoonekana ni
kikwazo.
Jambo la
kushangaza, kama sio kusikitisha, Mrajis anaweza akauona uovu unaofanyika ndani
ya vyama vya ushirika dhidi ya makelele yanayopigwa na wanaushirika wakiomba
msaada wake, yeye akaamua kufumba macho kama vile haoni kitu, akashindwa
kutumia mamlaka yake aliyopewa kisheria kuingilia kati na kuufutilia mbali uovu
unaopigiwa kelele!
Mfano wanaushirika wanapopiga sana kelele bila
msaada wowote toka kwa Mrajis mwishowe wanaishiwa nguvu na kunyamaza. Na huo
ndio unakuwa mwisho wa ushirika husika. Vyama vikuu vingi vya ushirika
vimeangamia kwa mtindo huo.
Hiyo maana
yake nini? Hivyo tuendelee kujiaminisha kuwa bila Mrajis wa Vyama vya Ushirika
nchini ushirika hauwezekani? Kama nafasi hiyo ipo kuuangamiza ushirika, basi
ushirika unawezekana bila nafasi hiyo?
Ngoja nitoe
mifano miwili iliyo hai. Kuna chama cha msingi kilichokuwa kati ya vinavyounda
chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. cha Kagera. Chama hicho cha msingi cha Magata, wilani
Muleba, kimejitoa katika KCU na kinafanya mipango ya kuwa chama
kinachojitegemea. Lakini kikwazo ni Mrajis Msaidizi mkoani humo.
Moja ya
kanuni za vyama vya ushirika inasema kwamba “Chama chochote chenye madhumuni ya
kuendeleza uchumi wa wanachama wake kufuatana na masharti ya vyama vya ushirika
kinaweza kuandikishwa”. Lakini pamoja na kulielewa hilo Mrajis Msaidizi bado
anakiwekea vikwazo, mbali na mambo mengine, ana madai ya kwamba kuna watu
wawili wameongezeka katika Bodi ya chama hicho ambao yeye hawataki! Watu hao ni
Enock John Babu na Yusuf Kakwata.
Wanaushirika
wa Magata wanasema kwamba hizo ni sababu binafsi za Mrajis Msaidizi kutokana na mazoea yake ya
kuvichagulia vyama vya msingi watu wa kuingia kwenye Bodi za vyama hivyo badala
ya wajumbe wa Bodi kuchaguliwa na wanaushirika.
Mfano wa
pili ni wa Ilango, Kata ya Buterankuzi, Bukoba Vijijini. Wanaushirika wa Ilango
wanata kuanzisha chama chao cha msingi ili wakajitenge na chama cha msingi cha
Itongo, Kata ya Ibwera, Bukoba Vijijini. Sababu zilizowafanya wafikie uamuzi
huo ni pamoja na umbali wa kutoka kata moja kwenda kata nyingine kwa ajili ya
kupeleka mazao.
Kanuni
mojawapo ya vyama vya ushirika inasema kwamba kwa upande wa vyama vya mazao
wakifika watu 50 wanaweza kuanzisha chama cha msingi. Wanaushirika wa Ilango
tayari wako 70. Na tayari wameishajenga ghala kubwa la kuhifadhia mazao, hasa
kahawa, lililofunguliwa na Afisa Ushirika wa Wilaya ya Bukoba, 2013. Pamoja na
hiyo wanasema tayari wameishafungua akaunti Benki.
Ibarahim
Rwamlaza ni mwenyekiti wa wanaushirika hao wanaotaka kuanzisha chama hicho cha
msingi cha Ilango. Rwamlaza anasema kikwazo pekee walicho nacho ni Mrajis
Msaidizi. Anasema haelewi ni kwa nini Mrajis Msaidizi anawafanyia hivyo.
Naamini
kwamba nafasi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika inatokana na Sheria ya Vyama vya
Ushirika iliyoundwa na Bunge. Kwa maana hiyo ni muhimu Bunge letu, linaloundwa
na wawakilishi wa wananchi, likairejea Sheria hiyo ya Vyama vya Ushirika na
ikiwezekana kuifutilia mbali nafasi hiyo ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika.
Bunge
linaweza kuutafuta utaratibu mwingine ulio bora utakaouwezesha ushirika
kushamiri tena nchini kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, hasa tangu enzi za
wakoloni. Hiyo ni iwapo kama wabunge wanawajali wananchi wanaowawakilisha.
Haiwezekani
nafasi zilizopo nchini kwa ajili ya masuala ya ushirika, kama ilivyo Wizara ya
Ushirika, Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Shirikisho la Vyama vya Ushirika
nakadhalika, vishamiri wakati ushirika wenyewe ukiwa umekata roho.
0784 989 512