PAPA NA NYANGUMI NI MIFANO IPASWAYO KUTUFIKIRISHA
Na Prudence Karugendo
NILIPOANDIKA juu ya Watanzania kuponzwa na utulivu na wema wetu baadhi ya
wasomaji walinipongeza na wengine kunilaumu. Vyote viwili, lawama na pongezi,
sikuvitilia maanani kwa vile waliofanya vile niliona kuwa hawakunielewa vizuri.
Walionipongeza wengi wao
walisukumwa na mtizamo wa ubaguzi wa rangi. Hawa imani yao ni kwamba uzalendo
ni rangi, ukiwa mweusi basi wewe ni mzalendo, kwao haijalishi kama unatoka
Msumbiji, Rwanda, Kongo au kwingineko nje ya nchi hii. Au kama unafanya matendo
yasiyoendana na uzalendo. Ilmradi wewe ni mweusi basi, kwao inatosha. Mimi huo
sio uliokuwa mtizamo wangu, mtizamo wangu ulikuwa uasilia wa nchi yetu na moyo
wa kuipenda na kuifia nchi yetu.
Vilevile kuna walionilaumu
kuwa nilichokiandika ni ubaguzi wa rangi. Hawa waliona kama nataka kurudisha
mambo nyuma kwa kuyataja mambo ambayo wao wanaona yamepitwa na wakati. Pia
katika kundi hilo la lawama kuna waliodhani naongelea vita ya papa na nyangumi
ambavyo wanaona ningeviacha badala yake
nikayatizama maisha ya mwananchi wa hali ya chini.
Nataka nieleweke kwamba mimi
siyo mbaguzi wa rangi hata kidogo, wala sikuandika kuonyesha chuki yangu kwa
Wahindi. Mimi ninao marafiki zangu wengi
Wahindi, kama ningekuwa nawachukia ningewezaje kuwa na urafiki nao? Mimi ninachokichukia ni hulka ya Wahindi
inayojionyesha imo katika utamaduni wao, ubaguzi. Hata wao uwa nawambia hivyo.
Wanabaguana hata wao kwa wao!
Sioni kwa nini tukalazimike
kuuheshimu utamaduni wao huo wa kishenzi wanaouendeleza hadi huku kwetu kiasi
cha kufikia kutubagua hata sisi tuliowakaribisha. Utamaduni ukiwa wa kishenzi,
wa kuumizana ndani ya jamii yoyote, unapingwa kwa kuzingatia wakati uliopo.
Ndiyo maana ukeketaji wa wanawake unapingwa kwa nguvu zote japo tendo hilo limo
katika baadhi ya tamaduni.
Wasomaji wengine walidhani
kwamba niliandika kuonyesha upande niliopo kati ya nyangumi na papa. Ukweli ni
kwamba nilikuwa sijashawishika kuvutika upande wowote kwa vile ni upande mmoja
tu uliokuwa umetoa mashambulizi yake ya
kushtukiza. Ile ilikuwa ni bahati mbaya tu kwamba makala yangu ilitoka kipindi
kile mashambulizi yale yanaanza, wala makala yangu haikuwa na uhusiano wowote
na mashambulizi yenyewe.
Vilevile kuna ambao kwa neno la Kiingereza naweza kuwaita “naive”, sipati
haraka neno la Kiswahili lenye maana hiyo, walionipa ushauri wa kwamba vita
hiyo tungeiacha tukaongelea maisha ya wananchi wa hali ya chini. Ingawa sikuwa kwenye vita hiyo lakini
niliwaeleza kuwa kama wewe ni samaki mdogo huna jinsi ya kuviona vitimbwi vya
papa na nyangumi havikuhusu wakati mko kwenye bahari ileile moja.
Nieleze kidogo kuhusu watemi
hawa wawili wa baharini. Papa nisamaki mdogo kulinganisha na nyangumi ila ni
mkorofi sana kuliko nyangumi. Nyangumi akilinganishwa na papa kitabia ataonekana
ni mtulivu sana na wakati mwingine kuonekana mwenye huruma. Ila angalia, kwa
ukubwa wake wa umbo havuliwi kirahisi kama papa mwenye makeke. Na kwa wema wake
huachia domo lake kubwa samaki wadogo waingie wakidhani wamepata mahali salama
pa kujihifadhi kumbe ndio kwanza wanageuzwa asusa.
Vilevile papa anaweza
kutunisha mgongo wake ukaonekana kama kisiwa kidogo kiasi cha kuwapa matumaini
hata wavuvi kuwa wamepata mahali pa kujipumzisha, kumbe ile ni hadaa ya
nyangumi, anataka azame na kuwazamisha wote walioweka matumaini mgongoni kwake.
Huo ndio ubaya na hatari ya nyangumi tofauti na papa ambaye kutokana na ukorofi
wake kila kiumbe cha baharini kimeishaelewa kiishi naye vipi, hata wavuvi nao wameishausoma ukorofi wake ndiyo sababu ya
papa kuvuliwa mara kwa mara tofauti na nyangumi.
Kwahiyo nadhani kutajwa kwa
mfano wa nyangumi hakukusukumwa tu na jazba iliyotokana na mfano wa kwanza wa
papa, bali huu unaonekana ni mfano uliotolewa kiumakini kwa kuzingatia mwenendo
wa hali halisi ulivyo nchini mwetu na hasa katika vita hii tuliyomo ya
kupambana na ufisadi. Vita hii ambayo kila mmoja anaweza kunyoosha kidole kwa
mwenzie kuwa ndiye adui ili kuyazubaisha mashambulizi ya pamoja inatugeuza kama
watu tuliozama baharini tukiwa tunatapatapa tukitafuta pa kushika ili kujinusuru, hapo ndipo
tunapotahadharishwa na hadaa za nyangumi ambaye kwa upole wake anaweza
kutufunulia domo lake ili tuingie tukidhani kwa kufanya vile tumejinusuru kumbe
ndio kwanza tumejigeuza chakula chake.
Hii inapaswa ibomoe fikira za
kwamba vita hii dhidi ya ufisadi tunaweza kuifanikisha kwa kutumia mbinu za ubaguzi, ukabila au madhehebu. Yeyote
anayetushawishi kutumia mbinu hiyo tayari anakuwa amejigeuza nyangumi kwa
kujifanya mpole na kutufunulia domo lake tuingie wenyewe eti kwa kutuonea
huruma baada kutuangalia tunavyotapatapa. Kumbe kuingia kwetu ndani ya domo
lake ndio unakuwa mwisho wa yote. Hakuna cha vita dhidi ya ufisadi
kitakachokuwa kinaendelea maana tutakuwa tumemezwa na ufisadi wenyewe.
Kwahiyo tunapopigana vita hii
inabidi tujihadhari na chuki, husda, vinyongo, ushindani nakadhalika. Mambo
haya tusipoyaangalia ni lazima yatugawe katika makundi niliyoyataja hapo juu.
Ni rahisi mtu kusema anashambuliwa kwa vile ni wa madhehebu fulani, kabila fulani au rangi fulani,
na hivyo kuwashawishi walio mstari wa mbele katika mapambano kuvunjika moyo kwa
vile anayeshambuliwa kaishajionyesha ni wa rangi yao, kabila lao au madhehebu
yao.
Kwahiyo mashambulizi
yanagawanyika na si ajabu yakageuka ya kushambuliana wenyewe kwa wenyewe badala
ya kumshambulia adui. Vita inakwama na adui anashinda kirahisi.
Katika makala yangu
niliyokuwa nawataja Wahindi kwa tabia yao chafu ya ubaguzi sikusukumwa na
mtizamo wa rangi yao, tatizo langu ni tabia yao. Kwahiyo walionipongeza kwa
misingi ya ubaguzi wa rangi kwamba kwa kuwataja Wahindi pengine nilimaanisha na
Wazungu, Waarabu Waajemi nakadhalika, hao walikuwa wamepotea kabisa. Hawa wengine,
japo rangi zao zinashabihiana na ya Wahindi, weupe, tabia zao ni tofauti
kabisa. Kitu cha Mhindi hakiguswi na asiyekuwa Mhindi. Angalia hata dini yao
Hindu, ni ya Wahindi watupu, tofauti na
hizi dini nyingine tulizozizoea, Ukristu na Uislamu.
Ningewataja Waarabu na
Wazungu kweli ningekuwa mtu wa ajabu, sababu hawa ni watu ambao nina undugu nao
wa damu. Ninao binamu zangu Waarabu, ninao shemeji zangu wengi Waarabu kwa
maana hiyo ninao wapwa zangu wengi wenye asili ya Uarabu. Vilevile niye baba
mdogo mzungu, mkwe wangu mzungu, shemeji zangu wawili wazungu. Kwahiyo ninao wadogo zangu wazungu, wapwa
zangu wazungu nakadhalika. Watu hawa
nitawasemaje kwa mtizamo wa ubaguzi wa rangi?
Wahindi ndio wanaotubagua,
najiuliza kwa nini?
Kama nilivyosema, Waarabu na Wazungu tunaishi kiundugu, kule
kwetu wamelima mpaka mashamba ya migomba “ebibanja” na kujenga nyumba za
kudumu. Sio watu wanaopendelea kuishi mijini tu wakiwa wamekaa mkao wa kuondoka
wakati wowote kama wenzetu Wahindi. Hilo tuliangalie kwa umakini.
Lakini hatahivyo kitendo cha
Wahindi kutubagua hatuwezi kukigeuza kichaka cha kuficha maovu yetu. Kwamba mtu
anapofanya matendo yanayoisaliti jamii yake, ufisadi, atuelekeze kwenye kichaka
kile cha Wahindi, au watu kutoka nje, kuwa ndimo ulimo uchafu wote ili yeye
asigeuziwe shingo. Inabidi kwanza tujisafishe sisi wenyewe na kujihakikisha
kuwa tumetakata kabla ya kampeni yetu ya usafi kuihamishia kwingine.
Tusikubali mtu yeyote kati
yetu kuiingilia kampeni hii na kutushawishi kufanya usafi nje kwa madai kwamba
ndiko kulikochafuka sana na kukuacha ndani. Kwa namna hiyo ni lazima mtu huyo
atakuwa amekalia rundo la uchafu hasiotaka uondosheke. Mtu huyo ni hatari
kwetu. Katika kampeni hii ya usafi, vita dhidi ya ufisadi, mtu wa aina hiyo
inabidi tumchukulie kama uchafu na pengine kutulazimu kumsafisha pamoja na
uchafu wake. Bila kufanya hivyo tutakuwa tunajisumbua na kupoteza nguvu zetu
bure, kusafisha nje tukiuacha uchafu ndani.
Hii ni kwa sababu nchi yetu
ilivyo hakuna namna yoyote ambayo watu wa rangi fulani, hususan wenye rangi ya
asili ya nje, wanavyoweza kufanya ufisadi unaohatarisha nchi bila ya kuwa na
mwongozo wa watu wenye asili ya ndani.
Hicho ni kitu kisichowezekana.
Ushauri wa kuwasakama watu wa rangi fulani tu kuwa ndio wanaoihatarisha nchi
kiufisadi nauona kuwa ndio hatari zaidi kuliko hata huo ufisadi uanotajwa.
Nasema hivyo nikizingatia ushahidi ambao umeishajionyesha ambapo watu wenye
asili ya nje wameishaishinda serikali mahakamani mara kadhaa na kuamuriwa
serikali iwalipe mara nyingi ya kiasi wanachokuwa wanatuhumiwa nacho. Hiyo
ndiyo sababu inayonifanya niuone ushauri
wa aina hiyo kuwa ni wa hatari kwa nchi yetu.
Endapo serikali itauzingatia
ushauri huo si ajabu Hazina ya nchi ikawa inafanya kazi ya kulipa tu fidia huku
kila kitu kikiwa kimesimama. Kwahiyo vita yetu dhidi ya ufisadi ni lazima
tuipeleke kwa uangalifu tusije tukajikuta tunaiingia kwenye mtego wa adui na
kuangamizwa sote, au tukafanya uzembe kama huu unaotaka kujitokeza tukaishia
kujilipua wenyewe.
Pia wapo wenye ushauri wa
kwamba tunapowasaka mafisadi tusiangalie maisha binafsi ya mtu, huu ni ushauri
wa ajabu! Maana kwa kuufuata ushauri wa aina hiyo inabidi hata vita hii ya ufisadi tuachane nayo kwa vile
ufisadi umejificha ndani ya maisha binafsi ya watu. Hakuna anayefanya ufisadi
kwa ajili ya umma. Kila ufisadi unalenga katika maslahi binafsi dhidi ya
maslahi ya umma.
Namalizia kwa kusema kwamba
nimelazimika kuonyesha msimamo wangu baada ya makala yangu moja kuwa
imewapotosha watu nakuonekana mimi naunga mkono ubaguzi wa rangi kitu ambacho
kwangu ni mwiko.
Nasema kwamba vita dhidi ya
ufisadi inapaswa kupiganwa kwa kuwalenga tu maadui, ufisadi na mafisadi, bila
kuangalia rangi zao, makabila yao, wala madhehebu yao. Anayejaribu kutushawishi
kuwa rangi fulani ndiyo ya ufisadi inabidi tumuogope kama ukimwi. Maana sumu
hiyo ikishatuingia haitutoki asilani, nchi itakuwa imeugua ukimwi wa aina yake.
Inabidi tumpuuze huku tukijiuliza lengo lake ni lipi hasa? Isije ikawa
anatutishia papa ili tupande mgongoni kwake tukidhani ni kisiwa salama kumbe ni
nyangumi anayetaka azame na kutuzamisha wote.
0784 989 512