RIDHIWANI KUWA MTOTO WA RAIS HAVUI HAKI YAKE YA URAIA
Na Robert Mdoe
WANA CCM wa
jimbo la Chalinze wamempendekeza Ridhiwani Kikwete kuwa mgombea ubunge wa jimbo
hilo kwa tiketi ya chama chao. Ni katika
uchaguzi mdogo utakaofanyika jimboni humo kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa
jimbo hilo, Saidi Bwanamdogo.
Baada ya jina
la Ridhiwani kutangazwa kuwa kashinda kura za maoni, tena kwa kishindo, ili
kupeperusha bendera ya chama chake
katika uchaguzi huo mdogo, maneno yameanza kutoka kona mbalimbali kuwa huyo
kapata nafasi hiyo kwa vile ni mtoto wa
kigogo, mtoto wa rais aliye pia mwenyekiti wa CCM! Wengine wakisema kwamba kwa vile Kikwete amewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo hivyo
haikufaa mwanae naye awe mbunge wa jimbo hilohilo eti katika kuliepusha
lisionekane linaongozwa katika mfumo wa kiukoo!
Makala
nyingi zimeandikwa katika magazeti mbalimbali zikikishangaa na nyingine
zikikilaani kitu hicho cha Ridhiwani kupendekezwa na wanachama wa chama chake
kuwa mgombea wao katika jimbo hilo.
Kuna makala
niliyoisoma katika gazeti la kila wiki ikisema “Ridhiwani, Mgimwa na ujio wa
nepotism Tanzania”. Makala hiyo inausakama ugombeaji wa Ridhiwani ikiufananisha
na undugunaizeisheni ambapo mambo hufanyika kwa kufuata mkondo wa undugu.
Katika makala hiyo wanatajwa pia watoto wa vigogo walioajiriwa katika sehemu
nyeti hapa nchini katika kuushadidia
undugunaizeisheni ambao mwandishi huyo anaufananisha na kitendo cha wana CCM wa
Chalinze kumpigia kura za maoni Ridhiwani ili akawe mgombea wao.
Makala
nyingine ilisema “Nateta na watoto wa marais wetu”. Hiyo inamsema Ridhiwani kwa
staili tofauti, kwamba kwa nini akiwa mtoto wa rais anaonekana kutajwatajwa
sana akihusishwa na mambo mbalimbali ukiwemo ukwasi wa kutisha unaosemekana
anaumiliki katika umri wake mdogo, tofauti na watoto wa marais wengine
waliomtangulia baba yake kwenye kiti hicho cha enzi. Lakini hata hivyo naye
huyo anasema hayo yote kutokana na wana CCM wa Chalinze kumchagua Ridhiwani awe
mgombea wao.
Kutokana na
maneno hayo yanayosemwa dhidi ya kijana huyo, mtoto wa rais, namimi nimeona
bora nichangie kidogo kujaribu kuweka mambo katika usawa wake, kusudi isijekuwa
wivu, kinyongo, chuki nakadhalika, vinachukua nafasi ya kuwashawishi wananchi
kwa njia ya upotoshaji vikionyesha kuwa ndivyo vilivyo sahihi.
Ridhiwani
Kikwete ni mtoto wa rais, sawa, lakini vilevile ni raia kama walivyo raia
wengine wote. Anayo haki ya uraia kama waliyo nayo wengine, kama mimi na wewe
tulivyo. Sababu hakuna mahali popote palipoandikwa kwamba ukiwa mtoto wa rais
haki zako nyingine za urai unazipoteza. Mpaka hapo sidhani kama ameishatoka nje
ya mstari.
Undugunaizeisheni
unaotajwa sielewi unaingiaje hapo. Kama pengine angetajwa tu kuwa sasa
Ridhiwani Kikwete ndiye mbunge wa Chalinze pasipo kufuata taratibu za uchaguzi,
hapo kweli hata mimi ningefikiria vingine. Lakini kagombea sawa na wengine,
wanachama wamepiga kura za maoni na kumpendekeza kwa kishindo, sasa
undugunaizeisheni unatoka wapi? Ina maana wanachama wote wa Chalinze waliopiga kura za maoni ni jamii ya Kikwete?
Kitu kingine
ni kwamba Ridhiwani ni kijana tena msomi, mwanasheria. Bilashaka atakuwa nayo
matamanio ya ujana kama waliyo nayo vijana wengine. Ispokuwa yeye kama kijana
msomi matamanio yake yatakuwa yanatofautiana na ya vijana ambao hawana kisomo
kama alicho nacho yeye. Hivyo si kwamba kila kijana atatamani kuwa mbunge, la hasha,
kila mmoja anapatamani anapopaweza. Hivyo Ridhiwani kuutamani ubunge ulio
kwenye uwezo wake, kiusomi, kuna tatizo gani?
Ni pale tu
kama angeutamani ubunge wakati tukielewa kuwa hauwezi, ambapo na mimi ningejiuliza
maswali ya kwamba imekuwaje kitu kama hicho kikatokea. Na kama hali
ingeendelea, mchakato wa ubunge, katika hali hiyo inayoonyesha kwamba ubunge
hauwezi, basi undugunaizeisheni ungekuwa umejitokeza katika picha ya rangi.
Pamoja na
Ridhiwani kuwa kijana msomi, mtoto wa rais, kizuri zaidi ni kwamba
anajichanganya sana na watu bila kujali usomi wake wala utoto wa rais. Hana
maringo yanayomfanya awabague watu kwa kufuata ni watu wa sampuli gani.
Na kawaida
ya binadamu hupendelea kutumia kila nafasi inayopatikana kuwa karibu na
wakubwa, kimazingira mtoto wa rais ni mtu mkubwa, kwa vile anatoka katika familia ya kwanza
katika nchi, familia ambayo waingereza
wanaita “first family”. Nafasi hiyo kwa Ridhiwani imewekwa wazi, kila anayetaka
kuitumia ni ruksa ili awe karibu naye.
Kwahiyo
inapotokea watu wakawa wanamsemasema sana sio kwamba wanamsema kwa ubaya, kama
wengine wanavyotaka kupotosha, hapana, wanamsema kwa vile wanamuona,
wanamuelewa, anajichanganya nao bila kuwabagua ilhali wakielewa kuwa sio mtu wa
kada yao, yeye ni mtu kutoka kwenye familia ya kwanza hapa nchini. Je, watu
kumsema kwa hilo la kujishusha chini na kuwa sawa na wao, linamfanyaje yeye
aonekane ana makosa?
Ikumbukwe
kwamba hiyo ni tofauti na watoto wengi wa marais wengine ambao watu walikuwa
hawawaoni na kuwafahamu, pengine kutokana na watoto hao kutopenda kujichanganya
na watu wakijiona wao ni matawi ya juu.
Kuhusu
ukwasi unaosemekana Ridhiwani anao, sijui kuna ushahidi gani kuhusu hilo.
Sababu karibu wote wanaosema Ridhiwani ana utajiri wa ajabu najua wanasemea
hisia tu kwa vile hilo ni jambo gumu kulithibitisha.
Mfano,
niliwahi kuwa mahala, mikoani, ndugu yangu mmoja akawa anakitaka kiwanja fulani
kilichokuwa wazi pasipo na nyumba yoyote, tena katika eneo zuri. Ni moja ya
viwanja vya manispaa vilivyokuwa vinagawiwa kwa ajili ya ujenzi wa kamazi ya
watu.
Tulipokifuatilia
mpaka makao makuu ya manispaa tukakuta kimeandikwa jina la Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, kuwa ndiye anayekimiliki. Kwa waliokuwa
hawamwelewi mtu huyo walijua kuwa kweli ndiye anayekimiliki, na kuna waliosema
kwamba mtu huyo ni tajiri sana aliyejimilikisha viwanja kila kona ya nchi kwa
kutumia cheo chake.
Kumbe mambo
hayo yanafanywa na matapeli wanaofanya kazi kwenye manispaa. Wanatumia njia
hizo za kuvipachika viwanja majina ya watu wakubwa kusudi viwanja hivyo
visiguswe na hata vigogo wa mikoa, ambao katika hali ya kwaida ni vigumu
kuwazuia kupata sehemu wanazozihitaji, ili baadaye wao hao matapeli waje
waviuze kwa bei ya juu sana. Sioni jambo kama hilo haliwezi kufanyika kwa
kutumia jina la Ridhiwani Kikwete linapokuja suala hilo la ukwasi wake.
Kuhusu
Ridhiwani kugombea ubunge, sioni tatizo lolote katika hilo. Hiyo ni haki yake
ya kiraia. Pengine kama kuna wanaosema kwamba yeye sio raia wa nchi hii. Lakini
kwamba yeye ni mtoto wa rais, hicho ni kichekesho. Maana kama nilivyosema
awali, kuwa mtoto wa rais hakumvui mtu haki zake za kiraia.
Na kwamba
baba yake alikuwa mbunge wa jimbo lilelile halafu akawa rais, ni hoja isiyo na
mashiko sababu ikiangaliwa vingine itaonekana inajipinga yenyewe.
Mfano ni
watoto wangapi ambao wazazi wao wote wawili, baba na mama, ni walimu au hata
mmoja wao, halafu wakatokea watoto wao wawili na hata watatu, nao wakawa
walimu? Je, kuna swali linaloulizwa kwa nini inakuwa hivyo?
Vivyohivyo
kwa madaktari, wanasheria, polisi, wawindaji na hata wavuvi. Sababu mara nyingi
kazi za wazazi huwa zinawatamanisha watoto kuzifuatilia kama watoto wanayo
mapenzi ya dhati kwa wazazi wao. Ni mara chache sana watoto kukosa kufuata
mkondo wa wazazi wao. Anayelishangaa hilo bora akapimwe akili zake kwanza.
Ndiyo maana
tunaona watoto wengi ambao wazazi wao ni wanasiasa au walikuwa wanasiasa nao
wanatamani kuwa wanasiasa.
Kwahiyo hili
la Ridhiwani kamwe haliwezi kufananishwa na la watoto wa vigogo wanaoajiriwa
kwenye sehemu nyeti za nchi. Kuajiriwa kunaweza kutokana na maelekezo, (…..
muajirini mtoto wangu au mtoto wa fulani). Kamwe lugha ya aina hiyo haiwezi
kutumika katika suala kama hili la Ridhiwani kugombea ubunge. Hakuna anayeweza
kuwaamrisha wananchi wamchague mtoto wake awe mbunge wao. Kinachoamrisha ni
mienendo ya Ridhiwani iliyokubaliwa na wapiga kura, basi.
Tena katika
kulifuatilia hili nimegundua kuwa Ridhiwani kashawishiwa na kuombwa na wana
Chalinze ili akachukue fomu na kugombea ubunge kwa ahadi kuwa watampa kura
akawe mbunge wao. Sidhani kama baba yake anahusika katika hilo.
Kitu
alichokuwa anaweza kukifanya baba yake, kilicho kwenye mamlaka tuliyomkabidhi
kama rais, kilikuwa ni kumteua Ridhiwani awe mbunge na kisha amfanye kuwa
waziri kama angetaka. Lakini hakufanya hivyo. Sasa wanaomsakama rais kwa mambo
ambayo pengine hayaelewi wana maana gani?
Nitamshangaa sana Rais Kikwete, pale atakapokaa
kama mwenyekiti wa CCM na kulifanya jina la mwanae liondolewe kwenye kinyang’anyiro
cha ubunge wa Chalinze, kama anavyoshauriwa na baadhi watu wanaomsakama bila
hatia yoyote, wakati wananchi wa Chalinze wakiwa tayari wameishaonyesha nani
wanamtaka awe mbunge wao. Kusema ukweli atakuwa hajawatendea haki.