UBABE,UKOSEFU WA HOJA NA HEKIMA VINAIPELEKA NCHI KUZIMU!
Na Prudence Karugendo
TANZANIA,
tangu ikijulikana kama Tanganyika, imejivunia amani na utulivu kiasi cha
kujiita kwa mbwembwe kuwa ni kisiwa cha amani, kama ilivyo kwa kisiwa cha
kijani katikati ya jangwa.
Lakini
hatahivyo, amani na utulivu si vitu ambavyo tunaweza kudai kuwa vinatudondokea
tu kutokana na Mungu kutupendelea, vitu hivyo vinatengenezwa na sisi wenyewe
katika mfumo tulioamua kuuishi. Katika jamii yoyote iwayo kutendeana haki,
uongozi kujiepusha na ubabe pamoja na kuwa na uwezo wa kujenga hoja
zinazowashawishi wanajamii kutokuwa na
fikra za kuanzisha vurugu, ni mambo muhimu na nyeti katika kuifanya jamii
husika iwe na vitu hivyo, amani na utlivu.
Ukosekano wa
vitu kama haki, hekima, busara na kutopenda kuonyesha ubabe katika jamii, ni
mwanzo wa vurugu zinazoweza kuipeleka nchi yoyote katika maangamizi. Ni kwa
sababu hakuna mwanadamu aliye tayari kuuona ukosekano huo ukitamalaki na yeye akavumilia
hali hiyo hata awe mnyonge kiasi gani.
Nchi yetu,
Tanganyika, kwa mfano, ilijaaliwa kupata
uongozi wenye hekima na uwezo wa kujenga hoja hata kabla ya kujitawala yenyewe.
Ikumbukwe
kwamba Tanganyika iliondolewa kwenye ukoloni baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia
iliyoisha kwa mkoloni wake, Ujerumani, kusalimu amri mwaka 1918. Baada ya hapo
Tanganyika ikawekwa chini ya uangalizi wa Jumuiko la Mataifa (League of
Nations), kabla ya Umoja wa Mataifa (United Nations) na kazi hiyo ya uangalizi ikaachiwa ifanywe na
Uingereza.
Lakini
baadaye Uingereza ikanogewa na kuigeuza Tanganyika koloni lake ambalo lakini haikulijali sana
kama yalivyokuwa makoloni yake mengine.
Wakati
tumeanza kudai uhuru ili tujitawale sisi wenyewe, Baba wa Taifa, Mwalimu
Nyerere, bingwa wa kujenga hoja, alitamka kwamba Waingereza walipaswa kutuachia
uhuru wetu sababu sisi hatukuwa koloni lao, kwamba kama wangeng’ang’ania
tungewashitaki Umoja wa Mataifa. Na endapo kule tusingesikilizwa basi
tungewashitaki kwa Mungu!
Nilibahatika
kupata fursa ya kumuuliza Mwalimu alikuwa na maana gani kwa kauli yake hiyo ya
kuwashitaki Waingereza kwa Mungu, akanifafanulia kwamba ilikuwa na maana ya
kushika silaha kisha kuingia msituni na kuudai uhuru wetu kwa nguvu. Akaongeza
kwamba alipolifikiria hilo la kushitaki kwa Mungu machozi yakamtoka.
Kwa upande
mwingeni, wenzetu wa Zanzibar waliamua kushitaki moja kwa moja kwa Mungu,
mashitaka yao yakakubaliwa, na ndiyo Mapinduzi ya mwaka 1964. Pengine ndiyo
maana yanaitwa Mapinduzi Matukufu mpaka sasa.
Kwa upande
wa Tanganyika hoja za Mwalimu zilikuwa na nguvu sana kuliko hata risasi, hivyo
hakukuhitajika silaha, Waingereza wakanywea na kutuachia uhuru wetu. Uhuru bila
kumwaga damu, jambo lililo nadra sana.
Lengo la
makala hii ni kuonyesha kwamba uongozi unapokuwa na hoja unaiepusha jamii
unayoiongoza na upelekaji wa mashitaka kwa Mungu. Sababu gharama yake ni kubwa
mno. Ndiyo maana machozi yalimtoka Baba wa taifa alipolifikiria hilo. Ila
bahati nzuri ujenzi wake wa hoja ukaipusha nchi na kitu hicho.
Kitu kingine
ninachotaka kukiangalia hapa ni kuhusu viongozi kutenda haki. Inapotokea
uongozi wa nchi ukashindwa kutenda haki, jamii inayoongozwa au sehemu yake,
inajikuta ikilazimika kupeleka mashitaka kwa Mungu. Hiyo ni kwa sababu kote
ambako mashitaka husika, ya kukosekana kwa haki, yangepelekwa kunatokana na
uongozi ulioshindwa au kutotaka kutenda haki.
Maana baada
ya uongozi au utawala kutotaka kutenda haki kinachofuatia ni ubabe wa kuwafanya
wanaonyimwa haki zao wanyenyekee na kuutii utawala husika. Jamii itatawaliwa
kadri ya matakwa ya watawala yalivyo. Na katika kuitawala jamii yoyote ubabe wa
aina hiyo lazima uwe na mwisho wake. Kamwe mwisho huo hauwezi kuwa mwema hata
siku moja. Mara nyingi huo unakuwa ni mwisho wa kimaangamizi.
Tunaweza
tukajikumbusha baadhi ya matukio yaliyotokana na ubabe katika utawala. Nchi ya
Uganda iliwahi kuwa na mtawala mbabe, Idd Amin Dada. Ubabe wake ulifurika
Uganda nzima na kulazimika kusambaa mpaka Tanzania, huku yeye akijiita, pamoja
vituko vingine, kuwa ni rais wa maisha wa nchi hiyo!
Ndipo
Tanzania ikalazimika kupeleka mashitaka kwa Mungu, ikaingia vitani ili kujinusuru na
ubabe pamoja na vituko vingine vya mtu
huyo. Maisha ya baadhi ya wananchi na askari wa pande mbili, Tanzania na
Uganda, yakateketea zikiwemo mali na miundombinu. Lakini ubabe wa mtawala huyo
ukakomeshwa ila kwa gharama hiyo kubwa.
Mbali na
hiyo, tumeshuhudia ubabe wa mtawala wa Irak, Saddam Hussein, ulivyokomeshwa na
kuiacha nchi hiyo haitamaniki. Mpaka leo nchi hiyo imeshindwa kutulia na kubaki
ikionekana kama jahanamu, mahali pa kusadikika ni pachafu, kiimani.
Lakini kama
hekima ingemtokea mtawala huyo, akaachana na ubabe, hali ya mambo nchini Irak
isingekuwa kama ilivyo kwa sasa, na pengine yeye ingemsaidia kuyanusuru maisha
yake.
Vilevile
tumeona jinsi uvumilivu ulivyowaishia wananchi wa Tunisia baada ya watawala wao
kushindwa kutenda haki, kukosa uwezo wa kujenga hoja, badala yake wakaendekeza
ubabe. Wananchi wakaamua kupeleka malalamiko yao kwa Mungu. Na kawaida Mungu
hawatupi mkono waja wake.
Vivyo hivyo
nchini Misri na nchini Libya. Kule Libya, pamoja na mema yote aliyoyafanya, Muamar
el Gadaffi, kwa wananchi wake, lakini ubabe wake wa kuwanyima watu wake haki ya
kujifanyia maamuzi umemgharimu maisha yake baada ya wananchi hao kufikisha
kilio chao kwa Mungu. Mpaka sasa Misri na Libya hakujatulia, na hakuna anayejua
patatulia lini.
Sudan
Kusini, nchi changa kuliko zote katika Afrika, sasahivi nayo imegeuka jahanamu!
Tamaa ya madaraka na ubabe wa viongozi wa nchi hiyo vinavy ochochewa na ukosefu
wa uwezo wa kujenga hoja vimegeuka kiama kwa wananchi. Maisha ya watu
yanateketea, wale ambao bado wamenusurika wako katika shida isiyosemekana!
Kule Afrika
ya Kati tunaona jinsi ubinadamu ulivyopotea kabisa. Binadamu wanaendesha maisha
ya kutisha kuliko hata ya wanyamapori! Fikiria mtu anamuua mwenzake, anamkata
mguu na kuanza kuutafuna hadharani! Hayo yote yanasababishwa na uongozi au
utawala mbovu, utawala ulioishiwa hekima na uwezo wa kujenga hoja
zinazokubalika kwa watu.
Syria nako
kumegeuka jahanamu! Utu umepotea, watawala wanawaza kutawala tu bila kujali
maisha na uhai wa wananchi ukoje. Watu wanakufa kama sisimizi, watawala wanaona
cha muhimu ni kulinda tu utawala wao, acha watu wateketee, kinacholindwa ni
utawala, sio watu!
Tunapoyaangalia
yote hayo bado sisi Tanzania tunaamini kwamba tuko hivi tulivyo, amani na
utulivu, kutokana na Mungu kutupendelea! Mpaka viongozi wetu wanafikia kutoa
kauli za ajabu bila kujali ni madhara gani yanaweza kutokana na kauli hizo! “……mimi
nasema wapigwe tu maana tumechoka…..”! Hakuna kujiuliza kwamba wanaoamriwa
wapigwe wakiamua kusema hapana, nasi tumechoka, kinachoweza kufuatia ni nini!
Sababu
wananchi wakishasema hapana, hatukubali kupigwa tu, elewa kwamba kauli hiyo ya
umma tayari iko kwa Mungu. Yanayoweza kufuatia waziri mkuu anakuwa hayawezi
tena. Anachoweza kufanya ni kukaa akijutia kauli yake ya wapigwe tu.
Wahaya
wanasema “ekiruga kanwa tikishubamu” wakimaanisha kwamba kitokacho kinywani
hakirudi tena kinywani, kwa maana ya kwamba hakifutiki.
Mara hii
mwenyekiti wa chama tawala, rais na Amiri Jeshi Mkuu, anawambia wanachama wake
kwamba wasiwe wanyonge, eti wajibu mapigo ya wapinzani! Anatoa mifano ambayo
naamini kwamba kapewa maelezo ya kuchongwa na wasaidizi wake. Eti ndiyo iliyomfanya akafikia kutoa
kauli hiyo.
Mwenyekiti
wa CCM anasema kwa uhakika kana kwamba aliwaona waliotenda anayoyatolea mifano.
Ila hasemi yeye akiwa rais, kwa nini hakuamuru waliohusika na matukio
anayoyataja, kama ya kutobolewa macho kwa bisibisi pamoja na kumwagiwa
tindikali, wakamatwe mara moja, kama walionekana na kujulikana kuwa ni
wapinzani, ili wakafikishwe kwenye vyombo vya sheria. Kama hilo halikufanyika
kwa nini aendelee kuwa na uhakika kwamba waliohusika ni wapinzani?
Lakini
hatahivyo mwenyekiti wa chama tawala, CCM, hasemi lolote kuhusu mashambulizi ya wazi
yanayofanyika dhidi ya wapinzani! Mbali na anayesemekana kutobolewa macho na
mwingine kumwagiwa tindikali, mwenyekiti wa CCM haonekani kukumbuka kuwa
Chadema walishambuliwa kwa bomu la kivita wakiwa kwenye mkutano wa hadhara,
bomu lililoua baadhi ya watu na kujeruhi wengine kadhaa Mjini Arusha!
Hakumbuki
jinsi Polisi wanavyotumia nguvu ya ziada kusambaratisha mikusanyiko halali ya
vyama vya upinzani, mfano kule Morogoro ambako risasi za moto zilitumika moja
ikimuua kijana muuza magazeti aliyekuwa hahusiki na mkusanyiko halali wa
Chadema!
Mwenyekiti
wa CCM haongelei chochote kuhusu fujo zilizodhamiriwa na aliyekuwa Mkuu wa
Polisi (RPC) mkoani Iringa, Michael Kamuhanda, na fujo hizo kuishia kwa mauti
ya mwanahabari, Daud Mwangosi, kijijini Nyololo, Mfindi, Iringa.
Swali la
muhimu kujiuliza ni kwamba, kama kweli wapinzani wanafanya fujo inakuwaje Amiri
Jeshi Mkuu awambie CCM wajilinde na kujibu mashambulizi? Ina maana kalifuta
Jeshi la Polisi? Au anayoyaona yakifanywa na vikundi vya Seleka na Ati-balaka kule
Afrika ya Kati anaona kuwa ndiyo
yanayofaa?
Je, Jumuiya
ya kimataifa, ambayo muda wote inahangaika kwa hali na mali kupatanisha penye
machafuko, hasa haya ya kujitakia, inapomsikia JK akitoa amri ya aina hiyo
kweli itaendelea kumuona kama mtu aliyedhamiria kukomesha machafuko na kuleta
upatanishi katika nchi nyingine wakati kwake akiyaandaa machafuko ya aina
ileile?
Nimalizie
kwa kusema, vyovyote iwavyo tuelewe kwamba hoja na hekima ndio mhimili wa amani
na utulivu wetu. Tunapoviacha vitu hivyo vitoweke kinyemela basi hatunabudi
kuelewa kuwa tumejiweka njiapanda ya kuelekea kuzimu.
0784 989 512