UZINDUZI WA JK WATUBADILISHA WENGI MTAZAMO
Na Bernard Kazinduki
KABLA ya uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba,
uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete siku ya Ijumaa, 21 / 3 / 2014, kichwa changu kilikuwa
kimejaa mambo mengi juu ya mustakabali wa nchi yetu.
Kabla
sijaeleza mengi kwanza nijitaje kuwa mimi ni mpinzani. Sikubaliani kabisa,
kiitikadi na kisera, na chama
kinachotawala hapa nchini kwetu, CCM, kutokana na haya nitakayoyaeleza hapa
chini.
Naamini
kwamba kuendelea kutawala kwa CCM kunaifanya nchi yetu iendelee kudumaa. Sababu
chama hicho kimeitawala nchi yetu kwa zaidi ya miaka 50, lakini nchi bado
inaitwa changa! Wakati huohuo chama hicho kinajidai kutuonyesha mafanikio ya
kitoto ambayo tunaweza kuyafananisha na mafanikio wanayoyafurahia wazazi ya mtoto
wao mdogo kuanza kutambaa au kusimama dede!
Ikumbukwe
kwamba wakati nchi yetu inapata uhuru wake toka kwa wakoloni, mwaka 1961,
kimaendeleo Tanganyika ilikuwa sawa na nchi ya Korea ya Kaskazini. Najua kuna
watakaoniona kichaa kuyalinganisha maendeleo ya Korea na ya Tanganyika
kulingana na tofauti iliyopo kwa wakati huu. Lakini huo ndio ukweli wenyewe.
Kwa upande
mwingine Tanganyika ilikuwa mbele kimaendeleo ikizitangulia nchi nyingi za
Mashariki ya Mbali kama Thailand, Singapore, Malaysia, Indonesia nakadhalika.
Lakini kwa sasa tofauti ya kimaendeleo kati ya nchi hizo na Tanzania, iliyokuwa
Tanganyika miaka hiyo, haitofautiani na tofauti ya ardhi na mbingu!
Ni kubwa
sana kiasi kwamba kwa mtu ambaye hakuwahi kuifuatilia tangu mwanzo akikusikia
unasema kwamba nchi hizo zilikuwa nyuma ya Tanganyika kimaendeleo wakati fulani
ni lazima akuone una kichaa.
Kwa ufupi ni
kwamba hayo yote yanasababishwa na chama tawala hapa kwetu ambacho mwanzoni
kilijulikana kama TANU, Tanganyika African National Union. Kwa tafsiri isiyo rasmi, Muungano wa Kitaifa
wa Waafrika wa Kitanganyika.
Ila miaka 15
baadaye, mwaka 1977, baada ya uongozi wa chama hicho kujiridhisha kuwa
kilichokuwa kimelengwa kimeishapatikana, uongozi ukaushawishi uongozi wa chama
kingine cha ASP, upande wa Visiwani, kwamba vyama hivyo viungane na kutengeneza
chama kimoja. Ndipo kikaundwa Chama Cha Mapinduzi, CCM.
Mpaka leo
sijaelewa jina hilo la CCN lina maana gani. Sielewi ni kitu gani kinapinduliwa
kiasi cha kuliona neno hilo linafaa kuwa jina la chama kinachotawala nchi ya
kidemokrasia. Ila kwa kuyaangalia mambo yalivyo nalazimika kuhisi kwamba
pengine kilicholengwa kupinduliwa na chama hicho ni mafanikio yaliyopatikana
katika kipindi hicho cha miaka 15 tangu nchi ilipopata uhuru wake mpaka mwaka
kilipoanzishwa chama hicho, huku kaulimbiu ikiwa kwamba chama kimeshika hatamu,
sawa na mpanda farasi.
Mara zote
mpanda farasi ndiye huwa anashika hatamu, asipofanya hivyo ni lazima ataanguka
wakati farasi akiendelea na safari zake.
Hayo
tuyaache. Lengo la makala hii ni kutaka kumpongeza mwenyekiti wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete, kwa hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba.
Kusema
ukweli watu wengi wa upande wa upinzani, nikiwemo mimi, tulikuwa tunaichukulia
hotuba hiyo ya rais kama ufagio wa kukifagilia chama chake ili katiba
itakayoandikwa na Bunge Maalumu ikijengee mazingira ya kuendelea kudumu
madarakani, hasa baada ya baadhi ya kanuni za Bunge hilo maalumu kutenguliwa,
kwa namna ambayo zilionekana zimevunjwa makusudi, ili Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba, atangulie kuwasilisha Rasimu
ya pili ya Mabadiliko ya Katiba ndipo rais aje kulizindua Bunge.
Kilichosababisha
kukawepo na mashaka juu ya uzinduzi huo ni utaratibu uliotumika wa kutengua
kanuni iliyokuwa ikisema kwamba Bunge litazinduliwa kwanza ili Warioba
awasilishe Rasimu katika Bunge ambalo tayari linafanya kazi, kwa maana ya
kwamba tayari limeishapewa dhamana ya kufanya kazi ya kuichambua rasimu.
Lakini sasa
kilichofanyika ni kama Warioba aliwasilisha Rasimu katika kitu tunachoweza
kukiita “kijiwe”, mkusanyiko ambao haukuwa rasmi. Ni kwamba aliwakabidhi Rasimu
watu ambao walikuwa hawajapewa rasmi majukumu ya kuichambua Rasimu hiyo, watu
ambao bado walikuwa wanajiandaa kutengeneza Bunge Maalumu. Lile lilikuwa
halijawa Bunge kwa sababu lilikuwa halijazinduliwa.
Jambo hilo
liliwafanya wapinzani, nikiwemo mimi, pamoja na wale wanaounda UKAWA, Umoja wa
Katiba ya Wananchi, wajawe mashaka ya kwamba mpango huo ulilenga kuyazima yale
yaliyokuwa kwenye maelezo ya Warioba kuhusu Rasmu ya Katiba Mpya.
Hata kwa
upande wa CCM, wapo ambao inaonekana hawaelewi kilichowapeleka Dodoma, watu
wasioutilia maanani mustakabali wa nchi yao. Wao walidhani JK anakwenda Dodoma
kumpiku Warioba ili suala zima la Katiba Mpya liwe la kukilegezea mambo chama
chama chao. Mawazo yao hayalengi hata kidogo katika kuinufaisha nchi ispokuwa
chama tu!
Lakini ajabu
rais alipopanda kwenye mimbari pale Bungeni akauvua ukada wa chama chake na
kuutupa pembeni na kubaki tu na uzalendo wa nchi yake! Kusema ukweli sikuuona
ukada wa Kikwete kwenye hotuba yake isipokuwa nilikuwa nauona uzalendo tu.
JK
alisisitiza kwamba katika tume 4 zilizotangulia suala la Muungano lilikuwa
linajitokeza likionyesha matatizo ya kiufundi yaliyohitaji marekebisho. Tume zote
4 zilishauri marekebisho hayo yafanyike kwa Jamhuri ya Muungano kuwa na
serikali 3. Lakini mara zote serikali hizo 3 zikawa zinashindikana na kubaki na
serikali 2 tu, jambo lilisababisha tatizo au “kero za Muungano” kubaki
palepale.
JK akawahimiza
wajumbe wa Bunge Maalumu kwa kuwashauri kwamba mara hii wajaribu kulimaliza
kabisa tatizo hilo. Baadhi ya wajumbe wa CCM, ambao naamini hawakumuelewa,
wakidhani anaongea kichama, waliinuka kwenye viti vyao wakishangilia kwa vile
walishajipanga kufanya hivyo ili kuwakomoa wapinzani!
Lakini mimi
mpaka hapo niliona kuwa JK anakubaliana na serikali 3. Sababu kama tume 4
zimeshindwa kuliondoa tatizo kwenye Muungano baada ya ushauri wake wa serikali
3 kutupiliwa mbali, sasa mara hii JK anasema wajitahidi kulimaliza, ana maana
gani kama sio kwamba tujaribu na serikali 3 ili tuone?
Sababu kwa
kauli yake hiyo alionyesha wazi kwamba hakuna namna yoyote ambayo ingeweza
kulimaliza tatizo lililoshindikana katika tume 4, isipokuwa ni kukubaliana na
serikali 3.
Ila akatahadharisha
kwamba kwa kufanya hivyo, kuzikubali serikali 3, ni kuwa tayari kuachana na
Muungano. Akatoa mfano ulio hai wa uliokuwa Muungano wa Urusi pale kila jimbo
lilipokubaliwa kuendesha mambo yake kivyake na juu kukiwepo na serikali kuu ya
muungano.
Akasema
kilichotokea ni serikali kuu kujikuta haina nguvu wala mamlaka katika
mabadiliko hayo ya Perestroika na Glasnost, wakati kila jimbo lilipogeuka kuwa nchi
kamili. Na huo ndio ukawa mwisho wa muungano mkubwa wenye nguvu sana wa Urusi.
Kwahiyo rais
alichokimaanisha hapo ni kwamba iwapo Katiba itasema Tanzania iwe na serikali 3
Muungano utakuwa haupo tena. Nadhani kwa mtu yeyote ambaye ni muumini wa
muungano huu, kama alivyo yeye rais aliyekalia kiti cha mmoja wa waasisi wa Muungano
huo, asingependa kuona muungano unamfia mikononi mwake kama ilivyotokea kwa
Mikhail Gorbachev wa Urusi. Bilashaka JK anaogopa historia isije kumhukumu.
Wakati
huohuo wapo waliokuwa wakisema kwamba rais alichotakiwa kukifanya ni kufungua
Bunge na kuondoka zake! Lakini eti badala yake akaanza kuchambua Rasimu. Kwa
upande wangu naona kwamba rais ambaye angefungua Bunge na kuondoka zake
angekuwa anafanya kama Wahaya wasemavyo kwamba “Birangw’enyuma”, usemi
unaoonyesha kutokujali, kwamba potelea mbali yatakayotokea sitakuwepo.
Lakini rais
anayejali ni lazima angefanya kama alivyofanya JK. Sababu naye, akiwa raia wa nchi
hii, hiyo ilikuwa nafasi yake, kuchangia
namna anavyoona Katiba ya nchi yake inafaa kuwa. Sidhani kama Jaji Warioba
aliwahi kuchukua maoni yake kabla. Ndiyo maana kila JK alipokuwa anamaliza kuongea anawambia wajumbe
kuwa hayo ni maoni yake wao wataamua ni kipi wakifuate na kipi wakiache.
Nimalize kwa
kusema kwamba kwa vyovyote ilivyo Rais Kikwete amenishawishi niwe upande wa
serikali 2. Nadhani atakuwa pia amewashawishi watu wengi kwa njia hiyo. Ndiyo
maana akawashauri wajumbe kwamba watumie nguvu ya ushawishi kuliko nguvu ya
kulazimisha katika kuunda Katiba Mpya.