WALIOWAJIBISHWA MAGATA- MULEBA WAANZA KUVURUGA SHUGHULI ZA KCU (1990)LTD
Na Deogratias
Kishombo
SASA ni dhahiri kwamba baadhi ya kikundi kidogo cha
waliokuwa viongozi wa chama cha msingi cha Magata katika Wilaya ya Muleba ambao
wamewajibishwa na bodi ya Chama kikuuu cha Ushirika mkoani Kagera (KCU 1990
ltd) kutokana na utovu wa nidhamu kwa kukiuka masharti ya msingi ya kilimo hai
(organic) kwa kununua na kuingiza kahawa ya kawaida (conventional coffee)
wameanza kuvuruga wanachama na ushirika wa mkoa.
Wameanza kuvuruga ushirika kwa kutumia baadhi ya vyombo vya
habari wakitaka kuwashawishi wakulima kujitoa katika chama kikuuu cha msingi
mkoani hapa cha KCU (1990) Ltd kitendo ambacho kimeanza kuwaacha wanachama wa
Magata njiapanda. Wanachama wanasema hawataki kuburuzwa.
Wakati serikali ya Wilaya ya Muleba chini ya Afisa Ushirika
wa wilaya hiyo Bwana Malelo Magoma ikisema hakuna taarifa rasmi ya kujitenga
kwa chama hicho, kiongozi wa kikundi hicho cha wanaotaka kujitenga Bwana
Yusufu Kakwata huku akijua kwamba anakiuka baadhi ya vifungu
vya sheria ya ushirika anasema lazima wajitenge.
Baadhi ya wanachama na viongozi waliohojiwa na mwandishi wa
makala hii wanasema hao wanaotaka kujitenga hawana nia njema na ushirika wa
Kagera wakisema kwamba ushirika wa Kagera umefanya mambo mengi na umeleta
manufaa kwa wanachama na umekuza uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.
Wanaenda mbali kwa kusema kwamba hicho kikundi cha akina
Kakwata kitaua ushirika na hakitaweza kuwasaidia wananchi walio wengi ambao
bado wana imani na KCU (1990) Ltd.
“Hatuna imani na hatuwezi kuwa salama kama Magata
itajitenga. Walio wengi tutapata shida tu hasa sisi wakulima wa kawaida ambao
tumekuwa kwa muda mrefu tukitegemea KCU (1990) Ltd” anasema Amrati Siraji, Mwenyekiti wa zamani
wa chama cha msingi cha Magata.
Anaongeza kwamba wakati akiwa Mwenyekitu wa chama hicho
amefanya mambo mengi kwa wanachama wake na wanachama wengi walikuwa na imani
naye lakini baadae alikuja kushangaa kuondolewa kwa mizengwe na kundi
linalotaka kujitenga.
“Sasa hivi wakulima tuliowengi nafikiri tuwe makini na watu
hawa wanaotaka tujitenge. Nafikiri wao waondoke watuachie Magata yetu” alisema.
Naye Mbunge wa Muleba Kusini Profesa Anna Tibaijuka akiongea
na mwandishi wa habari hizi akiwa Dodoma alisema kwamba hayo maneno ameyasikia
lakini hayaungi mkono.
“Kuna kamati ya chama cha msingi ilinifuata ikitaka kupata
maoni yangu nilichowaambia kujitenga hakukubaliki. Kwanini kujitenga? Alihoji.
Profesa Tibaijuka anaongeza kwamba jambo la maana siyo
kujitenga ila muhimu ni kuangalia ni namna gani
chama kikuu cha ushirika (KCU
1990 LTD) kinaweza kusaidiwa ili kifanye
kazi zake kwa ufanisi ili kifikie malengo yake.
”Mimi naamini katika kuboresha na kusaidia ni namna gani KCU
inaweza kuwa efficient kuliko kujitenga” anasema.
Naye Veterani wa Ushirika na ambaye ni Mwenyekiti wa chama
cha msingi cha Kamachumu Mzee Karugaba Mayanja anasema hayo maneno ya kujitenga
aliyasikia kwa baadhi ya watu lakini anasema hayo mambo ya kujitenga hayana
maana.
Akiongea kwa umakini mkubwa anasema amekuwa mwenyekiti wa
chama cha msingi cha Kamachumu tangu mwaka 1988 hivyo anafahamu mambo mengi ya
ushirika hivyo hoja zinazoibuliwa hivi sasa ni kuvuruga Ushirika wa Kagera
ambao umejizoelea sifa nyingi ndani na nje nchi.
“Kwani sisi Muleba tujitenge tuna nini?. Miundo mbinu yote
ya ushirika haipo hapa. Na ushirika hauko rahisi kama watu wanavyofikiri
unahitaji mambo mengi ya msingi ambayo hapa siyaoni” alisema Mzee Karugaba.
Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii vililipoti kwamba chama cha msingi cham Magata wanataka kujitenga huku
vikisema kwamba tayari maombi ya kujitenga yameishapelekwa serikali.
Kiongozi wa kikundi kinachotaka kujitenga Bwana Yusuf
Kakwata ambaye anatajwa na wanachama kwamba yeye ndiye kinara wa kutaka kujitenga
kwa Magata anasema kwamba nia yake ya kuwashawishi wana Magata inaendelea.
“Tunaendelea na mchakato wa kujitenga” alisema.
Alipobanwa zaidi na
maswali ya waandishi wa habari waliofika nyumbani kwake alisema: “Kwanza
mlipoanza safari kuja kwangu nilijua kwamba mnakuja hivyo najua mnachokitafuta”
alisema.
Alisema kwamba sababu ya kufukuzwa kwake kutoka kwenye
ujumbe wa bodi ya KCU (1990) Ltd ni kutokana na wivu dhidi yake kwa sababu
anazalisha kahawa nyingi na kufukuzwa kwake kwenye shughuli nyingine za KCU
(1990)Ltd ni chuki binafsi.
“Mimi ni mkulima wa kahawa namba mbili kitaifa hivyo yote
yanayotokea hapa ni chuki na wivu tu wa kahawa” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na ya Mkaguzi mkuu wa
Chama Kikuu cha Ushirika Bwana Stanislaus Mutahyabarwa inaonesha kwamba orodha
ya kikundi cha wanaotaka kujitenga cha Magata ni wale wote ambao bodi ya KCU
(1990) LTD imewawajibisha kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo udanganyifu
uliofanyika Magata PCS LTD tangu mwaka 2010 hadi 2012 ambao walio wengi walikuwa
viongozi chamani.
Pamoja na makosa mengine
viongozi hao wa zamani wanatuhumiwa kuuzia chama kwa bei ya kahawa hai
wakati siyo hai na kwa njia hiyo kukiibia chama jumla ya mamilioni ya shilingi na kuleta usumbufu
katika soko la biashara ya kahawa hai
(organic coffee).
Mwisho
Mwandishi wa makala
haya ni mshauri wa habari wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera.
Anapatikana 0688 065574. E-mail: pmediaconsultancy@gmail.com