WARIOBA UMENIRAHISISHIA KAZI YA KUIFUFUA TANGANYIKA:MTIKILA
Mjumbe wa
Bunge la Katiba, Mchungaji Christopher Mtikila amesema madai yake ya
zaidi ya miaka 20 kuhusu Serikali ya Tanganyika yamerahisishwa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba na ana imani Tanganyika inarejea muda mfupi
ujao.
Akizungumza
na gazeti hili nje ya viwanja vya Bunge, Mchungaji Mtikila, alisema
amefarijika kuona Jaji Warioba amewafahamisha Watanzania kuhusu ukweli
wa Muungano, hivyo wanaweza kuelewa sasa sababu za yeye kudai
Tanganyika.
"Naamini
sasa Tanganyika inarudi, lakini watu wachache wakizuia safari hii
nitakwenda Mahakama ya Umoja wa Mataifa kudai Tanganyika kwani ndio
ilipigania uhuru na tayari nina mawakili," alisema.
Aliongeza
kuwa Jaji Warioba ameunga mkono hoja ya kudai Tanganyika kwani haiwezi
kupotezwa na watu wachache kwani tayari Zanzibar imejitangaza kuwa ni
nchi huru ndani ya Muungano.
Alisema
Muungano ni suala la hiari, hivyo viongozi wachache wa chama tawala
hawawezi kulazimisha Muundo wa Muungano ambao unapingwa na mamilioni ya
Watanzania.
"Naamini
wale waliokuwa wamechomwa sindano za usingizi wa miaka yote sasa
watafufuka na kuungana na wazalendo waliopigania uhuru wa Tanganyika na
sasa imekuwa koloni la Zanzibar," alisema Mtikila.
Alisema
muundo wa Muungano uliopo sasa wa serikali mbili ni kongwa la utumwa wa
kikundi cha watu wachache ndani ya CCM ambao ndio wananufaika.
Chanzo:Mwananchi