WATANO WAONGOZA KUCHANGIA BUNGENI
Dodoma. Tangu kuanza kwa Bunge Maalumu la
Katiba, Februari 18 mwaka huu, wajumbe watano wanaonekana kuwa ndio
wachangiaji wakuu katika mjadala wa Rasimu ya Kanuni za Bunge hilo.
Bunge hilo la Katiba limekuwa likijadili Rasimu ya
kanuni za Bunge kwa takriban wiki moja sasa na mjadala huo bado hilo
haujamalizika kutokana na mivutano miongoni mwa wajumbe kuhusu baadhi ya
vifungu vya kanuni hizo.
Pamoja na Bunge hilo kuwa na wajumbe 629,
wanaochangia kila mara ni Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole
Sendeka, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, Mbunge wa Nzega
(CCM), Hamisi Kigangwalla, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika
(Chadema) na Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel
Oluoch.
Mbali na kuchangia, wakati mwingine wajumbe hao
wamekuwa wakinyoosha mikono au kusimama kwa lengo la kuchangia, lakini
wanakosa nafasi.
Mfano mzuri ilikuwa ni jana wakati wa mjadala
kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge hilo, wakati Ole Sendeka na Oluoch
waliposimama na kuchangia.
Katika mjadala wa juzi, wajumbe hao wawili kila
mmoja alichangia mara tatu na mara nyingi walipochangia hoja zao
ziliungwa mkono na wajumbe wengi.
Kigwangalla naye hayuko nyuma kwani katika mjadala
wa juzi alipewa nafasi mara mbili kuchangia na wiki iliyopita huchangia
mara mbili kwa siku isipokuwa siku moja tu ambayo alichangia mara
moja.
Mjumbe mwingine ni Mnyika ambaye katika mjadala wa
juzi alichangia mara mbili kuhusu mkanganyiko juu ya kuchagua aina ya
upigaji wa kura.
Naye Serukamba amekuwa mchangiaji wa karibu kila
siku na Ijumaa iliyopita alichangia kuhusu kifungu cha 37 na 38 cha
Rasimu ya Kanuni hizo.
Sasa imekuwa jambo la kawaida kwa wajumbe hao kuchangia katika Bunge hilo.