Bukobawadau

AUDIO YALIOJILI BUNGE MAALUM LA KATIBA APRILI 16,2014

SIKILIZA HAPA CHINI ALICHOKISEMA MH LIPUMBA
  SIKILIZA AUDIO HAPA CHINI TUNDU LISSU AKIFAFANUA KILE ALICHOKIITA VIOJA MCHANGO WA ZITTO KABWE KUHUSU SURA 1 NA 6 YA RASIMU YA KATIBA Ufuatao ni mchango alioutoa Mhe. Zitto Kabwe katika kikao cha leo APrili 16, 2014 cha Bunge Maalum na Katiba kilichopokea maoni ya Wajumbe kuhusu rasimu tajwa hapo juu.

Ndugu Mwenyekiti,

Kamati 12 za Bunge lako tukufu zimeleta Taarifa zake mbele yetu kwa ajili ya maboresho ya Rasimu ya Katiba ili kupata katiba inayopendekezwa itakayopelekwa kwa Wananchi. Maoni ya Kamati yamegawanyika katika aina Kuu 2, maoni ya walio wengi na maoni ya walio wachache. Ndani ya Bunge hili majadiliano pia yamekuwa yenye mwelekeo huo huo na kwa kweli hakuna majadiliano bali majibizano. Sio afya kwa nchi yetu hata kidogo kuwa na Taifa ambalo wawakilishi wake kwenye Baraza nyeti kabisa kama hili wanajibizana badala ya kujadiliana, wanabishana badala ya kuongea na wanatukanana badala ya kushawishiana.

Imefikia hatua zinatoka lugha za kibaguzi bila kukemeana na badala yake tunashangiliana na kupigiana vigelegele. Ubaguzi wa rangi au ubaguzi wa aina
yeyote ile ni sumu kali dhidi ya umoja wetu na Utu wetu. Kauli za kibaguzi, matusi dhidi ya waasisi na dhidi yetu wenyewe ni mambo ya kulaani kwa ukali unaostahili.

Ni muhimu kutambua kuwa tofauti na mabadiliko ya katiba yaliyowahi kufanyika nchini, mchakato huu wa sasa ni wa kipekee ambao unatoa nafasi kwa watanzania wote wa makundi yote kushiriki kwa njia moja ama nyingine. Ni wajibu wetu kutambua kuwa kuwa huu ni mchakato shirikishi ambao umelenga kuleta maridhiano ya makundi yote ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na sio kuongeza mgawanyiko uliopo katika jamii yetu. Endapo tutafanikiwa kuendesha mchakato huu katika hali ya kuheshimiana, kuthaminiana na kwa nia njema sio tu tutaweza kujenga mwanzo mpya wa kisiasa wenye kujali umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa lakini pia tutaweza kuerejesha imani yao kwa dola, serikali, viongozi na wanasiasa, imani ambayo imekuwa ikitoweka na hata kuathiri uhalali wa dola letu mbele ya macho na mioyo ya watanzania na kutishia hatma ya taifa letu. Mwenendo wa mchakato huu una umuhimu wa kipekee kulinusru taifa letu kutoka kwenye dalili mbaya tunazoziona kila siku zikijongea utaifa wetu.

Ndugu Mwenyekiti,

Muungano ni imani. Ni itikadi; ama unaamini katika Muungano au huamini katika Muungano. Muungano ni dhana inayoweza kutekelezwa kwa muundo wa aina yeyote. Pia ikumbukwe kuwa Muundo wowote unaweza kuvunja Muungano iwapo wananchi wa Nchi husika hawautaki.

Hatuoni Nchi ambazo zilikuwa S1 na zimevunjika? Ethiopia iliyozaa Eritrea ilikuwa Serikali 1. Somalia iliyozaa Somaliland ilikuwa Muungano wa Serikali 1. Malaysia na Singapore zilikuwa Serikali ya Shirikisho na zimevunjika. Sudan na Sudan Kusini zilikuwa Serikali 2 na zimevunjika. Kila muundo una hatari ya kuvunjika iwapo hakuna matakwa ya dhati ya watu kuungana.

Muungano ni imani. Ni itikadi. Maneno ya kusema Serikali 3 zitavunja muungano ni maneno ya siasa tu na hayana msingi wa kisayansi. Urusi ilivunjika sababu haikuwa na demokrasia na sio sababu ya idadi ya Serikali.

Ndugu mwenyekiti,

Rasimu ya Katiba ipo mbele yetu. Tuboreshe. Matusi kwa Tume sio jawabu. Vilevile matusi kwa wanazuoni wetu waliobobea sio jawabu. Kero za Muungano zilizoainishwa na Tume ni halisia na hakuna walilotunga. Lakini pia hofu za kuwa na Serikali ya Muungano dhaifu ni hofu halisi, tukibeza tutakuwa mahayawani. Lakini tukitumia hofu hizo kukwepa wajibu wa kuboresha Rasimu tutakuwa mazwazwa. Hakuna hoja isiyo na majibu. Tukae humu ndani tujibu tutoke na muundo imara.

Ndugu Mwenyekiti,

Kuna hoja ya gharama za kuendesha Serikali ya 3 iwapo tutapitisha Rasimu kwa msingi wake huo. Ni hoja ya msingi lakini inajibika. Hivi sasa Serikali ya 3 imejificha, ipo. Gharama ni zile zile. Sio lazima tuwe na Marais 3, hatujengi ikulu Mpya. Gharama za Wizara za Muungano zipo ndani ya Bajeti ya sasa ya Serikali mbili. Hakuna taasisi Mpya zaidi ya Tume za uwajibikaji nk. Lazima tuwe na Rais wa Tanganyika? Hapana.

Ndugu Mwenyekiti,

Tuwe na Rais 1 tu, Rais wa Jamhuri ya Muungano na Wakuu wa Serikali za Washirika watakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Unaweza kuwaita unavyopenda lakini Mimi nashauri tuwaite Mawaziri Wakuu na watokane na Chama chenye Wawakilishi wengi kwenye Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na chenye wawakilishi wengi kwenye Baraza la wawakilishi la Zanzibar.

Ndugu Mwenyekiti,

Uhuru wa Zanzibar ulipopatikana Zanzibar ilikuwa ‘parliamentary democracy’ na vivo hivyo Tanganyika ilipopata Uhuru. Zanzibar ilipinduliwa Serikali ya Wazanzibari chini ya Waziri Mkuu Mohamed Shamte. Sultan Jamshid alikuwa Mkuu wa Nchi tu (constitutional monarchy). Tanganyika kabla ya Jamhuri Mwalimu Nyerere na baadaye Mzee Kawawa walikuwa Mawaziri Wakuu. Malkia alikuwa Mkuu wa Nchi. Sasa tufanye tuwe na Mkuu wa Nchi mmoja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Chombo cha utendaji cha Zanzibar na Tanganyika viongozwe na Mawaziri Wakuu. Rais mmoja, Nchi moja na Serikali 3.

Hakuna gharama inayoongezeka, mambo ya Muungano yanapungua. Isipokuwa katika mambo ya Muungano kwenye Rasimu tuongeze shughuli za uratibu wa uchumi, kodi kadhaa na tuwe na masuala ya uratibu (concurrent) kama usafiri wa anga, mawasiliano, Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii na Usimamizi wa Maliasili za Taifa. Kwa hiyo tuwe na Mambo ya Muungano yatakayosimamiwa na Serikali ya Muungano, Mambo yasiyo ya Muungano yatakayosimamiwa na Washirika na mambo ya uratibu (concurrent matters) yatakayosimamiwa kwa pamoja na Serikali za Washirika na Serikali ya Muungano.

Ndugu Mwenyekiti,

Rasimu inapendekeza Muungano wa kisiasa bila Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Sarafu (Monetary Union). Chanzo cha mapato kilichopendekezwa na Tume hakitoshi kwa shughuli za Serikali imara ya Muungano isiyo egemezi au tegemezi.

Katika mwaka wa fedha 2012/2013 chanzo hiki (tena ushuru wa bidhaa na huduma – local and imports) kiliingiza Tshs 1.13 trilioni wakati matumizi ya Wizara za Muungano katika mwaka huo wa fedha ilikuwa Tshs 4.2 trilioni. Katika mwaka 2013/2014 chanzo hiki kinatarajia kuingiza Tshs 2 trilioni wakati matumizi ya Wizara za Muungano ni zaidi ya Tshs 5.3 trilioni. Hivyo ni lazima tuiboreshe rasimu kwa kuongeza vyanzo vya mapato ya Muungano ili kuwezesha Serikali ya Muungano kuwa imara, inayojitegemea na itakayoweza kuwezesha Serikali za Washirika kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma kwa wananchi

Turekebishe kwa kuboresha Rasimu maana ni lazima tuwe na sera za pamoja za fedha (monetary policy) kama tunataka Muungano imara. Baadhi ya hatua hizi zipo tayari ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hivyo napendekeza vyanzo vya mapato ya Muungano kuboreshwa ili Dola iweze kusimamia Uchumi, navyo ni;

1. Ushuru wa Forodha,

2. Mrahaba wa uvunaji wa Rasilimali za Nchi,

3. Ushuru wa Bidhaa na Huduma zilizozalishwa nje ya Tanzania,

4. Mapato kutoka kwenye kampuni za kibiashara za Serikali ya Muungano, Mamlaka za Usimamizi zenye maduhuli, maduhuli kutoka Wizara za Serikali ya Muungano na Gawio la Benki Kuu ya Tanzania.

Ndugu Mwenyekiti,

Mapato haya haya ya sasa yanaweza kugawanywa kwenye Muundo wa Serikali 3 na tusiongeze kodi hata senti moja na Muundo Mpya ukafanya kazi. Hatuhitaji Tshs 3 trilioni za ziada kwa ajili ya Serikali Mpya. Bajeti ya Serikali ya mwaka huu wa fedha 2013/2014 ni shilingi 18 trilioni, kati ya hizo mapato ya ndani ni shilingi 11 trilioni na katika mapato hayo ya ndani shilingi 10 trilioni ni kodi. Gharama za kuendesha Wizara za sasa za Muungano ni tshs 5.6 trilioni lakini kati ya hizi Tshs 3.3 trilioni malipo ya Deni la Taifa. Hakuna trilioni 3 za ziada, za kazi gani? Hata kama fedha hizo zikihitajika, zisitutishe maana zipo.

Hatuhitaji kuongeza kodi, tunahitaji kuondoa ubadhirifu na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima. Tunapoteza Mapato lukuki kwenye misamaha ya kodi (theluthi ya mapato ya idara ya forodha inasamehewa, sawa na Tshs 2 trilioni kwa mwaka), ukwepaji wa kodi (asilimia 5 ya Pato la Taifa inapotea, sawa na Tshs 2.3 trilioni kwa mwaka ) na ubadhirifu mwingine uliokithiri. Hivyo udhibiti wa asilimia 50 tu wa misamaha ya kodi na ukwepaji kodi unaongeza mapato zaidi ya trilioni 2 ambazo Serikali ya Muungano inaweza kugawa kwa Washirika kwa miradi maalumu ya kitaifa. Hivi sasa kamati ya PAC (Ya Bunge la Jamhuri ya Muungano) imeanza utaratibu wa ukaguzi wa misamaha ya kodi na kuweka wazi kwa umma ukaguzi huo ili kudhibiti misamaha holela. Vilevile kwa kibali maalumu cha Spika wa BUNGE, PAC imeanza uchunguzi (an inquiry) kuhusu ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya kimataifa. Hizi ni juhudi za kuongeza mapato mpaka kufikia uwiano wa 25% ya mapato ya kodi kwa GDP (tax GDP ratio).

Ndugu Mwenyekiti,

Serikali 3 zitaweka Uwazi wa Mapato na zitaweka Uwajibikaji kwa serikali kutazamana zenyewe. Hizi za sasa zimejaa lawama sababu hakuna Uwazi. Naomba kuuliza, fedha za mapato kutoka TCRA lini zimeenda Zanzibar? Mawasiliano ni jambo la Muungano. Lini fedha za TCAA zimeenda Zanzibar? Gesi Asilia ni jambo la Muungano, hivi Zanzibar wanapata mgawo wa asilimia ngapi kutoka gesi ya Songosongo? Anga ni jambo la Muungano, fedha za chenji ya rada zimerudi, Zanzibar imepata kitabu hata kimoja? Mimi ni mwenyekiti wa PAC, najua haya ninayosema na hamtayamaliza katika S2 sababu ya confusion ya Muundo. Tatu ni Muundo unaoeleweka. Tukiamua zifanye kazi zitafanya.

Ndugu Mwenyekiti,

Hoja ya gharama isitumike kutisha wananchi kwa sababu ni hoja ‘very relative’ na ninashangaa sana kuona baadhi ya wasomi, wachumi wanaongea suala hili bila kutafakari kwa kina. Unaweza ukawa na Serikali 1 ukawa na gharama kubwa zaidi kuliko Serikali nne. Gharama za kuendesha shughuli za usalama zitakuwa nafuu zaidi kwenye Serikali 3 kuliko Serikali 2 kwani kwenye Serikali 3 kila mtu atakuwa amefurahi, ndani ya 3 kuna 2 na 1. Zikiwa mbili, wa 3 watanuna maana ndani ya 2 hakuna 3. Watu wote wakiwa na furaha vitendo vya uhaini dhidi ya Dola vinapungua. Lakini Muungano ukivunjika gharama za Ulinzi wa nchi zote mbili zitakuwa kubwa sana na lazima mabeberu wataingia kati upande wa mmoja wetu. Hivyo nashawishi wajumbe tuulinde Muungano wetu kwa kuufanyia marekebisho makubwa ya kimuundo na kuunda Chombo kingine cha utendaji kwa masuala yasiyo ya Muungano ya Tanganyika.

Muungano kuvunjika?

Ndugu Mwenyekiti,

Kuna ambao wanaamini kabisa kwamba kuifukua Tanganyika ndani ya Muungano kutavunja Muungano na hivyo wanataka S2 ziboreshwe. Kuna ambao wanataka S2 kwa kufuata mkumbo tu na kwamba ni ‘sera’ ya chama chao.

Kuna ambao wanaamini kabisa kwamba S3 ndio njia ya kuimarisha Muungano na kuufanya endelevu kwa kuweka uwazi katika muundo wa Muungano na usawa wa Washirika. Kuna ambao S3 ni njia ya kutokea kuelekea kuvunja Muungano maana ama hawaamini katika muungano au hawana itikadi yeyote (ideological bankruptcy).

Wanaong’ang’ania S2 wakidhani wanalinda Muungano watambue kuwa wanawapa nguvu S3 wanaotaka kuvunja muungano.

Ni busara na maono ya mbali kwamba wale wanaoupenda Muungano (ideologically clear people) kuhakikisha S3 zenye Serikali imara ya muungano. Usipotaka mabadiliko, mabadiliko yatakutaka wewe.

Nataka Muungano. “I am a Unionist.” Lakini nataka Muungano unaoeleweka, wenye uwazi na uwajibikaji. Muungano wa usawa. Muungano endelevu.

Mimi ni Mtanzania.

Dodoma, 16.04.2014
Next Post Previous Post
Bukobawadau