OKUBEGA, OKUHA,OKUHONGA:UTAMADUNI WA KUTOA MIONGONI MWA WAHAYA.
Siwezi kudai kuifanyia utafiti wa kina sana dhana hiyo ya ‘upaji’ ambayo ndiyo okuha,
miongoni mwa Wahaya. Lakini hilo haliwezi kuwa sababu toshelezi ya
kunizuia kuijadili kwa kutumia uzoefu wangu wa miaka mingi kiasi kama
mwanajamii husika.
Umuhimu wa okuha, hauhitaji kupigiwa kinubi wala baragumu. Upana wake, kama msamiati, unatosha kutuonyesha jinsi okuha kulivyokuwa ni tunu inayothaminiwa sana katika utamaduni wa Wahaya. Kwa hakika, okuha ni
dhana ambayo haina mshindani katika ‘kamusi ya Kihaya’ kwa wingi wa
maana zake mbalimbali, ambazo baadhi yake zinaendelea kusikika
zikitumiwa hadi leo. Pamoja na kutokuwa gwiji wa lugha ya Kihaya, mimi binafsi nimeweza kukusanya maana zisizopungua dazeni kuhusiana na maana hizo. Kwa kuzitaja tu, maana hizo ni pamoja na okutangilila, okutwela, okukulata, okulongola, okuganuza, okugabila, okugaba, okubegela, okushalila, okuzilima, okubisila, okuhonga, okutekela, okulozya, okubegana, okueleza, na hata okuhao. Inawezekana kuwa yapo maneno mengine ya Kihaya yenye msamiati mpana kama hilo la okuha, lakini ninaamini kwamba yatakuwa ni machache sana.
Mbali na vitenzi nilivyoweza kuviorodhesha hapo juu na kuvihusisha na ‘kutoa’ tunu fulani zipelekwe au kuhamishiwa kwa mtu, ukoo, tabaka au watu wengine, vipo vitenzi ambavyo, japo sio kwa ukaribu wa kiwango cha uwazi, vinaweza kunyumbuliwa na kujenga taswira isiyokuwa mbali na dhana ya upaji. Kwa mfano, okulela maana yake ni kulea. Ni wazi kwamba muktadha wa neno hilo unaonekana zaidi katika mwelekeo wa upaji, okuha.
Hii ni kwa sababu kulea au kuhudumia, ni kitendo kinachohusiana kwa karibu na kutjiolea muda, raslimali na mapenzi kwa mtu mwingine aliye na hali ya kupungikiwa au kutindikiwa na amali fulani katika maisha yake. Mwisho wa siku, kusema kweli, kulea ni kumpa mtu kitu ambacho kukikosa kwake kitu hicho kungelimsababishia mlengwa unyonge na mapungufu kiafya au kumpotezea maisha kabisa. Hebu tulithibitishe jambo hili kwa mifano michache zaidi.
OKUBEGA:Okubega au okubegela ni mila iliyotekelezwa na Wahaya katika ngazi ya kaya, hususan wakati wanafamilia wanajipatia mlo wao. Vitendo vya okubega viliimarisha upendo katika kaya na kuwatia hamasa wanakaya walioonyesha nidhamu, uadilifu, utiifu na utendaji bora wa majukumu.
Japokuwa hapakuwepo na mipaka maalumu kuhusu nani ampe nani zawadi ya kitoweo (omukubi)
kama ishara ya shukrani au pongezi kwa tabia nzuri, adabu na utendaji
uliotukuka, ni watu wa rika andamizi zaidi ndani ya kaya (hasa bibi),
walioidhibiti zaidi mila hii ya okubega.
Kwa kawaida, kitoweo (samaki,
nyama au maziwa) kiligawiwa katika utaratibu wa hatua kadhaa. Katika
hatua ya awali, bibi (mgawaji wa mafungu ya kitoweo) alimgawia kila
mwanakaya fungu lake stahiki, kulingana na rika au hadhi yake ndani ya
kaya. Kadiri mlo ulivyoendelea, alifanya mgawo mwingine mdogo. Kwa kawaida, mgawo huu nao uliwahusisha karibu watu wote wa kaya waliojumuika pamoja kwa chakula.
Lakini
kulikuwapo na hatua nyingine zaidi, iliyohusu ugawaji wa fungu maalum
ambalo bibi alikuwa amelitenga kando kwa madhumuni ya kuligawa kama tuzo
kwa kuzingatia vigezo na sifa maalum. Mara nyingi, utoaji wa mgao huu
wa ziada uliandamana na maneno ya kukaripia, kusifia, kuhimiza, kufundisha, kuonya, kuadabisha, kuhamasisha na kuelekeza.OKULONGOLA
Okulongola, ni kitendo cha hiari alichokifanya mtu kwa kusudi la kumuonyesha mwenzake jinsi alivyoridhishwa na kitendo kingine ambacho yeye mwenyewe alipata kutendewa huko nyuma. Waingereza hukiita kitendo kama hicho reciprocity. Sisi hatuwezi kukosea kukiita Nipe - Nikupe. Ni kitendo cha kurudisha fadhila.
Mfano mzuri hapa, ni mila nyingine ya Kihaya, ambayo kwayo mwanamke hutoka na kwenda porini (wakati wa msimu wa musenene) na kukamata senene kwa ajili ya mumewe. Baada ya kuwaandaa wale senene na kuwawasilisha kwa mumewe kwa wakati muafaka, hutazamiwa mume naye aonyeshe kufurahi na kuridhishwa na juhudi za mkewe, kwa kumnunulia mkewe zawadi maalum, hususan doti ya kitenge au khanga. Akifanya hivyo, anakuwa ametekeleza mila ya okulongola. Mambo yalikuwa vivyo hivyo kwa maswahiba walioshibana.
OKUHONGA;Katika maana yake ya kiasili, Okuhonga katika jamii ya Wahaya, hakukuhusiana na kutoa rushwa, kufanya vitendo vya kifisadi au kununua mapenzi ya mwanamke. Enzi kabla ya ujio wa Wazungu walioleta na kutupandikizia imani na taratibu zao za kumuabudu, kumcha na kumtukuza Mungu, nasi Waafrika tulikuwa na taratibu zetu za kuwaenzi miungu yetu.
Okuhonga, kulikuwa
ni utaratibu wa kuwatolea miungu sadaka na zawadi mbalimbali ili
iwapendeze kututunuku baraka na kutujalia neema na rehema tele katika
maisha yetu ya kila siku. Na katika jambo hili, Waafrika
hatukutofautiana sana na Wazungu wa Ulaya, karne za kale (eila lya kalanda).
Miungu ya Wahaya, ilikuwa ni pamoja na kasi (mungu wa ardhi na kilimo), ilungu (mungu wa nyika na wanyamapori), lyangombe (mungu wa mifugo, hasa ng’ombe), mugasha (mungu wa Ziwa Lweru- Victoria), nyakalembe, (mungu wa ustawi wa wanawake na mambo ya uzazi), n.k.
Katika Agano la Kale, tunasoma sana habari za dhabihu na matambiko ya kuchoma na kuteketeza kwa ajili ya Mungu? Wahenga wetu nao hawakuwa mbali katika kuwatambikia miungu yao ili iwajalie neema walizozihitaji ili kukidhi shida zao lukuki maishani mwao na kuondokana na maangamizi yaliyowazinga? Na ndiyo tunavyofanya hata sisi leo, chini ya madhehebu yetu mbalimbali - kwa kutoa zaka na sadaka kwa ajili ya kusifu na kushukuru ? Kimsingi, ni dhana ile ile?
Kwa kuhitimisha maelezo haya ya utoaji na upaji kwa ajili ya miungu, okuhonga, Wahaya hawakukosa kukiri imani yao katika uweza wa miungu hao. Kila walipobanwa na matatizo na kuelekea kukosa suluhu ya kutokea, walisikika wakiungama na kujinyenyekeza: “ tubihongele mukama mungu”.
Maelezo ya mifano hiyo hapo juu, yatoshe kuonyesha jinsi utamaduni wa Kihaya ulivyosheheni utajiri mkubwa katika nyanja ya ukarimu na upaji, okuha.OKUTANGILILA ;Katika ‘nchi ya Wahaya’ (Buhaya), pengine hakuna mila ambayo imeenea na kuzingatiwa zaidi kuliko Okutangilila. Huwezi kuingia katika mji wa Muhaya ukatoka bila kutangililwa, yaani kulakiwa kwa kahawa au pombe, kama ishara ya ukarimu na upendo.
Hata awe masikini kiasi gani, Muhaya atafanya juhudi kubwa kuhakikisha anaweka nyumbani kwake akiba ya kahawa (emwani) za kutafuna kwa ajili ya wageni wanaoweza kumfikia hata bila taarifa; haijalishi wageni hao wanatoka masafa ya mbali au karibu. Kaya masikini iliyotembelewa na mgeni inaweza kutindikiwa na huduma nyingine yoyote, ikiwa ni pamoja na kitoweo, kiasi cha mgeni huyo kulazimika kula chakula ‘maluma’, jambo ambalo ni fedheha ya kutosha kwa mwenyeji, lakini kahawa ya mgeni kutafuna itapatikana tu, japo iwe nusu ya kibaba. Miaka hii, pombe, hasa gongo (enkonyagi), inatumika zaidi kukidhi haja, lakini mila inakuwa timilifu ikihusisha pia kahawa za kutafuna.